Kwa mara nyingine, Loliondo imetawala kwenye vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi. Sina desturi ya kuitetea Serikali, lakini hiyo haina maana kwamba inapoamua kufanya jambo la manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo, nishindwe kuitetea.

Mgogoro wa Loliondo hatuwezi kuujadili kwa jazba, na tena ufumbuzi wake hauwezi kuletwa na wanasiasa waoga kama kina Mwigulu Nchemba, wasioijua “siasa na biashara ya Loliondo”. Kabla ya mtu yeyote kuingia kwenye ushabiki, na kabla hajawa na upande anaotaka kuegemea kwenye mgogoro huu, anapaswa kujua siri iliyofichika hapa.


Ni kwa sababu hiyo, nimeamua, kwa makusudi kabisa, kurejea makala ya uchunguzi niliyoidnaika mwaka jana; pamoja na kuongeza mambo mengine machache yaliyojitokeza kwa wiki mbili sasa. Makala hiyo ya mwaka jana ilisema hivi:


Suala la mgogoro wa Loliondo limekuwa likitawala katika vyombo vya habari kwa miongo kadhaa sasa. Safari hii kuna kampeni inayoendeshwa kwenye mtandao kwa wiki kadhaa sasa. Chanzo cha mjadala huo ni kwamba Serikali ya Tanzania inataka kuwaondoa wafugaji wa Kimasai ndani ya Loliondo ili kupisha biashara ya uwindaji wa kitalii. Kampeni hiyo inaendeshwa na mtandao wa Avaaz.


Kinachopaswa kujadiliwa hapa ni uhalali wa hao wanaoendesha kampeni hiyo, kujua kama kweli wana jambo la msingi wanalolipigania, au kuna msukumo uliofichika nyumba ya mkakati huu. Ili kulifahamu vema suala hili, yampasa mtu kufikiria kwa makini, kupembua na hatimaye kufikia suluhisho.

Historia

Mgogoro huu upo ndani ya Wilaya ya Ngorongoro, ambayo ni moja kati ya wilaya tano zinazounda Mkoa wa Arusha. Kaskazini inapakana na Kenya , Mashariki kuna wilaya za Monduli na Longido, Kusini ipo wilaya ya Karatu na Magharibi inapakana na Mkoa wa Mara.  Wilaya imegawanywa katika maeneo matatu ya kiutawala; Kusini mwa Ngorongoro kuna Mamlaka ya Ngorongoro (Ngorongoro Conservation Area Authority) yenye matumizi mseto ya ardhi; Kaskazini kuna Loliondo inayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti; Tarafa ya Loliondo inajumuisha Pori Tengefu (Loliondo Game Controlled Area –LGCA). Eneo hili limetengwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori, wafugaji wa asili, kilimo na utalii wa kiikoloji.


LGCA ni eneo lenye vitega uchumi vingi. Baadhi ya vitega uchumi katika eneo hili ni:-

*Otterlo Business Corporation Ltd (OBC). Hawa wana leseni ya kuwawezesha kufanya shughuli za uwindaji wa kitalii katika LGCA kama zilivyo kampuni nyingine 60 katika maeneo mbalimbali nchini.

*And Beyond: Hawa wameweka kambi ya kudumu na kiwanja cha ndege. Shughuli zao zinaweza kuonakena katika tovuti yao ya www.kleinscamp.com

*Thomson Safaris: Hawa wanaendesha shughuli zao za utalii wa asili katika maeneo ya Sukenya, Soitsambu. www.thomsonsafaris.com

*Dorobo Tours and Safaris: Hawa wanaendesha utalii wa kiikolojia. [http://www.tanzanianorphans.org/dorobo.html] na [http://www.marilynmason.com/dorobo.html]

*Sokwe Asilia: Hawa wana kambi za kudumu na za muda. www.asiliaafrica.com/

*Nomad Safaris: Kampuni hii inamiliki kambi.

www.nomad-tanzania.com/

Haishangazi kuona kuwa hitimisho la yote haya ni mambo makuu matatu. Mosi, masilahi kutokana na utalii. Pili, vita ya kiuchumi, na tatu, huwezi kushindwa kubaini kuwa washindani wengi katika vita hii wanasukumwa na ukwasi uliopo Loliondo-wanalitaka eneo hilo.


Hoja hizi ndizo zinazosababisha uwepo wa nguvu za kisiasa zinazopenyezwa kupitia ushindani wa kibishara. Kila kundi linajitahidi kujiwekea mazingira ya kuhakikisha linafaidi mazao ya utalii katika Loliondo.


Utafiti unaonyesha kuwa Loliondo ni eneo pekee lenye vivutio vya aina ya kipekee katika mazingira ya asili ambavyo vinavutia watu wengi. Hali hiyo imewafanya washindani wengi, hasa wafanyabiashara watumie mbinu mbalimbali kuhakikisha wanafaidi rasilimali katika eneo hilo .


Wanaojiita waharakati, kwa kelele zao nyingi za kutunga, na kwa kujali masilahi yao , wameifanya Serikali ya Tanzania iingilie kati suala la Loliondo na kutoa matamko mbalimbali.


Hata hivyo, baada ya matamko hayo, NGOs na wadau wao wamejipanga kuendeleza mapambano. Kwa mfano, kabla ya msimamo wa Serikali hapakuwapo kundi lililojitambulisha kama (Avaaz) ambalo limeshiriki katika kuukuza mgogoro huu hata ukaweza kuvuma duniani. Kana kwamba jambo limefikia machweo, kundi hilo likajitokeza na kujitangaza kama la wanaharakati wa haki za binadamu. Vyovyote iwavyo, matamko yake yanaonyesha wito wake kwa Serikali ni kuhakikisha kuwa Ortello Business Corporation Ltd inanyang’anywa leseni.


Lakini jambo ambalo linazua maswali mengi ni kuhusu wawekezaji wengine walioko Loliondo. Kwanini hawahusishwi katika mpango wa kuondolewa au kwenye tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu? Hapa huhitaji maarifa zaidi kutambua kuwa mlengwa kwa mpango wote huu ni Ortello Business Corporation Ltd.

 

Kwanini wengine hawaguswi? Mbona hawapigiwi kelele licha ya ukweli kwamba hawana lolote la maana wanaloifanyia jamii ya wakazi wa Loliondo?  Ilitarajiwa kuwa kama suala ni la wafugaji ndani ya Loliondo, wawekezaji wengine nao wangesakamwa.

 

Thomson Safaris katika mradi wao wa Sukenya waliwazuia wafugaji kunywesha mifugo yao katika eneo la Mto Pololet wakati wa ukame mkali kweli kweli. Je, hiyo haikuwa uvunjaji wa haki za binadamu? Kwa kuwa Thomson si mlengwa kwenye mkakati wa kuondolewa Loliondo, hawaguswi.


Chukulia himaya za kampuni za Klein’s Camp, Dorobo Tours & Safaris je, ni rafiki wa wafugaji? Jibu ni hapana. Suala hapa si kampuni gani, bali kwanini mkakati huu umeelekezwa kwa kampuni moja pekee miongoni mwa kampuni nyingi zilizoko ndani ya eneo moja la Loliondo.


Wanaojiita watetezi wa haki za binadamu wana ajenda yao mahsusi. Miezi kadhaa iliyopita kulikuwa na kutoelewana kati ya wafugaji wa Kijiji cha Ololosokwan na kampuni ya Kleins camp; Thomson dhidi ya Sukenya. Iliripotiwa kuwa baadhi ya watu walipoteza maisha. NGONET, PINGOS Forum, Oxfam Ireland na wengine walilifikisha suala hili katika Universal Periodic Review of Human Right process (UPR-process). Mbona sasa hawasemi lolote? Kitu gani kimewazima?

Ushiriki wa mashirika ya kiraia

Ushiriki wa mashirika ya kiraia katika migogoro ya Loliondo si jambo jipya. Kinachoonekana kuwa kipya ni aina ya kampeni. Uongo ulioibuliwa safari hii ni kwamba Serikali inataka kuwaondoa wafugaji wa Kimasai ili kupisha uwindaji wa kitalii.

 

Kampuni inayotajwa kuwapo kwenye mpango wa kupewa eneo hilo ni Ortello Business Corporation Ltd. Uzushi huu umeibua taharuki kubwa. Hii ni kampeni yenye malengo nyuma yake. Hao wanaoendesha propaganda hizi hawazungumzi lolote la kuwahusu wawekezaji wengine walioko Loliondo.

 

Hii ni sababu tosha kwamba suala si la Wamasai wafugaji kuondolewa Loliondoa au kupokwa ardhi, bali ni Ortello Business Corporation Ltd ndiyo inayotakiwa iondoke. Kama sivyo, wawekezaji wengine waliopo eneo hilo , tena wasio na msaada wowote kwa jamii, nao wangehusishwa.


Pia ikumbukwe kuwa Oxfam ni shirika linaloongozwa na Wazungu. Ortello ni kampuni ya Waarabu. Wanaochochea vurugu hizi ni kampuni za Wazungu. Haihitaji akili kubwa kutambua kwamba hapa mwarabu anapigwa vita ili wazungu walitwae eneo hilo.


Kinachoenezwa kwamba ni mgogoro kati ya Otterlo Business Corporation Ltd na wafugaji katika LGCA si kinachochochea mgogoro kati ya pande hizo mbili. Inajulikana wazi kwamba Otterlo Business Corporation Ltd inachangia kwa kiwango kikubwa mno maendeleo na ustawi wa wafugaji katika eneo hilo , inasomesha watoto wengi hadi vyuo vikuu, inachangia maendeleo ya Wilaya ya Ngorongoro, sambamba na kuongeza pato la Taifa. Lakini mtu anaweza kujiuliza, inakuwaje kampuni inayoongoza kutoa huduma kama hizi, ionekane kuwa haina manufaa kwa Loliondo na Taifa kwa jumla?


NGOs zenye mlengo wa kibiashara zinashirikiana na Oxfam Ireland . Shirika hilo la misaada ndilo linalofadhili NGONET, Ujamaa Community Resource Trust (U-CRT) na PINGOS. Asasi hizi ndizo zinazosabambaza sumu ya chuki. Miezi kadhaa iliyopita walizusha uongo wa kwamba Serikali inataka kuwaondoa wafugaji Loliondo. Kinachopaswa kuhojiwa hapa ni kwamba iweje asasi hizi za kibiashara ziitumie Oxfam Ireland ambayo miaka kadhaa iliyopita imefunga miradi yake Loliondo?


Kuna ushahidi unaojitosheleza kuwa baadhi ya NGOs hizi zinazoendeleza chokochoko zinafadhiliwa moja kwa moja na Sokwe Asilia na Rubin Hurt Safaris; NGONET kupitia Tanzania Natural Resources Forum (TNRF); ilhali Dorobo Tours and Safaris inafadhili U-CRT na PWC. NGOs hizi zimekuwa zikijihusisha na masuala ya Loliondo kwa miongo kadhaa sasa.


Upo ushahidi usio na shaka kwamba karibu robo tatu ya madiwani wa Ngorongoro, ama ni waajiriwa kwenye NGOs hizo, au ni sehemu ya wamiliki wake. Hawa ndiyo wanaopambana kuhakikisha kuwa Ortello inaondolewa. Endapo ikiondolewa, ardhi yote ya vijiji itakuwa chini ya vijiji. Kwa sababu hiyo, madiwani kama mawakala wa wazungu, watashiriki kuanzisha WMA na kwa sababu hiyo watakuwa na biashara kubwa na nono zaidi.


Kadhalika, mtandao wa Avaaz ambao sasa umevalia njuga uongo huu, inataka kujionyesha kuwa imeguswa mno na suala la wafugaji katika Loliondo. Hata hivyo, hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa wamechukua hatua kama hizo kwa maeneo mengine nje ya Loliondo.

 

Je, hii ni kutaka kusema kwamba wafugaji katika maeneo mengine nchini Tanzania hawakabiliwi na changamoto zinazofanana na zile za Loliondo? Kwa hakika yapo maeneo mengine nchini, lakini Loliondo ndipo penye kile wanachokitaka, hasa kutokana na ukweli kwamba kunapatikana wanyamapori wa aina zote ambao ni kivutio kikuu cha kampuni za uwindaji wa kitalii.


NGOs zimekuwa zikienda nje zaidi ya kile ambacho zimekuwa zikijinasibu nacho, yaani kuwatetea wafugaji. Zimekuwa na masilahi na kampuni za utalii ambazo nimezitaja. Oxfam Ireland , PINGO’s Forum, U-CRT, NGONET na Pastoral Women Council (PWC) zimekuwa zikihaha kuwa na uhusiano wa karibu wa kibiashara na kampuni za kitalii na mashirika mengine ya kimataifa ndani na nje ya Tanzania .


Kinachonyamaziwa, na ambacho kwa muda mrefu hakijawekwa wazi ni kwamba NGOs hizi hazijihusishi moja kwa moja na kwa uwazi na masuala ya kibiashara, lakini nyuma yake ni za kibiashara zaidi.


Dorobo Tours and Safaris ndiyo wafadhili na waendesha mambo mengi ya U-CRT na PWC.

Kulithibitisha hilo ni kwamba ofisi za U-CRT na PWC zipo ndani ya ardhi inayomilikiwa na Dorobo Tours and Safari. Ushirikiano huu hauhitaji maono ya ziada kuweza kutambua kilichofichika. Unaweza kujiuliza, inawezekanaje kwa NGO inayojihusisha na ‘haki za matumizi ya maliasili’ iwe pamoja na kampuni ambayo kazi yake ni kusaka faida? Hapa ikumbukwe kuwa ni kampuni hizi hizi zinazojihusisha na biashara za utalii ambazo zinalalamikiwa kwamba zinapora rasilimali za nchi na kuiacha jamii husika ikiwa masikini.

 

Kadhalika, David Peterson ni mmoja wa wakurugenzi wa Dorobo Tours and Safaris na vile vile U-CRT. Kwa hali kama hii huhitaji kuhangaika kujua ni kwanini U-CRT na PWC wanajihusisha mno kwenye mgogoro wa Loliondo. Katika kuthibitisha haya, tovuti ya Dorobo Tours and Safaris imeweka bayana.

 

Waweza kujionea haya kupitia [http://www.tanzanianorphans.org/dorobo.html]

na [http://www.marilynmason.com/dorobo.html]

 

Kadhalika, Sokwe Asilia imekuwa na masilahi Loliondo, na kwa kuyalinda wamejipenyeza kwenye NGOs.  Wamefanya hivyo kupitia asasi ya “Honey Guide Foundation” ambayo inaifadhili TNRF. Muhimu hapa ni kwamba David Bell ni mmoja wa wajumbe mahiri kabisa wa Kamati ya Utendaji ya TNRF na pia ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa nyumba za wageni na kambi za Sokwe Asilia. Anapatikana zaidi katika kambi ya Suyan iliyo katika Kijiji cha Ololosokwan, Loliondo.


Katika “klabu” yao ya TNRF, Keith Roberts ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji, lakini pia ndiye anayeendesha Friedkin Conservation Fund ambayo inaendesha shughuli zake katika vitalu karibu 14 sehemu mbalimbali nchini Tanzania . Sasa wamekusudia kuongeza kitalu kingine cha 15 endapo watafanikiwa katika mgogoro huu wa Loliondo!


Ni wazi kwamba wafugaji katika maeneo mengine nchini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali. Wafugaji waliopo Kilosa, Bunda, Mvomero, Kilombero, Mbarali, Rufiji na sehemu mbalimbali za Tanzania wanahitaji kusaidiwa kuyakabili matatizo wanayopata. Lakini hawa wanaojiita wawekezaji, wakiwamo Oxfam kupitia NGOs mbalimbali wamejikita Loliondo pekee kana kwamba hakuna wafugaji sehemu nyingine za Tanzania.

 

Hapa ikumbukwe kuwa hata Jumuiya ya Ulaya (EU) ni miongoni mwa wachochezi wa mgogoro katika Loliondo. Hawa ndiyo wamekuwa wakijinasibu kwa kutaka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inadumu. Wameshiriki kupinga ujenzi wa barabara ya Mto wa Mbu-Musoma. Lengo lao ni kuilinda Serengeti. Na ni hawa hawa wanaojua kwamba bila kuilinda Loliondo, Serengeti haipo!

Uamuzi wa Waziri Kagasheki

Hivi karibuni Serikali ilifanya uamuzi wa kuliondoa eneo la Kilomita za mraba 2,500 kutoka Pori Tengefu la Loliondo na kuwapatia wananchi ili walimiliki kisheria na kuitumia ardhi hiyo kwa hiyari yao kwa ajili yakuwaletea maendeleo. Eneo lililobaki la kilomita za mraba 1,500 litaendelea kuwa Pori Tengefu na kumilikiwa na Wizara kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009.


Serikali imefanya hivyo kwa sababu kuu tatu: Ni sehemu ya mazalia ya wanyamapori; ni sehemu ya mapito ya wanyamapori; na ni vyanzo vya maji. Eneo hilo litaendelea kuwa chini ya Wizara, kwa kuwa linachangia kwa kiwango kikubwa kuimarisha mfumo-ekolojia wa Serengeti. Serikali imechukua uamuzi huo kwa kuelewa kwamba mazingira ya uhifadhi ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha mfumo-ekolojia na kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

 

Lakini baada ya uamuzi huo kumekuwapo maoni ya kupotosha kutoka kwa NGOs na mawakala wao kupotosha ukweli wa mambo. Wakati eneo la wananchi likiwa limeongezwa kwa uamuzi huu, wapotoshaji wanasema wananchi wamenyang’anywa eneo. Wanazua uongo huu wakitambua kuwa Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009, Sehemu ya16 Vifungu Na. 4, 5 na 6 vinampa nguvu Waziri mwenye dhamana uwezo wa kupitia upya mapori tengefu na kufanya marekebisho mbalimbali yenye lengo la kuleta manufaa kwa wananchi na kulinda uhifadhi.


Waziri alifanya uamuzi huo kwa kuzingatia taarifa mbalimbali za utafiti na uchunguzi ambazo ziliwahi kufanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori(TAWIRI). Pia alizingatia mapendekezo ya tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza mgogoro uliokuwapo.  Mojawapo ya tume hizo ni Tume ya Waziri Mkuu ya mwaka 2010 ambayo ilijumuisha wajumbe kutoka wizara kenda, Mkoa wa Arusha na Wilaya yaNgorongoro. Vilevile, kwa muda mrefu viongozi wa Wizara wamekuwa wakikutana na wananchi na viongozi wa Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro kuzungumzia suala la Loliondo. Sasa ukigeugeu huu unasababishwa na nini?

Hitimisho

Kwa maelezo haya ya awali, lakini yanayojitosheleza, Watanzania na walimwengu hawapaswi kufundishwa tena kutambua nani wapo nyuma ya mchezo huu mchafu wa Loliondo.


Kinachopaswa kujulikana sasa, na ambacho tunapaswa kwenda mbali zaidi, ni kujua ni nani hasa huyo mkubwa aliye nyuma ya “sinema” hii yote. Bila kukwepesha maneno, ni wazi kuwa Oxfam na kampuni za kigeni kupitia NGOs ndiyo wapo nyuma ya mchezo huu mbaya.  Hawa ndiyo wafadhili wakuu wa vikundi hivi.

 

Wametafuta uongo wa kila aina kuhalalisha vurugu na migogoro isiyokoma katika Loliondo. Huu ni upuuzi unaopaswa kudhibitiwa ili Loliondo na Tanzania iendelee kuwa ya amani. Lakini lililo muhimu ni kwamba hakuna Serikali yoyote duniani ambayo inaongozwa na NGOs.


Uamuzi wa Serikali kwa Loliondo, hauna manufaa kwa Loliondo na Tanzania pekee, bali kwa ulimwengu mzima wa uhifadhi.


Urithi wa wanyamapori unastahili kulindwa kwa busara zote. Wananchi wa Loliondo wana haki ya kuishi Loliondo na kuendesha shughuli zao. Lakini haki hiyo haimaanishi kuwa wana haki ya kuzuia uhifadhi wa vyanzo vya maji, mapitio na mazalio ya wanyamapori. Bila kuwa na Loliondo kama “buffer zone”, Serengeti haipo.


Mambo muhimu yanayohusu uhai wa Taifa kwa faida za sasa na kwa vizazi vijavyo, hayapaswi kuonewa aibu au kuogopa kuyasema wazi wazi.

Please follow and like us:
Pin Share