Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Ukijenga nyumba nzuri, inakupasa usisherehekee sana kabla mvua haijanyesha. Kuna msemo kuwa tusubiri mvua inyeshe tuone panapovuja.

Msemo huu haulengi nyumba peke yake, bali unahusu jamii tunayoishi, taasisi mbalimbali tunazojenga na uhalisia katika maisha. Mwaka 2006 ilipoanzishwa kisheria Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), biashara ya mafuta ilikuwa huria.

Sitanii, ni wakati huo ambapo uchakachuaji wa mafuta ulikuwa wa kiwango cha lami. Mafuta yaliyokuwa yanauzwa katika vituo vyote vya mafuta nchini yalikuwa na madini ya risasi.

Baadaye EWURA ikaweka viwango kuwa mafuta yote yanayouzwa nchini lazima yasiwe na madini ya risasi (unleaded). Kwa lugha nyepesi, mafuta haya yalikuwa mekundu kama damu na ilikuwa petroli inalipuka kama risasi moto ukiisogelea. EWURA kwa Tanzania wamemaliza hili tatizo.

Wakati EWURA inaanza kufanya kazi vituo vya mafuta ilikuwa wanajipangia bei. Baadaye EWURA ikaja na mpango wa kutangaza bei za mafuta kila Jumatano ya mwisho ya mwezi. Zilifika nyakati, bei zikawa zinapanda kiholela haijapata kutokea. Kimsingi hili ndilo limenifanya niandike makala hii. Chini ya EWURA mafuta ni bidhaa pekee nchini ambayo katika soko la dunia bei zikipanda, hapa kwetu pia zinapanda, zikishuka, hapa kwetu pia zinashuka. Kweli si kweli?

Nchi zilizotuzunguka wao bei ikipanda, imeenda hiyo. Hairudi nyuma. Sote tunafahamu jinsi mbabe wa dunia, Donald Trump, alivyoanzisha vita dhidi ya nchi ya Iran. Vita hii ni mwendelezo wa vita ya Urusi na Ukraine. Urusi kabla ya vita ya Ukraine, ndiyo ilikuwa nchi ya pili kwa kuzalisha mafuta mengi duniani. Ilikuwa inazalisha mapipa milioni 12 kwa siku. Marekani ikaitumia Ukraine na sasa mafuta ya Urusi yamewekewa vikwazo.

Iran kwa siku inazalisha mapika milioni 3.3. Baada ya mafuta ya Urusi kuwekewa vikwazo, mafuta ya Iran yamekuwa ‘keki ya moto’, wamepata fedha nyingi ndani ya muda mfupi. Marekani haikupenda. Kama walivyoudanganya ulimwengu, wakaivamia Iraq na kuharibu mfumo wa uzalishaji mafuta, sasa wameingia Iran. Wanataka kuharibu mfumo wao wa uzalishaji wa mafuta. Ikiwezekana waweke vibaraka wao, wachote mafuta kama wanavyofanya Venezuela kwa sasa.

Sitanii, kwa bahati mbaya madhara yako wazi. Mchezo wao ni mauti yetu. Iran naye ameamua kufunga mlango wa Strait of Hormuz, ambao ni njia inayotumiwa na meli za mafuta kutoka kwa wazalishaji wakubwa wa mafuta; yaani nchi za Oman, Saudi Arabia na Qatar.

Mlango huu wenye upana wa kilomita 33, ndiyo njia kuu ya meli zinazosafirisha mafuta duniani. Kwa Iran kuufunga na kudungua meli zinazopita, ni wazi dunia inapata upungufu wa mafuta wa kutisha.

Marekani imejitutumua ikapeleka askari wake kulinda njia hii, Iran ikasema meli itakayopita itadunguliwa. Kweli meli kama tatu zimejaribu kupita zikadunguliwa. Kampuni za bima duniani zikasema haziwezi tena kuweka bima kwa meli inayopita kwenye eneo hili la Straight of Hormuz. Meli za mafuta bila bima, kuna hatari ya mtaji wa matajiri wanaofanya biashara hii kupotea siku moja. Nao wamesema hawasafirishi tena mafuta. Dunia bila mafuta ni janga.

Sitanii, nimeyasema haya kuonyesha kuwa kupanda kwa bei ya mafuta hapa kwetu kuwa Sh 3,820 kwa lita si kwa kupenda. Si siasa, bali ni uhalisia. Hapa dunia imepoteza mapipa milioni 15.3 kwa siku kwenye mzunguko na yanayozalishwa na nchi za Oman (mapipa milioni 1.02 kwa siku), Qatar (mapipa milioni 1.9 siku) na Saudi Arabia (mapipa milioni 10 kwa siku), hayafiki sokoni kutokana na Iran kufunga mlango wa Straight of Hormuz. Unaweza kufahamu hali iliyomo dunia kwa kuondokewa mafuta karibu mapipa milioni 28 kwa siku kutokana na vita hizi.

Nchi jirani katika sakata hili nyingi zimekimbia kuondoa kodi kwenye mafuta, ila haijawasaidia. Kenya kwa mfano Jumapili (Aprili 19, 2026) lita moja ya dizeli ilikuwa inauzwa Sh 206, sawa na Sh 4,738 za Tanzania. Nchini Uganda lita imeuzwa kwa Sh 5,290 sawa na Sh 3,677, Rwanda faranga 2,938 sawa na Sh 5,192, Burundi faranga 4,000 sawa na Sh 3,458. Kwa hiyo, Rwanda wananunua mafuta kwa Sh 1,372 juu zaidi yetu, Kenya wako juu zaidi yetu kwa Sh 918.

Sitanii, sisemi turidhike au tujivune kuwa sisi bei ya mafuta iko chini. Tunapaswa kutafuta suluhisho la kudumu. Zipo taarifa kuwa nchi yeatu inayo mafuta kwenye maeneo ya Ziwa Natron, Manyara. Zipo taarifa kuwa ukanda wa kusini ilipopatikana gesi katika mikoa ya Mtwara na Lindi kuna mafuta. Zipo taarifa kuwa Pemba na maeneo mengi kadhaa ya Zanzibar kuwa yana gesi na mafuta.

Jambo moja lenye A na B. Tanzania tuache kigugumizi. Tuchimbe mafuta. Angola walichimba, leo wanakula maisha. Pili, katika kuchimba mafuta tusichukue mkondo wa Uganda. Tujenge na kiwanda cha kusafisha mafuta. Mwalimu Julius Nyerere aliishajenga Tipper, hivyo huu utakuwa mwendelezo. Tusifanye kosa la kuchimba mafuta kisha kusafirisha kwenda Oman kusafishwa, mkataba wa hivyo tuukatae.

Baada ya kupitia mawanda marefu, nirejee katika umuhimu wa EWURA. Hii ni taasisi yenye nafasi ya kipekee katika kulinda ustawi wa sekta ya nishati nchini, hasa kwenye eneo la mafuta ambalo linaathiri moja kwa moja maisha ya wananchi na uchumi wa taifa.

Kupitia jukumu lake la udhibiti, taasisi hii huhakikisha mafuta yanapatikana kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa, na kwa bei inayozingatia hali halisi ya soko. Ndiyo maana kila kunapotokea changamoto kuhusu mafuta, wananchi wengi huiangalia EWURA kama taasisi yenye wajibu wa kutoa majibu na mwelekeo.

Katika kipindi hiki cha sakata la mafuta linaloendelea, mjadala umeongezeka kuhusu bei, upatikanaji wa bidhaa hiyo, pamoja na mabadiliko ya mara kwa mara ya soko. Hoja hizi zimevuka mipaka ya wananchi wa kawaida na kuingia bungeni, ambako wabunge kadhaa wameonyesha wasiwasi wao. Baadhi yao wameitaka serikali na EWURA kuongeza uwazi katika namna bei zinavyopangwa, huku wengine wakisisitiza haja ya kuwalinda wananchi dhidi ya mzigo wa gharama za maisha.

Mbunge mmoja alinukuliwa akisema kuwa: “Wananchi wanahitaji majibu ya wazi kuhusu kwa nini mafuta yanapanda kila mara, bila maelezo ya kutosha.” Kauli hii inaonyesha hitaji kubwa la mawasiliano ya mara kwa mara kutoka kwa mamlaka husika. Mbunge mwingine alieleza kuwa: “Sekta ya mafuta ni nyeti sana, taarifa zikichelewa hutengeneza hofu na sintofahamu kwa wananchi.”

Mbunge wa tatu alisisitiza kuwa: “Tunataka kuona uwajibikaji zaidi kwa taasisi zote zinazohusika na usimamizi wa mafuta.” Kauli hizi zinaonyesha kuwa hoja kubwa si mafuta pekee, bali pia namna taarifa zinavyotolewa kwa umma.

Hata hivyo, ni muhimu kutazama hali ya kikanda ili kupata picha pana zaidi. Wakati Tanzania inapitia changamoto hizi, baadhi ya nchi jirani zimekuwa na hali ngumu zaidi, ikiwamo uhaba wa mafuta, foleni ndefu vituoni, na kupanda kwa bei kwa kiwango kikubwa zaidi.

Katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Afrika Mashariki, wananchi wamewahi kushuhudia vituo vikikosa mafuta kwa siku kadhaa, jambo lililoathiri usafiri, biashara na huduma muhimu. Hii inaonyesha kuwa changamoto ya mafuta si ya Tanzania pekee, bali ni sehemu ya msukosuko mpana wa soko la dunia na usambazaji wa kikanda.

Katika mazingira haya, EWURA ina wajibu mkubwa wa kufuata mkakati madhubuti wa mawasiliano. Taasisi hii inapaswa kutoa taarifa za mara kwa mara zinazoeleza sababu za mabadiliko ya bei, hatua zinazochukuliwa, na matarajio ya soko. Pia iwe na msemaji anayepatikana kwa haraka kujibu maswali ya wananchi na vyombo vya habari. Uwazi wa taarifa utasaidia kuondoa uvumi unaoweza kuongeza taharuki.

Zaidi ya hayo, EWURA inapaswa kushirikisha wadau wote wakiwamo wafanyabiashara, wasafirishaji, wabunge na wananchi ili kujenga uelewa wa pamoja. Sekta ya mafuta inahitaji ushirikiano wa karibu, si lawama pekee. Pale ambapo wananchi wanaona taasisi inawasikiliza na kuwapa taarifa sahihi, imani huongezeka.

Kwa ujumla, EWURA ni nguzo muhimu katika sakata hili la mafuta. Ingawa changamoto zipo, Tanzania bado ipo kwenye nafasi bora ukilinganisha na baadhi ya nchi jirani zilizopitia hali mbaya zaidi. Kilichobaki sasa ni taasisi husika kuimarisha mawasiliano, kuongeza uwazi, na kuhakikisha wananchi wanaelewa kinachoendelea. Hapo ndipo imani ya umma itaimarika na taharuki kupungua. Najiuliza, bila EWURA bei ya mafuta ingefikia shilingi ngapi wakati huu?

Mwisho, naamini EWURA wanao Mkakati wa Mawasiliano, kama haujakaa hivi, wanipe kandarasi niupitie. Katika mazingira ya sasa, msemaji wa kwanza anapaswa kuwa Meneja Mawasiliano ya EWURA. Hali ikizidi kuwa mbaya, aseme Mkurugenzi Mkuu wa EWURA. Kama bado inatokota, aseme Katibu Mkuu (Nishati).

Kama bado tatizo lipo, aseme Waziri. Ikiwa bado kuna joto, walipeleke kwa Waziri Mkuu. Waziri Mkuu atanong’ona na Rais, kisha atamruhusu alisemee. Ikiwa bado ni la moto, Rais anaweza kutafuta nafasi ya kulisema. Mtiririko huu unatoa nafasi ya kusahihisha taarifa ambayo haijakwenda vizuri, ila wakubwa nyote mkikimbia eneo la kuzimia moto, sitashangaa mkisahau maji.

Aseme mmoja kwa wakati mmoja. Mafuta ni janga la dunia, tuliendee kwa utaratibu, ila mwisho wa siku, hili nalo litakwisha. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827