DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu 

Sikupata bahati ya kuiona mechi nzima ya ‘Mnyama’ akiwa ugenini dhidi ya Kinondoni Municipal Council kwa kifupi KMC, iliyopigwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora. 

Hii ni kwa kuwa nilikuwa na majukumu mengine kadhaa ya kikazi na kifamilia, hivyo nikaishia kuona baadhi ya matukio kwenye vipande vya mechi ile.

Vilikuwa ni vipande vingi tu kwa kuwa mchezo wenyewe ulijaa matukio mengi ya kusisimua. Lakini kwa mtazamo wangu, mimi binafsi nimevutiwa na matukio matatu ndani ya mchezo wenyewe. 

Tukio la kwanza lililonivutia ni la bao la mkwaju mkali uliopigwa na Kibu Dennis.

Tukio la pili ni la askari kumpiga mtama shabiki wa Simba aliyekuwa amewafuata wachezaji wa Simba kushangilia nao bao. Na tukio la tatu ni la Pascal Wawa na Kocha wake Pablo Martin. 

Hebu tuanze kuyatazama matukio haya na kufafanua mawili – matatu yanayoyahusu. 

Tuanze na tukio la kwanza ambalo ni bao la Kibu. Kwa hakika bao hili lilipaswa kuendelea kwenye mijadala yetu mpaka mwisho wa mwaka huu, lakini kinachouma ni kwamba matukio mengine mawili yaliyotokea; askari kumpiga mtama shabiki wa soka na tukio la Wawa; yamefunika simulizi za bao lile la Kibu. 

Hakuna shabiki wala mchambuzi wa soka anayetaka kulijadili lile bao, kila mmoja anahoji kwa nini Wawa kasukumwa vile na Pablo?

Wengine wanajiuliza ni kwa nini askari karusha mtama wa aina ile kwa shabiki? Watu wamejibana kwenye kona za sehemu hizi mbili. Hawana muda na bao murua la Kibu.

Tuje tukio la pili. Jamani, askari wanaopewa majukumu viwanjani mna la kujifunza mnapokutana na mashabiki ‘wakorofi’ kama yule wa Tabora. 

Muwe mnajiuliza, kwanza hivi ni shabiki gani atatamani na kuvutika kwenda uwanjani iwapo ataiona video ile mbele ya mboni zake za macho? 

Ni wazi na inaeleweka kabisa kuwa shabiki yule hakufanya jambo jema kuuruka uzio unaowatenga mashabiki na wachezaji, kisha kuwafuata wachezaji wa Simba. Kitendo hiki hakikubaliki lakini pia hii haimhalalishii shabiki huyo kukutana na aina ya adhabu aliyokutana nayo siku ile.

Sisi wafuatiliaji wa soka kila siku huwa tunahoji kwa nini mashabiki hawaji kwa wingi viwanjani? Nadhani sasa tunaweza kusema tumepata sehemu ya majibu ya maswali yetu. Viwanjani kwetu hapa Tanzania si sehemu salama. Ukijichanganya unaweza kuaibika na hata kupata madhara ya kudumu. 

Ukiingia kwenye 18 za askari wa Tanzania kwa hakika utashika adabu. Hii ni tofauti kabisa na tunachokishuhudia Ulaya.

Kulikuwa na ulazima gani kwa yule shabiki kupigwa vile wakati angeweza kuondolewa bila kupigwa hata kofi moja? Au askari yule alikuwa na hasira! Kwa nini?

Ni lazima kuwepo au kujengwe urafiki kati ya askari wanaolinda usalama viwanjani na mashabiki wa aina ile na wengine wengi.

Nchi nyingine si kama hakuna mashabiki wanaoruka uzio na kuingia uwanjani, wapo. Tena hata kwenye Kombe la Dunia tumewaona. Lakini mashabiki wa wenzetu hutolewa kwa ustaarabu kabisa, tena wanasindikizwa hadi sehemu salama.

Muda mwingine mashabiki wenzake jukwaani humshangilia mwenzao. Ni vionjo tu hivi vya viwanjani. 

Tukio la tatu ni la Wawa. Kuna mambo mawili ndani ya tukio lile; mosi, hakuna maelewano katika benchi la Simba. Pili, siku za Wawa zinahesabika Msimbazi.

Nani alitaka Wawa aingie? Kocha Mkuu Pablo? Au wasaidizi wake Seleman Matola na Thierry Hitimana? Kuna kitu hakiko sawa katika benchi la Simba. Hiki ni kidonge cha uchungu kinachopaswa kumezwa na mabosi wa Simba. 

Sijui itakavyokuwa, lakini chini ya Pablo, Wawa hana maisha. Tulichokiona pale ni mwisho wa maisha yake. Inahitajika miujiza kuendelea kumuona Wawa akiwa Msimbazi huku Pablo akiwa kocha mkuu. 

By Jamhuri