*Ni msanii aliyedokezwa na gazeti hili wiki iliyopita

*Mrembo akiri walikuwa pamoja kutangaza utalii

*Asisitiza sehemu kubwa ya bajeti ilitoka wizarani

*Yaelezwa ndicho kilichomkera Rais Kikwete Marekani

Msanii wa filamu za Tanzania (Bongo Movie), Aunty Ezekiel Grayson, amekaa Marekani kwa siku 14 akiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kwa kile kinachoelezwa kuwa wamekwenda kupumzika na wakati huo huo kumtumia kutangaza vivutio vya utalii ili kuvutia watalii wengi kuja nchini, JAMHURI inathibitisha.

Binti huyo wa mwanasoka mahiri wa zamani aliyechezea Simba na Yanga kwa nyakati tofauti, Ezekiel Grayson (Jujuman), amethibitisha kwa kusema: “Nilikuwa Marekani na Nyalandu.”

Kiasi cha fedha kilichotumiwa kwenye utangazaji huo wa kitalii kimeendelea kuwa siri, lakini chanzo chetu cha habari kimezungumza kwa ufupi kwa kusema, “Ni pesa ndefu (fedha nyingi), inawezekana zikafikia hata Sh milioni 100 au zaidi.”

Nyalandu alikuwa nchini Marekani pamoja na msanii huyo, ilhali Rais Jakaya Kikwete naye akiwa huko huko, lakini akiwa hana taarifa za uwepo wake.

Hatua hiyo inatajwa kuwa ilimkasirisha Rais Kikwete, hasa kwa kuona Nyalandu amekuwa akienda Marekani karibu kila wiki na hivyo kuacha vikao vya Bunge Maalum la Katiba ambalo lilifikia tamati Alhamisi iliyopita.

Akizungumza na JAMHURI, Aunty alikiri kuwapo Marekani kwa wiki mbili kuanzia Septemba 10, mwaka huu, wakifanya kazi ya kutangaza shughuli za utalii zilizoandaliwa na vijimamboblog.spot.

“Tulikuwa na Waziri Nyalandu na sehemu kubwa ya bajeti ya kutangaza utalii ilitolewa na Serikali. Kwenye ile party (hafla) tulialikwa na waziri ili nasi tuelezee utalii wa nchi,” anasema Aunty.

Ameendelea kusema: “Baadaye tukasikia Rais Kikwete naye yupo Marekani na tukaenda kuungana naye, kabla ya kurejea nchini. Tulirudi Tanzania Septemba 24.”

Msanii huyo alipoulizwa kama ana uhusiano wowote wa ‘kijamii’ na Waziri Nyalandu, aling’aka na kusema kilichompeleka ni shughuli za utangazji utalii tu.

Aunty anasema hakuwa msanii pekee aliyekwenda na Nyalandu huko ughaibuni: “Tulikuwa wasanii wawili, mimi na (anataja jina). Hebu ngoja, nitakutajia hoteli na ukumbi ambao tulikuwa tukitangazia utalii.”

Jina la msanii huyo wa pili tunaendelea kulihifadhi kwa kuwa hatujazungumza naye, lakini habari za uhakika zinasema bado anaendelea kuburudika nchini Marekani kwa ufadhili wa Nyalandu.

Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Nurdian Chamuya, amezungumza na JAMHURI kuhusu ziara hiyo ya aina yake na kusema: “Ukweli ni kwamba Waziri Nyalandu alikwenda Marekani. Lakini wakati wa kupangwa au wakati waziri anasafiri, mimi sikuwa ofisini Dar es Salaam. Nilikuwa Arusha kwenye maonesho ya utalii. Kuhusu ziara hiyo naomba mumtafute Msaidizi wa Waziri, Bwana Nkuwi.”

Kwa upande wake, Imani Nkuwi amethibitisha kuwapo kwa ziara ya waziri nchini Marekani. Hakutaka kuingia kwenye undani wa suala hilo, badala yake akasema: “Kwa hatua iliyofikia, anayeweza au mwenye mamlaka ya kuzungumzia ziara hiyo ni Katibu Mkuu wa Wizara, Maimuna Tarishi.

“Hata kama najua, mimi mambo yote niliyafikisha wizarani kwa Katibu Mkuu, hivyo kwa ushauri tu kama unataka kupata undani wa ziara hiyo wasiliana na Katibu Mkuu.”

Tarishi hakupatikana kwa simu yake ya mkononi. Duru za uchunguzi zinaonesha kuwa kwa sasa Wizara ya Maliasili na Utalii ni kama ‘inakufa’ kwa kuwa Waziri Nyalandu amekuwa hapatikani ofisini, na pia haelewani na watendaji wengi, akiwamo Tarishi.

Waziri huyo amekuwa akitajwa kuwa miongoni mwa viongozi wa Serikali wanaofuja fedha za umma, huku mambo yake mengi akiyatekeleza kwa fedha zinazotokana na kuziamuru taasisi na idara zilizo chini ya wizara yake, kumlipia. Wabebeshwaji wakuu wa malipo ni Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA). Pia fedha nyingine zimekuwa zikichotwa kutoka kwenye Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori.

Pamoja nao, gharama zake nyingine zimekuwa zikibebwa na kampuni binafsi hasa zenye kusaka maslahi, ikiwamo ya TGTS ambayo imediriki kwa nyakati kadhaa kumpa ndege kwa ajili ya matumizi yake binafsi na ya kiofisi. Ni kampuni hiyo hiyo ambayo hivi karibuni wamiliki wake Wamarekani aliwazawadia kuua wanyamapori 704 kwa kutumia Leseni ya Rais.

Ukaribu wa Nyalandu na Wamarekani umekwenda mbali zaidi kwani ni hivi karibuni, akiwa nchini humo, alikusudia kuwaleta askari wastaafu wa Jeshi la Marekani kuja nchini katika kile alichosema ‘kusaidia kupambana na majangili’. Mpango huo ulipingwa na Ikulu pamoja na watumishi katika Wizara ya Maliasili na Utalii, kwani ulionekana kama ni wa kuwakaribisha mamluki ambao wanaweza kuhatarisha usalama wa nchi.

Miongoni mwa walioupinga ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Herman Keraryo; ambaye ameshika wadhifa huo kutokana na uamuzi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Kuna habari kwamba Nyalandu ameanza kumchukia Keraryo, akitaka Paul Sarakikya na Julius Kibebe ambao wamehamishwa, ndiyo waendelee kushika nafasi hizo nyeti. Nyalandu amewazuia kwenda kuripoti NCAA na TAWIRI ambako wametakiwa waripoti kwa ajili ya kupangiwa kazi nyingine.

Waziri huyo ana vyumba maalum katika hoteli kadhaa za kitalii kwenye majiji ya Arusha na Dar es Salaam. Inaelezwa kwamba imekuwa nadra mno kuonekana ofisini kwake Dar es Salaam; na hata anapotaka kuzungumza na waandishi wa habari, amekuwa akitumia hoteli za kitalii ambazo malipo yake huanzia Sh milioni 3 kwa saa kadhaa. Anafanya hivyo, ilhali wizarani kwake kukiwa na ukumbi wa kisasa wenye viyoyozi na huduma zote za kuendeshea mikutano.

Chanzo cha habari kutoka kwenye msafara wa Rais Kikwete nchini Marekani, kimesema kiongozi huyo mkuu alikasirishwa na hatua ya Nyalandu kwenda nchini humo na wasanii kinyemela na kuendelea na shughuli zisizokuwa kwenye ratiba ya Rais.

Chanzo chetu cha habari kinasema Nyalandu amekuwa hana wasiwasi wowote wa kupoteza nafasi yake kutokana na kujiamini kwake kuwa yuko karibu mno na Rais Kikwete na baadhi ya mawaziri waandamizi.

Wakati hayo yakitajwa upande wa Rais Kikwete, kuna habari zisizotiliwa shaka kuwa wabunge kadhaa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wengine kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wanajiandaa kuibana mamlaka ya uteuzi kuhakikisha Nyalandu anang’olewa.

“Haiwezekani kashfa zote hizi zikawa zinaandikwa, hazikanushwi na bado huyu mtu anaendelea kuwa waziri. Tunasubiri Bunge la Novemba tuibane mamlaka ya uteuzi imuondoe. Huyu mtu hafai kuwa waziri. Tunataka tujue hiki kiburi anakitoa wapi,” amesema mmoja wabunge aliyesema ameanza kuandaa hoja ya kumng’oa waziri huyo.

Pamoja na Nyalandu, Naibu wake, Mahamoud Mgimwa, naye yuko kwenye hatihati kutokana na kukumbwa na kashfa ya ugawaji vitalu vya miti.

Kwa siku kadhaa sasa, vyombo vya habari vimekuwa vikiandika kashfa hiyo, huku Mgimwa akitajwa kama miongoni mwa wahusika wakuu ambao, ama wamejichotea, au wamefanikisha kuwasaidia marafiki zao kujipatia vibali vya ukataji miti kwa ajili ya mbao.

Kwa Nyalandu idadi ya kashfa zinazomkabili ni kubwa mno. Kashfa ya karibuni ni mpango wake wa kuigomea Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma iliyoamuru kuhamishwa kwa baadhi ya watumishi wa Maliasili na Utalii.

Waziri huyo aliandika dokezo akiwazuia watumishi hao, akiwamo Paulo Sarakikya, kwenda walikopangiwa. Hadi wiki iliyopita, Sarakikya alikuwa hayupo katika kituo chake kipya cha kazi.

Bado wachunguzi wa mambo wanashindwa kubaini nguzo inayompa jeuri Nyalandu, lakini kuna habari kwamba anapata nguvu kubwa kutoka kwa mawaziri wawili wanaotajwa kuwania urais.

Kashfa nyingine inayomtikisa Nyalandu ni ya kutoa Leseni ya Rais kuua wanyampori 704; ‘zawadi’ ambayo aliwapa marafiki zake Wamarekani wa familia moja.

Gazeti JAMHURI lilifanya kazi kubwa ya kuandika habari hizo na hivyo kufanikisha kuokoa wanyama hao 700. Pamoja na habari hiyo, JAMHURI ilichapisha picha zilizowaonesha watoto wadogo wakiwa na bunduki wakiwinda katika kitalu kinachomilikiwa kihalali na kampuni ya Green Miles Safaris (GMS). Kifungu cha 43(3) cha Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 kinazuia watoto chini ya miaka 18 kuwinda.

Waziri Nyalandu amekiuka kifungu kinachoweka ukomo wa idadi ya vitalu ambao ni vitalu vitano kwa kampuni. Ameruhusu TGTS kumilikishwa vitalu vinane pamoja na eneo la wazi na hivyo kukiuka Kifungu cha 38(7) cha Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009.  Kwa kawaida kitalu chochote kinapobaki wazi sharti kitangazwe kwanza na waombaji washindanishwe katika mfumo na utaratibu ulio wa haki na uwazi [Kanuni ya Uwindaji wa Kitalii 18(1)].

Pia amevunja sheria hiyo kwa kuruhusu uwindaji wa kitalii kufanyika eneo la Makao, sehemu ambayo haijatengwa kama kitalu.

Kashfa nyingine kwa Nyalandu ni mpango wake wa kusafiri kwenda nchini Afrika Kusini  na kufanya mazungumzo na kampuni ya African Parks Network (APN) kwa ajili ya kuikabidhi uendeshaji wa Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu.

Kwenye mpango huo alishirikiana na mmoja wa wakurugenzi katika Bodi ya APN ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, James Lembeli. Kwa mara nyingine, gazeti hili lilifichua kashfa hiyo na kwa sasa bado wanatafuta mbinu nyingine za kuuendeleza.

Kwenye mlolongo wa kashfa hizo, Nyalandu alikuwa na mpango wa kufungua mpaka wa Bologonja unaotenganisha Tanzania na Kenya ili kuruhusu watalii kutoka Kenya kupita aneo hilo. Mpaka huo ulifungwa wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa kuzingatia maslahi mapana ya kiuchumi ya Taifa.

Kwa mara nyingine, JAMHURI ilifichua mpango huo na kuchapisha nyaraka mbalimbali na hatimaye kufanikiwa kuuzima. Waziri Nyalandu anakabiliwa na kashfa ya kujihusisha na ujangili mkoani Singida.

Nyaraka ambazo JAMHURI inazo, zinaonesha kuwa Juni 11, 2012 Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwanyonye, Rehema Manji, alimwandikia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida akilalamikia kutishiwa kwa bastola.

Anasema, “Napenda kutoa taarifa ya kuvunjiwa geti/kizuizi cha mazao na kutishiwa kwa silaha aina ya bastola na mtu ndani ya gari Na. T505 BKM usiku wa kuamkia leo tarehe 11/04/2012 yaani saa 6.00 usiku katika eneo la Kijiji cha Mwanyonye na Kinyeto.”

Aliongeza kuwa; “Pia tumefungua kesi Na. IR/SI/1570/2012, aidha tangu usiku huo hadi sasa geti liko wazi na magari ya mizigo yanapita bila kukatiwa risiti za ushuru.”

Siku hiyo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Singida alipokea waraka wa Meneja wa Mkoa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Singida ukisema; “Nakiri kupokea barua yako ya tarehe 11/04/2012 yenye kumb. SDC/K.2/1/PART ‘E’/45 kuhusiana na somo tajwa hapo juu. Napenda kukufahamisha kwamba mmiliki wa gari Na. T505 BKM ni ndugu Lazaro Samwel Nyalandu, mwenye namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN: 105-059-701).”

Barua hiyo ilitiwa saini na Mnubi kwa niaba ya Meneja wa Mkoa wa TRA Mkoa wa Singida. Pamoja na tuhuma hizo za ujangili, rekodi hazioneshi kama Nyalandu alishawahi kuwajibishwa kwa jambo hilo.

Katika hatua nyingine, wiki iliyopita watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii waliotumwa, walinunua nakala za Gazeti JAMHURI mjini Dodoma na kuziteketeza. Pamoja na Dodoma, JAMHURI iliadimika katika miji ya Arusha na Moshi ambako masuala ya utalii yanafuatiliwa na wasomaji wengi.

Habari za uhakika zilizopatikana na kuthibitishwa na mawakala katika miji hiyo zilisema watumishi hao (majina tunayo) walinunua nakala hizo kwa maelekezo waliyodai yametolewa na kiongozi mkubwa wizarani.

Katika toleo hilo Namba 156, habari kubwa ilikuwa: “JK amchoka Nyalandu”. Habari hiyo ilieleza kwa urefu ziara ya Nyalandu nchini Marekani akiwa na wasanii wa Bongo Movie, akiwa amemkwepa Rais Jakaya Kikwete.

Pia habari hiyo ilisheheni kashfa chache kati ya nyingi zinazomkabili Nyalandu zikiwamo za kutoa Leseni ya Rais kwa marafiki zake Wamarekani kuua wanyamapori 704; kuhusishwa kwake kwenye matukio ya ujangili; kugawa vitalu kinyemela bila kufuata sheria; kung’ang’ana kufungua mpaka wa Bologonja; kukomalia uuzaji wa hifadhi za Taifa na mapori mbalimbali kwa asasi ya makaburu ya African Parks Network (APN) akishirikiana na Mjumbe wa Bodi ya APN, James Lembeli; na kashfa ya kutoonekana ofisini baada ya kuhamishia ofisi na makazi yake katika hoteli za kitalii katika miji ya Arusha na Dar es Salaam.

Hii ni mara ya tano kwa JAMHURI kuandika habari, na kisha kununuliwa nakala zote kunakofanywa na walioandikwa.

By Jamhuri