BABA GASTON Mtunzi wa ‘Kakolele’, wimbo usiochuja

TABORA

Na Moshy Kiyungi

Msimu wa sherehe za mwisho wa mwaka 2021 unamalizika na kama ilivyo kwa miaka mingine, zipo nyimbo kadhaa ambazo husikika zaidi nyakati hizi pekee.

Mmoja miongoni mwa nyimbo hizo ni ‘Kakolele’, maarufu kama ‘Viva Krismasi’.

Wimbo huu ulitungwa miaka ya 1970 na mwanamuziki mkongwe, Ilunga Omer ‘Baba Gaston Ilunga wa Ilunga’, aliyekuwa kiongozi wa Bendi ya Orchestra Baba Nationale.

Kwa miaka mingi wimbo huu umekuwa ukipigwa na kusikika kwenye vituo vingi vya redio kila Desemba, kuashiria kuwadia kwa moja ya sikukuu kubwa duniani, Krismasi. 

Hata kama lugha iliyotumika kwenye wimbo huo haieleweki kwa wengi, lakini bado umeendelea na utaendelea kukubalika kwa watumiaji wa Kiswahili, hasa kutokana na maneno; ‘Yesu! Yesu anakuya!’ yaliyomo ndani ya muziki wenyewe.

Wimbo huu ni miongoni mwa zile chache zinazoaminika kuwa ni ngumu kuigwa, wataalamu wa muziki wakiamini kwamba ni kutokana na ufundi mkubwa uliotumika katika kuupangilia na umahiri wa hali ya juu katika uimbaji wake.

Wimbo huu uliimbwa na muimbaji mahiri, Kasongo wa Kanema, ambaye kwa mapenzi ya Mungu, alifariki dunia Aprili 15, 2020 huko Lang’ata, jijini Nairobi, Kenya, akiwa na umri wa miaka 73.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba mtunzi mwenyewe, Baba Gaston Ilunga wa Ilunga, alizaliwa Julai 5, 1936 katika mji wa Likasi, jirani na Lubumbashi, Jimbo la Shaba, kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), na  kupewa jina la Ilunga Omer.

Mkongwe huyo alikuwa mwanamuziki wa kwanza kutoka DRC kufanya makazi Afrika Mashariki, akianzia Tanzania miaka ya mwanzoni ya mwaka 1970 wakati taifa hilo likitawaliwa na Rais Joseph Mobutu.

Ni wakati Mobutu alipowataka raia wote wa Zaire (wakati huo, sasa DRC) kuacha mara moja kutumia majina ya kigeni na badala yake watumie ya Kiafrika, ndipo Ilunga Omer akabadili jina na kuitwa ‘Ilunga Chenji Kamanda wa Kamanda’.

Kama kiongozi, Mobutu naye akaonyesha njia na kuachana na jina lake la ubatizo la ‘Joseph’ na kuitwa Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu Wa Zabanga.

Kipaji cha muziki cha Baba Gaston kilianza kuonekana baada ya kufundishwa kucheza piano na raia wa Ugiriki, Leonides Rapitis. 

Wakati bado akiwa mwanafunzi wa muziki, gwiji huyo akaibuka na wimbo ‘Barua kwa mpenzi Gaston’.

Akiwa na umri wa miaka 20 tu huko Lubumbashi, akaunda bendi na kuiita Orchestra Baba Nationale ambayo mara moja ikawa maarufu ndani na nje ya Afrika; ikifanya ziara kadhaa Zambia, Zimbabwe na Ulaya kabla ya kuhamia Tanzania na baadaye kuweka makazi ya kudumu Kenya.

Akizungumzia ‘safari ya muziki’ na umaarufu wake, mtunzi na mwimbaji wa Orchestra Baba Nationale, Kabila Kabanze ‘Evany’, anasema walisafiri kutoka Lubumbashi  kwenda Kinshasa kwa ajili ya kurekodi.

“Ilikuwa ni mwaka 1971. Kutokana na ubovu wa barabara tulilazimika kupita njia ya Kisangani hadi Kalemie mpakani mwa Tanzania. Sasa badala ya kwenda Kinshasa, tukaamua kuingia Afrika ya Mashariki.

“Mara tukajikuta tupo Dar es Salaam ambapo tukaweka makazi na kuanza kupiga muziki katika kumbi mbalimbali kwa miaka minne mfululizo,” anasema Kabila Kabanze.

Miaka hiyo Tanzania kulikuwa na studio moja tu ya kurekodi muziki, ikimilikiwa na Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na kutokana na wingi wa makundi ya muziki, kulikuwa na foleni kubwa kusubiri nafasi ya kurekodi.

Ni sababu hiyo ndiyo ikawafanya Orchestra Baba Nationale kusafiri hadi Nairobi na kuweka makazi.

“Huko tukakuta ushindani mkubwa! Kulikuwa na bendi nyingi zikiwamo Les Wanyika, Virunga, Super Mazembe na Shika Shika,” anasema.

Mwaka 1975 Baba Gaston akafikiria kuondoka Nairobi baada ya kubaini kuwa bendi yao haikuwa na wapenzi wengi.

Hata kabla ya kufikia uamuzi, Julai 1976, kukatokea kutoelewana kati ya wanamuziki na uongozi, kitu kilichosababisha kusambaratika kwa bendi.

Wanamuziki walioodoka kundini ni Bwami Walumona, Kasongo Wakanema, Kabila Kabanze, Kalenga Nzaazi Vivi, Lutulu Kaniki Macky na Twikale wa Twikale.

Hawa wakaunda bendi mpya na kuipa jina la Orchestra Les Mangelepa inayokumbukwa kwa vibao kadhaa maarufu kikiwamo ‘Embakasi’.

Mwaka mmoja baadaye zikaja taarifa kwamba Baba Gaston Ilunga Chenji Kamanda wa Kamanda amefariki dunia jijini Arusha.

Mwamba huyo aliacha mke na watoto saba na ataendelea kukumbukwa daima pamwe na wimbo wake wa ‘Kakolele Viva Krismasi’ ambao unaendelea kutamba kila nyakati za sikukuu za mwisho wa mwaka.

Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi. Amina.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa namba: 0713331200, 0767331200, 0784331200 na 0736331200.