Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali imetoa Sh milioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya ikiwemo dawa na vifaa tiba pamoja na vitendanishi kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi Zaidi.
Hayo yameelezwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Jiji la Dodoma, Joshua Mwalongo wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, yenye lengo la kuwahabarisha juu ya maboresho na utekelezaji wa majukumu ya Bohari ya Dawa (MSD).
Amesema hospitali hiyo ilianza kujengwa mwaka 2023 na kuanza kutoa huduma mwaka huo huo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
“Uanzishwaji wa hospitali hiyo umeleta nafuu kubwa kwa wananchi baada ya kupunguza msongamano uliokuwa ukizikumba hospitali za rufaa na zile za muda mrefu kama Hospitali ya Mkoa wa Dodoma (General) na Makole, ambazo hapo awali zilikuwa zikihudumia idadi kubwa ya wagonjwa kwa wakati mmoja” amesema Dk Mwalongo.
Dk Mwalongo amesema hadi sasa zaidi ya Sh2.7 bilioni zimetumika katika ujenzi wake, ukiwa na jumla ya majengo 10, huku Serikali ikitoa Sh milioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya ikiwemo dawa na vifaa tiba pamoja na vitendanishi kuhakikisha huduma zinaanza kwa ufanisi.
“Awali hospitali za General na Makole zilikuwa zikilemewa sana na wagonjwa, lakini kwa sasa mzigo umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na huduma nyingi kuhamishiwa hapa Hospitali ya Jiji,” amesema Mwalongo.
Ameongeza kuwa hospitali hiyo kwa sasa inahudumia kati ya wagonjwa 600 hadi 700 wa nje kwa mwezi, huku wajawazito wanaofika kupata huduma wakifikia takriban 60 kwa wiki.

‘Kadri siku zinavyosonga ndipo idadi ya wagonjwa katika vitendo mbalimbali ikiongezeka, ambapo kwa sasa tunawahudumia hadi 700 kutoka nje, huku huduma za mama wajawazito nazo idadi yao ikiongezeka ulikinganisha na awali” amesema.
Kwa mujibu wa Mwalongo, hospitali hiyo inatoa huduma mbalimbali zikiwemo za wagonjwa wa nje, afya ya mama, baba na mtoto, huduma za uzazi, mionzi (radiology), meno, pamoja na huduma za kuhifadhi miili (mochwari).
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma zote zinazopatikana katika hospitali za rufaa zinapatikana pia katika hospitali za wilaya na za jiji ili kupunguza adha kwa wananchi,” amesema.
Mbali na kupunguza msongamano, hospitali hiyo pia imekuwa chanzo cha ajira kwa vijana, ambapo wengi wa watumishi wake ni wa ajira mpya wanaopata nafasi ya kujifunza na kuendeleza taaluma zao.
Katika kuboresha upatikanaji wa dawa, Mwalongo ameipongeza MSD kwa ushirikiano wake, akisema imekuwa ikihakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wakati.

Kwa upande wake, Meneja wa Mawasiliano wa MSD, Etty Kusiluka amesema kuanzishwa kwa hospitali hiyo kumeenda sambamba na kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi, zikiwemo huduma za maabara, upasuaji na meno.
“Huduma za meno sasa zimeboreshwa zaidi, siyo kung’oa tu jino bali tunatoa matibabu ya kisasa yanayolenga kulihifadhi jino,” amesema Kusiluka.
Naye Meneja wa Kanda ya MSD Dodoma, Mwanashehe Jumaa amesema ndani ya miaka mitano iliyopita Serikali imefanikiwa kuhakikisha kila halmashauri inakuwa na hospitali yake, hatua iliyosaidia kupunguza utegemezi kwa hospitali chache zilizokuwa zikilemewa.
Ameeleza kuwa vituo kama Makole na Kilimani vilikuwa na mzigo mkubwa wa wagonjwa, lakini sasa huduma zimeboreshwa na kusambazwa katika hospitali mpya ikiwemo Hospitali ya Jiji na MSD imewezesha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa wakati.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa dawa, Mfamasia wa Jiji la Dodoma, Magreth Mhalule amesema hali imeimarika kwa kiasi kikubwa, huku upatikanaji wa dawa muhimu ukifikia asilimia 91.

“Hapo awali kulikuwa na changamoto ya uhaba wa dawa, lakini sasa hali imeimarika kutokana na Serikali kuongeza bajeti ya ununuzi wa dawa kutoka Sh900 milioni hadi zaidi ya Sh1 bilioni,” amesema.
Aidha, amesema hospitali hiyo inapaswa kuwa na aina 203 za bidhaa za afya, zikiwemo dawa, vifaa tiba na vitendanishi, huku dawa zinazohitajika zaidi zikiwa ni za maumivu (antipain) na antibiotiki kutokana na ongezeko la maambukizi ya bakteria.
Kwa upande wa huduma za meno, Daktari wa meno, Abisai Sadaka amesema kitengo hicho kimekuwa kikipokea angalau wagonjwa 10 kwa siku, wengi wao wakiwa na matatizo ya meno kuoza na magonjwa ya fizi.
Amesema tofauti na ilivyozoeleka, matibabu ya meno kwa sasa yanalenga zaidi kuhifadhi jino badala ya kuling’oa, kwa kutumia teknolojia ya kisasa ikiwemo matibabu ya mzizi wa jino (root canal).
“Tunawahimiza wananchi kutumia dawa za meno zenye fluoride ili kulinda afya ya meno na kuhakikisha wanabaki na meno yao hadi uzee,” amesema.

Naye Mtaalamu wa Teknolojia ya Mionzi, Bertha Magembe amesema ujio wa vifaa vya kisasa hospitalini hapo umeongeza ufanisi wa huduma na kupunguza muda wa kusubiri matibabu.
Amesema kwa sasa anahudumia hadi wagonjwa 20 kwa siku tangu aanze kazi Juni 2025, akibainisha kuwa hospitali za Serikali zimeboreshwa kwa vifaa na wataalamu waliobobea.
“Huduma zote ambazo daktari anakuandikia unazipata hapa bila kuchelewa, na ubora wa vifaa ni wa kiwango cha juu,” amesema.
Kwa ujumla, uwekezaji huo wa Serikali katika Hospitali ya Jiji la Dodoma umeanza kuonyesha matokeo chanya, ukiwa sio tu umepunguza msongamano wa wagonjwa, bali pia umeongeza upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wa Dodoma na maeneo ya jirani.





