Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Aprili 23, 2026 nchi yetu imepokea taarifa za kusitikisha mno kupitia ripoti iliyowasilishwa na Jaji Mkuu (mstaafu), Mohamed Chande Othman ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025. Nilikuwapo Ikulu. Viongozi wote wakuu wa taifa hili walikuwapo.
Alikuwapo Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk. Emmanuel Nchimbi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, Jaji Mkuu, Spika wa Bunge, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa vyama, mawaziri, wakuu wa mikoa, makatibu wakuu na baadhi ya wakuu wa wilaya.
Sitanii, kwa kazi yangu hii ya uandishi imeniwezesha kushiriki vikao vingi vya kitaifa. Nilikuwapo Ikulu kama nilivyosema. Kilikuwa kikao cha huzini. Kwa mara ya kwanza Tanzania vimetokea vifo 518, vifo vinavyohusiana na masuala ya kisiasa. Ukumbi ulikuwa kimya. Jaji Chande wakati anawasilisha ripoti, utadhani alikuwa anapita katikati ya msitu usio na ndege wala ndezi. Kila mtu alikuwa kimya kwa masikitiko.
Ndiyo, zimepotea mali zenye thamani ya Sh bilioni 125, lakini mali hizi haziwezi kulingana na maisha ya Watanania 518 waliopotea. Januari 26 na 27, mwaka 2001 kulitokea vurugu za kisiasa Zanzibar. Takwimu zinatofautiana, lakini zilizopo ni kuwa walikufa watu 21 hadi 46 huko Pemba. Taarifa nyingine zinasema walikufa watu 60, nyingine zinasema walikufa watu 89.
Ikumbukwe mimi ndiye niliandika habari yenye kichwa cha habari kilichosema: “CUF watoa siku 90.” Habari hii nilimhoji aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Wilfred Lwakatare, baada ya uchaguzi wa mwaka 2000, ambaye aliniambia nami nikaiandika kwenye Gazeti la Mwananchi, kuwa baada ya siku 90 wangefanya maandamano makubwa hadi uchaguzi wa Zanzibar urudiwe.
Sitanii, baada ya kuandika habari hiyo, CUF waliendelea na kaulimbiu yao ya “Ngangari”. Aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi wakati huo, Omari Mahita, aliitisha mkutano na waandishi wa habari akasema: “Kama CUF ni ngangari, polisi ni ngunguri.” Hii ilikuwa ni mnyambulisho wa maneno kwa kuanza na …nga, nge, ngi, ngo na ngu… hivyo akimaanisha kuwa polisi walikuwa zaidi ya CUF.

CCM kwa upande wao walianzisha kaulimbiu ya “Nginjanginja.” Kilichofuata baada ya habari hiyo, tulianza kuhesabu siku na kila upande kama waandishi tulitafuta wanasemaje. Kadiri siku zilivyozidi kushuka, joto lilizidi kupanda. Zilipobaki siku 20, niliona kabisa kuna shida. Niliandika makala kuwaomba polisi na vyama vya siasa wazungumze, kwani mwisho usingekuwa mzuri. Meli iliishang’oa nanga, sijui hata kama makala hiyo waliisoma.
Kilichofuata baada ya hapo ni historia. Tukashuhudia Tanzania kwa mara ya kwanza inazalisha wakimbizi kwenda Shimoni, Mombasa, Kenya. Tukashuhudia vifo vya Watanzania wenzetu kwa idadi niliyoitaja hapo juu. Idadi hii haikuwa hata robo ya vifo vilivyotokea Oktoba 29, 2025. Haraka haraka, Machi 17, 2001 vyama viwili – CCM na CUF katika kushusha joto la kisiasa viliingia mwafaka wa awali kwa kusainishana makubaliano ya kusitisha uhasama.
Makatibu wakuu wawili wa vyama hivi, Philip Japhet Mangula, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), waliingia kwenye majadiliano ya kina jinsi ya kuiondoa Zanzibar katika kadhia hii. Waliendelea na mazungumzo hadi Oktoba 10, 2001 wakati pande hizi mbili ziliposaini mwafaka wa kisiasa wa kumaliza uhasama na kuleta utangamano wa kisiasa.
Makatibu wakuu hawa walikuwa na wasaidizi kila upande. CCM wasaidizi katika majadiliano haya walikuwa ni Kingunge Ngombale-Mwiru, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu – CCM na Mohamed Aboud Mohamed, ambaye naye alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa – CCM. Ni ujumbe mzito sana huu. Hawakuwa watu wepesi.
Kwa upande wao CUF walikuwa na wasaidizi Ali Haji Pandu, aliyekuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi – CUF na Hamad Rashid Mohamed, ambaye naye alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi – CUF. Oktoba 10, 2001 hawa waliongoza pande zao kutia saini mwafaka wa kisiasa, huku wakishuhudiwa na viongozi wakuu ambao nao walitia Saini mwafaka huo pale Zanzibar. Sikusimuliwa, nilishuhudia.
Rais (wakati huo), Benjamin William Mkapa, akiwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (wakati huo), Amani Abeid Karume na Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa Chama Cha Wananchi (CUF).
Prof. Lipumba alisema: “Tusameheane, ila tusiyasahau.” Hii ilikuwa sentensi nzito na inayoishi hadi leo. Mambo yaliendelea kutibuka katika uchaguzi wa mwaka 2005 huko Zanzibar, lakini Rais Karume na Maalim Seif, walikutana wakazungumza, ikazaa mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar, ambayo imezaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Sitanii, nafikiri msomaji unajiuliza kwa nini nirudie historia ya mgogoro wa Zanzibar, wakati ripoti ya Jaji Chande ilihusu matukio ya vurugu wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025? Na kwamba mbona Zanzibar hakukuwapo vurugu, Watanganyika wengi walikimbilia Zanzibar kujiokoa kinyume cha ilivyozoeleka wakati wa uchaguzi?
Ilikuwa ninajenga hoja. Yaliyowafikisha Wazanzibari hapo hayana tofauti sana na yaliyochukua roho za Watanzania wenzetu 518 na kujeruhi wengine zaidi ya 2,000. Naomba niazime neno kwa neno kutoka kwenye nyaraka ya mwafaka wa CCM na CUF, Zanzibar wa Oktoba 10, 2001 juu ya mambo au madai waliyokuwa wanapambana yarekeshwe kama ifuatavyo:-
a) Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufanyiwa marekebisho ili kuifanya iwe Tume Huru na ya haki kufuatana na mfumo unaokubalika katika nchi za Jumuiya ya Madola. b) Kuanzishwa kwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. c) Kufanyiwa mapitio Katiba ya Zanzibar na Sheria za Uchaguzi ili ziafikiane na matakwa ya demokrasia ya vyama vingi.
d) Vyombo vya Habari vya Serikali kurekebishwa ili viepukane na upendeleo katika kutangaza shughuli za vyama vya siasa. e) Kuhakikisha kuwepo kwa uhuru wa vyama vya siasa kuendesha shughuli zake bila bughudha au vitisho. f) Mahakama za Zanzibar kufanyiwa marekebisho ili kukuza uhuru wake, utaalamu na heshima yake mbele ya jamii.
g) Viongozi wa zamani wa kisiasa katika serikali kupata heshima na haki sawa baada ya kustaafu. h) Vyama vya siasa kuheshimu Katiba na Sheria za nchi na kuepuka kutumia lugha zinazochochea chuki baina ya vyama vya siasa, ukabila, uhasama na kutovumiliana…

VYOMBO VYA DOLA KATIKA UCHAGUZI – 7. Kwa lengo la kuhakikisha kwamba vyombo vya dola
vinatekeleza majukumu yake kwa utaalamu na kwa kuongozwa na maadili ya kazi katika mfumo wa vyama vingi vya siasa ambapo vyama vyote vina haki ya kutendewa sawa, CCM na CUF vimekubaliana kupendekeza Serikali zihakikishe hatua zifuatazo zinachukuliwa:
a) Askari wapatiwe mafunzo mapya (retraining) yatakayozingatia wajibu wao katika mfumo wa siasa wa vyama vingi. b) Vyombo vya dola visiwe vinajihusisha kabisa na ushabiki wa siasa za vyama (non-partisan). c) Sheria na kanuni zinazotawala utendaji wa askari zifuatwe kikamilifu na kwamba wote wanaozikiuka wachukuliwe hatua stahiki bila kulindwa.
d) Sheria na kanuni za uajiri ziangaliwe upya ili kuhakikisha hakuna upendeleo wa kisiasa au wa aina yoyote. Kadhalika, watu ambao hawajaainishwa katika sheria na kanuni za uajiri wa askari, kwa mfano Masheha, wasishirikishwe. Mwisho wa kunukuu.
Tume ya Jaji Chande ukiisikiliza, matitizo ya msingi ni haya haya iliyoyabaini. Uchaguzi kutakiwa kuwa huru na wa haki, Katiba Mpya, kurekebisha mifumo ya sheria, ajira kwa vijana, kuwasikiliza vijana, watu hawataki kutekwa, kesi za kisiasa zifutwe na mengine kama hayo. Kumbe kikombe hiki tulikwisha kinywea. Ilitupasa na inatupasa kuwa makini.
Sitanii, kama vurugu za kisiasa ziliua watu 46 mwaka 2001, miaka 25 hivi baadaye mwaka 2025 zikaua watu 518, na hapo tunaambiwa kuna ndugu 39 wanaoendelea kuwatafuta ndugu zao. Naamini hata kama hatujui kusoma, picha tunaiona. Mwafaka wa Zanzibar kati ya mambo ulioingiza Zinzibar ni viongozi wote wa kisiasa (chama tawala na upinzani) kuacha kutumia lugha za kejeli, uchochezi na kuhamasisha vurugu. Zanzibar wamefanikiwa katika hili, nawapongeza.
Hapa kwetu tunazo kesi zinazotajwa kuwa ni za kisiasa. Tunao viongozi wanaotumia lugha kali na za kejeli kutoka pande zote mbili. Naamini busara ya Oktoba 10, mwaka 2001 ya kuhakikisha pande mbili zinamaliza uhasama, bado ina thamani hadi leo. Njia waliyoipitia Zanzibar, majirani zetu Kenya, Zambia, Malawi na DRC, tayari tumeikanyaga. Siamini kama kuna Mtanzania anayetamani kuona vurugu zinaendelea na yakatokea mauaji mengine ya Watanzania wenzetu. Watu 518 si mchezo.
Sitanii, nimemsikia Rais Samia. Nimesikia alivyosikia sauti za watu wanoasema “Tunamtaka Samia wetu na si huyu.” Amesema yeye ni Samia yule yule wa 4R. Hajabadilika. Amesema si muda mrefu ataunda Tume ya Maridhiano. Tume hii naiona kuwa ndiyo mzizi wa ufufuko wa Tanzania. Tume hii itakuwa na mamlaka ya kumshirikisha kila mtu. Iwe mtu yuko nyumbani, gerezani, kwenye siasa, nje ya siasa au hospitalini, itamshirikisha. Hiyo Tume ya Uchunguzi wa Jinai, acha nayo ifanye kazi tujue nani alishiriki uhalifu.
Tume ya Maridhiano itatoa nafasi ya watu kusema ukweli. Naamini ukweli utasemwa si kwa nia ya kufukua makaburi, bali kuponya vidonda. Ni katika msitari wa kupatana ndipo tunaweza kuandika hata hiyo Katiba Mpya ikawa na maana. Kama bado tuna lugha gongana, akina John Heche wakiamini bado anapaswa kuja Mzungu kutusuluhisha, huku Mzee Stephen Wassira akiamini Heche hata kama “mama yake mzazi (Heche) angekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi asingemwamini,” hatutafika.
Zanzibar waliambiana ukweli wakaliponya taifa. Ni maridhiano yaliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Afirika Kusini hadi leo wana Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kenya, Rais William Ruto alianza na mkwara kuwa “hakuna nusu mkate”, lakini leo ana Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Najua Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, yuko mahabusu anaendelea na kesi. Wala mimi siingilii ushahidi, lakini ukisikiliza watu wanavyosema huko nje, wanaiona kesi yake kuwa ni ya kisiasa zaidi kuliko uhalisia. Kwa upande mwingine wapo watu ukiwasikiliza wanamwona Lissu kama mtu asiye na fadhila kwa Rais Samia. Wanajiuliza mtu ambaye Rais Samia alikwenda kumwona hospitalini Nairobi, mtu aliyekwenda kumwona Ubeligiji, inakuwaje Lissu hathamini hata moja kati ya hayo aliyotendewa na Rais Samia?
Sitanii, Rais Samia ni kiongozi pekee wa Serikali ambaye bila kuogopa macho ya watu alitenda alilopaswa kulitenda. Aliweka kando mipaka ya kisiasa na akaenda kumwona Lissu katika mahangaiko yake ya matibabu. Na taarifa zipo kuwa hata baada ya Job Ndugai akiwa Spika (Mungu amlaze mahala pema peponi) kumkana Lissu akisema “hajui alipo”, Rais Samia kwa utu na sura ya ulezi wa Mama, alimlipa Lissu mafao yake yote ya ubunge.
Ndugu zangu Watanzania. Hapa tulipofika, naomba tufunge mlango wa lawama. Tushikamane, tuisubiri Tume ya Maridhiano, sote tushiriki. Kipindi cha nyuma vimekuwapo vyama vinavyosusia mazungumzo kama ilivyotokea kwenye suala la Kikosi Kazi cha hali ya Siasa Nchini. La kufahamu ni kuwa kususia si njia sahihi ya kujenga. Ni heri kujitokeza kama alivyofaya Maalim Seif Shariff Hamad Zanzibar, hadi akafanikisha kuweka alama ya mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 2010, iliyomaliza au kupunguza uhasama wa kisiasa kwa kiasi kikubwa Zanzibar. Tushikamane. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827


