Helikopta za uokoaji ni kitu kingine muhimu sana kinachompasa Rais John Magufuli awafanyie Watanzania baada ya kazi nzuri kwenye Bombardier, Dreamliner na Airbus.

Tunahitaji kwa uchache helikopta moja ya uokoaji kwa kila kanda. Tuanze na kanda kabla ya mkoa kwa mkoa. Tunazo kanda sita au saba kama sikosei.

Tunaweza kutumia kanda hizi hizi au zikaundwa kanda mpya za uokoaji kulingana na ukaribu na urahisi wa kufikika kwa eneo.

Oktoba na Novemba, mwaka jana moto uliwaka katika misitu ya California, Marekani kwa wiki zaidi ya mbili. Fikiria tunapata moto kama huo wa kuwaka wiki mbili kwenye hifadhi zetu tunazotegemea kwa utalii. Nini itakuwa manusura yetu?

Hata milima huwa inaungua. Fikiria tunapata moto kama huo Mlima Kilimanjaro. Ipi itakuwa hatima ya tukio kama hilo? Ni gari lipi la Zimamoto au kifaa kipi cha Zimamoto kitafanya kazi hiyo? Tunapaswa kujiandaa.

Kwa sasa tuna majengo ambayo yanafikia hadi ghorofa 30 hasa kwa Dar es Salaam. Fikiria moto unawaka ghorofa ya 10 na kuzuia watu wa juu kushuka chini. Tutawasaidiaje watu hawa kutoka huko juu?

Tusidanganyane. Tulipata aibu sana tulipositisha uokoaji kule Ukara kwa sababu ya giza. Nani anajua labda tungekuwa na helikopta za uokoaji zenye taa kali (spot light) tungewapata baadhi ya Watanzania wakiwa hai kwa usiku ule, hivyo tukaokoa maisha yao?

Tupate helikopta, na uwezo wa kuipata moja kila kanda tunao. Tumenunua Dreamliner moja kwa dola milioni 224.6 ambazo ni karibia Sh bilioni 512. Na uzuri ni kuwa hawa hawa wanaotuuzia ndege za abiria wanatengeneza helikopta pia.

Mfano Airbus wanatengeneza helikopta ndogo (light helicopter), wanatengeneza saizi za kati (medium helicopter) na zile kubwa kabisa H155. Za bei ya chini zinaanzia dola milioni 5 wakati zile za saizi ya kati zinauzwa hadi dola milioni 11 ambazo ni kama Sh bilioni 24 hivi kwa kila helikopta. Tupate hizi za saizi ya kati za Sh bilioni 24. Bilioni 24 kila helikopta kwa kanda 7 ni Sh bilioni 168.

Kwa fedha hizi Sh bilioni 168, kila kanda itapata helikopta moja ya uokoaji. Fedha hizi za helikopta saba hazifikii hata nusu ya fedha za Dreamliner moja.

Huu ni mfano, tunaweza kufanya zaidi ya hapo au vinginevyo. Uwezo huu rais ameonyesha kuwa tunao.

Rwanda ni nchi ndogo, ila wana utaratibu wa kutumia helikopta hata katika ajali za barabarani ili kuokoa maisha. Tutafanya hivyo na sisi. Basi lililopata ajali Mikumi halitasubiri magari yanayopita ya IT kubeba majeruhi wawili wawili au mmoja mmoja kuwapeleka Iringa hospitalini. Helikopta ya kanda hiyo itafika haraka, itabeba watu haraka na kuwafikisha hospitalini kwa wakati. Tupate Tanzania ya aina hii.

Fanya utafiti, utaona kuwa watu wengi kwenye ajali za barabarani hutoka wakiwa wazima. Wengi hufia nje wakitumia muda mrefu kusubiri magari ya msaada au hufia njiani wakipelekwa mbali kupata matibabu. Tupate helikopta, tutaokoa maisha ya wengi.

Helikopta ndicho chombo pekee duniani cha haraka kufika katika ajali yoyote ile, iwe ya angani, nchi kavu ama majini. Ajali nyingi hata zile za majini vifo huwa vinaongezeka kwa sababu hatuna vyombo vya haraka kufika kwenye matukio.

MV Bukoba ilianza kuzama saa 12 alfajiri. Ili kuiandaa MV Victoria na MV Butiama zifike kwenye tukio kuokoa ilikuwa mpaka saa tano, saa sita mchana. Ni idadi ya watu wangapi walikufa katika muda huo wa katikati wakisubiri kuokolewa? Ni wengi.

MV Spice Islanders iliua watu wengi kwa sababu meli na boti za uokoaji zilipata ugumu kukaribia eneo la Nungwi kutokana na eneo hilo kuwa la dhoruba lisilo salama kwa vyombo vya majini. Kwa kurusha kamba na maboya helikopta za uokoaji zingenusuru maisha ya wengi.

Basi, salamu za mwaka mpya, na mwaka huu hii iwe ajenda, na Inshaallah tutafika.

By Jamhuri