Hali ya misitu baada ya miaka 60 ya Uhuru

Na Dk. Felician Kilahama

Awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na amani hadi kushuhudia taifa letu linaadhimisha miaka 60 tangu ‘Tanganyika’ ilipopata uhuru Desemba 9, 1961. 

Kadhalika, ifikapo Aprili 26, 2022 tutafikisha miaka 58 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aprili 26, 1964 ni siku ambayo Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia. 

Hiki ni kipindi kirefu, hivyo mengi yametokea ikiwamo changamoto za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kimazingira. Misitu ni moja ya sekta ambazo zimekumbwa na misukosuko mingi tangu tupate uhuru. 

Wakati tumepata uhuru kutoka kwa Waingereza walioitawala Tanganyika baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia; maeneo mengi nchini yalikuwa yamefunikwa na misitu na uoto mwingine wa asili; mfano, mimea na nyasi aina mbalimbali. 

Hivyo nchi ilikuwa kijani na hapakuwepo na changamoto ya kupata maji huku mvua zikinyesha kwa wakati na za kutosha ukilinganisha na hali ilivyo sasa. 

Tasnia ya misitu imegawanyika katika sehemu kuu mbili; misitu ya asili na ya kupanda (mashamba ya miti). 

Makala hii imejikita zaidi katika misitu ya asili na hatima yake kwa masilahi yetu na taifa kwa kuzingatia miaka 60 tangu tupate uhuru.

Tulipopata uhuru mwishoni mwa mwaka 1961, hapakuwepo takwimu zilizoonyesha misitu ilikuwa imefunika eneo kiasi gani. 

Baada ya uhuru jitihada zilifanyika kwa kupima na kutathmini eneo la misitu. Hatua hiyo iliwezesha kujulikana kuwa eneo la hekta milioni 33.5 (sawa na asilimia 36) ya eneo lote la Tanganyika (Tanzania Bara) limefunikwa na misitu. 

Kadhalika, wakati wa ukoloni misitu ilisimamiwa kwa kuzingatia Sera ya Misitu ya mwaka 1953 na Sheria ya Misitu (Forest Ordinance) ya mwaka 1955 na Kanuni zake. Kwa kutumia vyombo hiyo, Wakoloni, katika miaka ya 1950, walitangaza na kuanzisha misitu mingi iliyohifadhiwa kisheria (Forest Reserves).  

Mathalani, misitu ya Hifadhi ya Pugu na Kazimzumbwi wilayani Kisarawe, Pwani, karibu na Dar es Salaam. 

Vilevile, wakoloni walikuwa wakishirikiana na utawala wa kijadi (machifu/watemi), na kwa kuwa wataalaamu wa misitu walikuwa wachache sana, hivyo walitegemea sana kupitia watawala wa kijadi wasimamia misitu katika maeneo yao na matumizi yake kudhibitiwa ipasavyo.

Idara ya Misitu iliendelea kusimamiwa na wataalamu wa kikoloni. Hata hivyo, mwaka 1963 serikali ilimteua mtaalamu wa kwanza Mtanzania kuwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa Misitu. 

Baada ya uteuzi huo, juhudi ziliendelea kuimarisha usimamizi wa misitu ya asili. Mathalani, kuimarisha mipaka kwa misitu iliyohifadhiwa lakini pia kuongeza mingine kwa kuitangaza kuhifadhiwa kisheria. 

Kati ya mwaka 1961 na 1998 (ikiwa ni zaidi ya miongo mitatu tangu uhuru) tuliendelea kutumia Sera na Sheria za ukoloni. 

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa wakati tunapata uhuru eneo la misitu hekta milioni 16.7 lilikuwa chini ya usimamizi wa kisheria lakini baada ya uhuru ziliongezeka hekta 12,000 na kufikisha hekta milioni 16.712  (karibu asilimia 50 ya eneo lote la misitu) ikisimamiwa kisheria. 

Kadhalika, serikali iliendelea kuisimamia misitu katika maeneo matajiwazi (public land) ikiwa ni pamoja na kutoa leseni kukusanya mapato. Baadaye kukawapo na kada ya walinzi misitu hasa katika maeneo yaliyohifadhiwa kuhakikisha hayaharibiwi kwa kukata miti au kufyekwa hovyo kwa shughuli za makazi, kilimo na ufugaji.

 Pamoja na kuwapo juhudi za kuisimamia misitu, shughuli za binadamu ziliendelea kuongezeka. Tulipopata uhuru (1961) kulikuwa na Watanzania karibu milioni 10. Kadiri miaka ilivyosonga mbele idadi ya watu na mifugo iliongezeka ikiambatana na ongezeko la matumizi ya ardhi na rasilimali misitu. 

Miaka ya 1970 baadhi ya maeneo yalionekana kuathirika kutokana na matumizi yasiyo endelevu. Mfano, katika sehemu za Kondoa, makorongo makubwa kutokana na mmomonyoko wa ardhi yakawepo. 

Kwa hali hiyo tulilazimika kuanzisha mradi wa kuhifadhi ardhi katika maeneo hayo na sehemu nyinginezo mkoani Dodoma kupitia Hifadhi Ardhi Dodoma (HADO). 

Kufikia miaka ya 1980 sehemu za Kanda ya Ziwa hususan mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Mara misitu ilitoweka kwa kasi kubwa kutokana na kilimo cha pamba na makazi. 

Vilevile, kufyeka misitu kwa lengo la kufukuza mbung’o kuzuia ugonjwa kwa mifugo. Hali hiyo iliathiri sana ustawi kwa misitu na uoto wa asili. 

Matokeo yakawa ni uharibifu mkubwa wa ardhi na kusababisha maeneo ya Mkoa wa Shinyanga kugeuka jangwa. Mwaka 1984 kulifanyika mkutano na kuhudhuriwa na viongozi wa kitaifa chini ya uenyekiti wa Mwalimu Julius Nyerere. 

Mkutano huo ukaazimia kuanzishwa mradi: Hifadhi Ardhi Shinyanga (HASHI) kwa lengo la kuongoa ardhi na kudhibiti matumizi yasiyo endelevu. 

Pamoja na juhudi hizo, katika miaka ya 1970 Idara ya Misitu ilianzisha upandaji miti na kuwaelimisha wananchi ili waweze kupanda miti katika vijiji wanakoishi. 

Mwaka 1998 tulipobadilisha Sera ya Misitu ya kikoloni; utunzaji misitu na upandanji miti vikapewa msukumo zaidi na kuvifanya vijiji viwe vitovu vya kuhifadhi misitu ya asili kupitia mkakati wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu. 

Hata hivyo ongezeko la watu na kufutwa kada ya walinzi misitu kulisababisha usimamizi wa misitu kudorora. Vilevile serikali ilifuta utawala wa kijadi ambao, kwa namna moja au nyingine ulisaidia kulinda misitu isitumike hovyo. 

Hatua hizo zilisababisha misitu ionekane ni rasilimali isiyokuwa na mwenyewe kutokana na usimamizi kuwa duni. Hali hiyo ilifanya matumizi ya bidhaa za misitu na makazi pamoja na kilimo cha kuhamahama kuongezeka sana. 

Mathalani, matumizi ya kuni/mkaa kuwa zaidi ya asilimia 90 ya matumizi yote ya nishati nchini. Kadhalika kasi ya uvunaji miti ikawa kubwa na kusababisha misitu ya asili kuendelea kutoweka kwa kasi kubwa kila mwaka. 

Katika misitu ya asili hata baada ya kuanzisha Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) mwaka 2010; kasi ya kupoteza misitu ya asili imeendelea. Hii inatokana na ukweli kwamba Idara pamoja na Wakala kutokuwa na uwezo wa kutosha kutimiza wajibu wake.  

Kwa hali hiyo misitu ya asili ikawa ‘shamba la bibi’ kwa kukosa ulinzi, hivyo watu kufanya wanavyotaka. Mwaka 2015, takwimu zilionyesha kuwa kutokana na misitu ya asili kutosimamiwa vizuri; hekta 372,000 hutoweka kila mwaka.  

Vilevile, Kituo cha kufuatilia masuala ya gesiukaa (CO2) kilichopo SUA, Morogoro, mwaka 2017 kilionyesha kasi ya kutoweka misitu kuwa ni hekta 469,420. Isitoshe, kasi ya kuharibika ikaongezeka katika mikoa ya magharibi mwa Tanzania. 

Ukiunganisha ukataji miti kiholela, kilimo cha kuhamahama na uchomaji moto; athari zake kimazingira ni kufanya maisha kuwa magumu zaidi. 

Misitu ni muhimu kuhifadhi mazingira na kuwezesha wananchi kuishi maisha yanayostahili; lakini katika miaka 60 ya uhuru misitu ya asili imeathirika sana. 

Makala zinazofuata zitafafanua zaidi kuhusu uharibifu wa misitu na athari zake kwa mazingira na maisha yetu: kwa kutathmini tumekosea wapi na tufanye nini kwa faida yetu wote.

Mwandishi wa makala hii ni Mkurugenzi (mstaafu) wa Misitu na Nyuki. Anapatikana kwa simu namba …