Hivi kweli Polepole ni mwanaharakati?

DODOMA

Na Javius Byarushengo

Huwa sipendi kuandika maisha ya mtu binafsi, isipokuwa kama kuna ulazima na kwa masilahi ya taifa.

Kwa miezi kadhaa sasa Mbunge wa Kuteuliwa, Humphrey Polepole, kwa kutumia kipindi alichokianzisha mtandaoni cha ‘Shule ya Uongozi’, amekuwa akizungumzia masuala mbalimbali ya serikali na wakati mwingine ya Chama (chake) Cha Mapinduzi (CCM).

Ukifuatilia kwa makini mafundisho yake ya ‘shule ya uongozi’ unabaini kwamba Polepole ni mwanasiasa/kiongozi mwenye uwezo wa kujenga hoja, mwenye kujiamini na ni mbunifu.

Si tu anazo sifa hizo pekee, bali pia ni mchambuzi makini kutokana na uelewa wake wa mambo bila kusahau sifa ya ukweli.

Hata hivyo, pamoja na sifa zote alizonazo kijana huyu machachari katika siasa za Tanzania, baada ya kuanzisha kipindi hicho, licha ya kuungwa mkono na watu wengi, hasa vijana wanaomfuatilia, bado wengine wamekuwa wakimkosoa vikali hadi kufikia hatua ya kumuita msaliti na mnafiki anayepigania tumbo lake.

Inaweza ikawa vigumu kuelewa kwa nini wanaompinga Polepole wanamuita msaliti na mnafiki lakini ukifuatilia kwa makini wengi wanatumia hoja ya suala la Katiba mpya.

Wakati wa mchakato wa kutafuta katiba mpya miaka ya 2011 – 2014; mchakato uliotumia mabilioni ya fedha za walipa kodi, Polepole alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiipigania kweli kweli.

Ajabu mwaka 2015 ilipoingia madarakani Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli aliyetamka hadharani kuwa suala la katiba mpya si kipaumbele chake kwa kuwa anataka kujenga nchi kwanza, watu wakabaki wakiugulia mioyoni huku Polepole aliyekuja kuwa mmoja wa watu muhimu katika serikali hiyo, akipatwa ububu wa ghafla katika suala la katiba mpya.

Ikumbukwe kuwa mchakato wa kupata katiba mpya ulianza tangu mwaka 2010, wakati Rais wa wakati huo, Dk. Jakaya Kikwete, alipotangaza nia ya serikali ya kuanzisha mchakato huo.

Mchakato ukaanza rasmi mwaka 2011 kwa kutungwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83/2011 na baadaye sheria ya Kura ya Maoni Na. 11/2013.

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilitamka kuanzishwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Ikaanzishwa chini ya Mwenyekiti Jaji Joseph Warioba, ikaratibu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya kwanza ya katiba ambayo kupitia uhariri wa Mabaraza ya Katiba, ikapatikana Rasimu ya Pili ya Katiba.

Rasimu hii ya pili, maarufu kama ‘Rasimu ya Warioba’, ikawasilishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba (BMK) lililokuwa na wajumbe wengi kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Ndani ya BMK kukaibuka mivutano mikali kuhusu masuala kadhaa yaliyomo kwenye Rasimu, ndipo baadhi ya wajumbe hasa kutoka upinzani wakaamua kujitoa na kususia mchakato.

Hata hivyo, waliobaki waliendelea na ikapatikana Katiba pendekezwa ambayo wengi waliiona kama imekosa muafaka na maridhiano ambayo yanaonekana kama ndio msingi wa kupata Katiba bora ya kitaifa yenye kukubaliwa na wengi.

Mchakato ukaishia hapo mwaka 2014. Ni dhahiri kwa wanaomfahamu vizuri Polepole kwamba ni mwanasiasa mtetezi, walitegemea kwa kuwa ndani ya Serikali ya Awamu ya Tano inayopinga mchakato ulioishia njiani, hatanyamaza, bali angetumia ushawishi wake kumrudisha Magufuli katika njia sahihi. Hakufanya hivyo.

Polepole alitakiwa kumrudisha JPM katika mstari kwa kuzingatia kuwa Katiba mpya ndiyo ingeondoa changamoto mbalimbali zikiwamo kero za Muungano, Tume Huru ya Uchaguzi, mamlaka yanayotajwa kuwa makubwa ya Rais na madaraka ya umma.

Masuala mengine ni Haki za Binadamu na Utawala Bora. Mgombea binafsi na mgawanyo wa madaraka ya mihimili mitatu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) pamoja na uhuru wa Bunge na Mahakama.

Kutokana na udhaifu uliomo katika Katiba ya sasa inayompa Rais mamlaka makubwa, inasemekana JPM alitumia udhaifu huo kuhakikisha serikali inatunga sheria kali za kuvibana vyombo vya habari na wakati mwingine akitoa hadharani matamko makali dhidi ya vyombo vilivyokuwa vinachokonoa mambo. Polepole hakusema lolote!

Nani hakumbuki Serikali ya Awamu ya Tano ilivyotunga Sheria ya Takwimu kwa lengo la kuzuia uhuru wa kuweka takwimu sahihi? Je, Polepole hakuwapo?

Je, mamlaka makubwa ya Rais kutokana na katiba iliyopo yaliyoiwezesha serikali kuingilia uhuru wa Bunge hadi kulifungia lisionyeshwe mubashara, Polepole anayeibuka sasa wakati huo alikuwa wapi?

Je, wakati ilipoonekana wazi Rais anaingilia uhuru wa Mahakama, Polepole mbona aliendelea kulinda mkate wake bila kusema lolote?

Je, kwa nini Polepole aliubana ulimi wake huku haki ya uhuru wa wananchi kudai haki zao, uhuru wa kuandamana, kutoa maoni na vyama vya siasa kufanya mikutano ya nje vikiporwa na serikali?

Katika muktadha huo, wadadisi wa masuala ya siasa wanadai kuwa japo Magufuli alikuwa akijinadi kuwa yeye si mwanasiasa, lakini kiuhalisia siasa alikuwa anazijua kweli kweli.

Wadadisi wanasema Magufuli siasa alizijua kweli kwa maana alikuwa mjanja kuwanunua kwa akili wanasiasa walioonekana wana vidomodomo na ndiyo maana katika kipindi chake wabunge wengi wa upinzani walikimbilia CCM kwa kivuli cha ‘kuunga mkono juhudi’ zake.

Magufuli kwa kutambua kuwa Polepole ana ‘kidomodomo’ chenye ushawishi mkubwa kwa chama na jamii, alihakikisha anapewa minofu ya kumpumbaza, ikiwamo ukuu wa wilaya, baadaye kuwa Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, kasha Mbunge wa Kuteuliwa.

Si tu Polepole kupata vinono hivyo, bali pia alipewa mamlaka makubwa ya kutamka chochote kwa sauti ya ukali mpaka viongozi wengine ndani ya chama na serikali kumuogopa.

Sasa ni Awamu ya Sita ambayo licha ya kumbakizia ubunge wa kuteuliwa, lakini kwa kitendo cha kumuondolea ukatibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM na mamlaka ya kutamka chochote, kwa wakati wowote anaoutaka, inasemekana vinamuumiza kijana huyu, kwani umaarufu wake umezikwa.

Je, Polepole aliyekuwa mwanasisa wa ‘ndiyo mzee’ katika serikali iliyopita, huku akitumia fursa ya uhuru wa kujieleza katika serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kujifanya anatoa ‘shule ya uongozi’ ili kuwalaghai Watanzania wenye historia ya kusahau matukio ya nyuma, si ndiyo inaleta tafsiri ya unafiki na usaliti wenye nia ya kusaka tonge na umaarufu?

[email protected], 0756521119