Ofisi ya CAG sasa yasambaratishwa

 

*Naibu CAG aondolewa, Utouh atakiwa ajiandae kung’atuka

 

Hasira za watendaji kadhaa wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma na taasisi mbalimbali dhidi ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, zimeanza kuzaa matunda baada ya kuwapo mpango wa kuwang’oa viongozi wake wakuu.

Habari za uhakika zilizopatikana kutoka serikalini, zinasema wakati Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh (pichani), akitakiwa ajiandae kung’atuka, Naibu wake, Athanas Pius, ameshatupwa nje.

 

Pius, mmoja wa watu wanaotajwa kuwa wana-Mungu na waadilifu, ameshapewa barua ya kuondolewa katika cheo hicho, na ametakiwa aripoti Wizara ya Fedha ambako hajapangiwa kazi yoyote.


Ofisi ya CAG inatajwa kama moja ya sehemu ngumu sana za kufanya kazi. Taarifa za ofisi hiyo zimeleta mabadiliko makubwa tangu Rais Jakaya Kikwete aliporidhia taarifa ya CAG kuwekwa bungeni, kwa mujibu wa Katiba na wabunge kupata wasaa wa kuijadili.

 

Katika majadiliano hayo, mwaka jana mawaziri sita na naibu mawaziri wawili waling’olewa, kutokana na shinikizo la wabunge baada ya kuipitia na kuichambua vilivyo ripoti ya CAG.

 

Pamoja nao, watendaji kadhaa wakiwamo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango, Charles Ekelege, na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari, Ephraim Mgawe, waling’olewa kwenye nafasi zao.

 

“Ofisi ya CAG si ofisi ya marafiki, huwezi kufurahisha kila mtu, kila ripoti inapotoka ujue kwa CAG wanaibua maadui wapya,” amesema mmoja wa watoa habari ndani ya Wizara ya Fedha.

 

Dalili za kuanza kuikata makali ofisi ya CAG zimeshajionesha bungeni ambako kwenye ratiba ya Mkutano unaoendelea, tofauti na mikutano iliyopita, hakuna fursa iliyotolewa kwa wabunge kuijadili ripoti ya CAG aliyoiwasilisha bungeni wiki iliyopita.

 

Jambo hilo limepingwa vikali na wabunge wengi, wakisema kitendo hicho kinarudisha nyuma uwajibikaji serikalini na kulipoka Bunge haki yake ya kuishauri na kuisimamia Serikali.

 

Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), akizungumza katika mkutano wa CAG na waandishi wa habari, ametoa wito kwa wabunge wote – bila kujali tofauti ya itikadi zao – kushikamana kuhakikisha kuwa muda unatengwa kwa ajili ya kuijadili ripoti ya CAG. “Ikishindikana Bunge hili, iwe kwenye Bunge la Oktoba, tusiache utaratibu wa kuchangia ripoti ya CAG, uamuzi huu wa kuzuia mjadala ni wa kukurupuka. Serikali ndiyo mkaguliwa, sasa wanataka mkaguzi akienda kuwakagua wawe wamekaa kwa raha tu…bila wasiwasi.

 

Wanajipa (Serikali) sifa chafu ya kumdhibiti CAG. Hela za Serikali lazima zijulikane zinafanya nini. Ukichukua hela ya Serikali lazima ujibu,” amesema Cheyo. Mbunge wa Ludewa, Deo Filikujombe, akinukuu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , amesema kazi ya Bunge ni kuisimamia na kuishauri Serikali, lakini ilivyo sasa ni kwamba kuna njama za kuondoa “kusimamia” na kubaki na “kushauri” tu.


“Walianza kupunguza siku za kujadili ripoti ya CAG, sasa hakuna kujadili kabisa….Tunapoteza muda na fedha. Hakuna dhamira ya dhati ya Serikali kuwajibika. Mwenyekiti kupitisha sheria kwa kuhoji na kusema ‘nadhani’ waliosema ndiyo…, ‘nadhani’. Hapa Serikali lazima iwe na dhamira ya dhati. Kwa sasa dhamira ya dhati hakuna. Tumeng’olewa meno (wabunge hawana nguvu),” amesema Filikunjombe.


Mpango mwingine ambao Spika wa Anne Makinda ameufanya kwa kile kinachoonekana kuwa ni manufaa ya kuilinda Serikali, ni kufutwa kwa iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe. Kwa utaratibu wa kikanuni, Kamati hiyo na nyingine kadhaa zinaongozwa na wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.


Akizungumzia kuvunjwa kwa POAC, Utouh amemkosoa Spika Makinda, akisema kwa sasa Kamati hiyo inahitajika pengine kuliko wakati wowote ule. Amesema kazi za POAC kuunganishwa kwenye PAC kutaifanya Kamati hiyo mpya isiweze kabisa kutekeleza wajibu wake hata kwa kiwango cha nusu.

 

“Kuzifanya kazi hizo zote kunahitaji Mwenyezi Mungu ashuke mbinguni. Nayasema haya kwa nia njema kabisa kwamba kuna haja kubwa ya kurudisha Kamati hii (POAC) hata kama ni kwa jina lolote,” amesisitiza Utouh.

1297 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!