Azam Yafanikiwa Kutetea Ubingwa Kombe la Kagame Yaitandika Simba 2-1

AZAM FC imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa Kombe la Kagame baada ya jana Ijumaa kuifunga Simba mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Katika mchezo huo ulioanza majira ya saa 12 jioni, Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 32 kupitia kwa Shaban Idd Chilunda aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Ramadhani Singano ‘Messi’.

Simba ilisubiri mpaka dakika ya 62 kusawazisha bao hilo ambapo straika wake mpya, Meddie Kagere alifunga bao hilo akiwa ndani ya eneo la hatari la Azam na kumchambua vizuri kipa. Dakika sita mbele, Azam ikaongeza bao la pili kwa mpira wa faulo uliopigwa na beki, Aggrey Moris na kujaa moja kwa moja langoni mwa Simba na kumuacha kipa Deogratius Munish ‘Dida’ akiruka bila ya mafanikio.

Kutokana na ushindi huo, Azam ambayo inanolewa na Kocha Mholanzi, Hans van Der Pluijm imekabidhiwa kombe na dola 30,000, Simba ikiwa nafasi ya pili, imeondoka na dola 20,000 na Gor Mahia ikakabidhiwa dola 10,000 kwa kushika nafasi ya tatu.

https://youtu.be/Q3_ik6hWI_w