Soko la ajira jinamizi linalowatesa wahitimu

Madhumuni ya elimu ni kumkomboa mhitimu kifikra ili aweze kuyamudu na kuyatawala mazingira yanayomzunguka. Elimu pia inatoa nafasi kwa mhitimu wa ngazi fulani kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku.

Elimu wakati wa ukoloni ilitolewa kwa matabaka makubwa ambayo yalilenga kuwapatia elimu bora watu weupe na kuwapatia Waafrika elimu ya tabaka la chini.

Kwa kutambua umuhimu wa elimu katika maendeleo endelevu ya jamii na taifa kwa ujumla, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere baada ya kupata Uhuru wetu mwaka 1961 alianzisha elimu ya kujitegemea kuanzia shule za msingi.

Pamoja na malengo ya kupata wataalamu wa fani mbalimbali wakiwamo viongozi, elimu pia ililenga kuwawezesha wahitimu kujitegemea badala ya kutegemea tu kazi za kuajiriwa maofisini.

Katika harakati za kuhakikisha elimu inawasaidia wahitimu kujitegemea, zilianzishwa shule za michepuo maalumu kama vile shule za ufundi, kilimo, biashara na vyuo vya kati vinavyobeba wahitimu wengi hapa nchini.

Miaka 60 tangu tupate uhuru wa nchi yetu, tumepiga hatua kubwa sana katika sekta ya elimu. Kumekuwa
na idadi kubwa ya shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati, vyuo vikuu hapa nchini. Kwa hili hatuna budi kujipongeza na kuendelea kuweka mikakati zaidi ya kuboresha elimu yetu.

Pamoja na mafanikio hayo kumekuwa na mijadala mingi isiyokwisha kuhusu soko la ajira kwa vijana wanaohitimu mafunzo katika ngazi mbalimbali za elimu hapa nchini. Tatizo ambalo limeendelea kuwa gumzo hata kwa mataifa mengine duniani kote.

Vijana wengi wanapokuwa masomoni hutegemea kuajiriwa mara wamalizapo masomo yao, ndoto ambayo imeendelea kuwatesa pale soko la ajira linapokuwa chungu kwao na mara nyingi huitupia lawama nyingi serikali kwa kushindwa kutoa ajira za kutosha.

Ni wahitimu wachache sana wenye malengo ya kujiajiri baada ya kumaliza kozi zao, wengi wanalalamikia
mitaji kama kianzio cha kujiajiri na baadhi kutokuthubutu kabisa kujiajiri miaka nenda – miaka rudi, wamekaa wakisubiri ajira serikalini. Ndoto ambayo imekuwa ngumu sana hata kwa serikali kuwatimizia wahitimu wote.

Kila mwisho wa mwaka wanafunzi huhitimu masomo ya ngazi tofauti za elimu nchini, hasa vyuo, na hivyo kuwa tayari kuingia kwenye soko la ajira.

Soko la ajira linatazamwa katika sera mbili kuu; kwanza ni kuajiriwa
au kujiajiri. Ili kuingia katika soko la ajira kwa urahisi bila kujali ni kuajiriwa au kujiajiri kuna mambo muhimu ya kuzingatia.

Wana uchumi wanasema ni vizuri kwa wahitimu wazazi, walezi na taasisi za elimu kuelewa ni kwanini kunakuwa na uhaba wa ajira sokoni.

Uhitaji wa nguvu kazi unapokuwa mkubwa kuliko waombaji kunakuwa hamna tatizo la ajira kinyume cha hapo kuna kuwa na tatizo la ajira.

Wahitimu wanapokuwa wengi kuliko mahitaji ya waajiri kwa kuzingatia idadi na ubora, baadhi yao hukosa ajira kwa kigezo hicho.

Inaelezwa kwamba waajiri wanaajiri pale kunapokuwa na huitaji wa bidhaa na huduma wanazozalisha. Hii ni kwa sababu waajiriwa huwagharimu waajiri walio wengi.

Pamoja na hayo waajiri wengi hutazama mambo mbalimbali kwa wanaotaka kuajiriwa kama wana sifa na vigezo vinavyokwenda sambamba na matakwa ya taasisi zao.

Kwa maana nyingine waajiri wengi hawaajiri tu mtu yeyote bali hutaka kupata nguvu kazi itakayowawezesha kumudu ushindani sokoni. Wanataka watu madhubuti wenye ubora wa hali ya juu kulingana na kiwango cha taasisi husika.

Miongoni mwa mambo mengi wanayotazama waajiri ni pamoja na ujuzi wa wahitimu waliosomea darasani kuendana na mahitaji ya taasisi husika ili kuleta ufanisi zaidi.

Ni muhimu kwa taasisi za elimu nchini kutoa wahitimu wenye utaalamu unaohitajika sokoni. Ni jukumu la wanafunzi pia washauri hata wazazi
na walezi kuhakikisha kabla ya
kuanza masomo wanayafahamu mahitaji ya soko. Pamoja na utaalamu unaofundishwa darasani, waajiri hutafuta sifa za ziada kwa wahitimu wanao wahitaji ambazo hutofautiana kutoka kwa mwajiri mmoja hadi mwingine.

Hata hivyo sifa za msingi zinazotakiwa na waajiri wengi ni uwezo wa kufanya kazi na watu wengine, kujiamini na kuchangamana na wengine kirahisi.

Zingine ni kuwa na uwezo wa kusikiliza, kuandika na kuwa na lugha sahihi ya mwili katika mazingira tofauti, pia waajiri wanataka ubunifu, uvumilivu, ujasiri, kujituma, uwezo wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, kujitoa kuwa na mtazamo mpana na uwezo wa kubadilika kulingana na mazingira.

Sifa nyingine anazopaswa kuwa nazo mwajiriwa ni kuonyesha nia ya kujifunza wakati wowote kuendana na mabadiliko yanayotokana na kazi au kitengo chake.

Ifahamike kuwa siku hizi waajiriwawengi wanaomba kufanya kazi ambazo kimsingi zilikuwa hazihusiani na nafasi zao.

Lakini kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia, kazi zinabadilika na watafuta ajira inabidi waonyeshe nia ya kukua na kujifunza kwa pamoja kukubaliana na mabadiliko hayo.

Katika hali ya kukidhi sifa na vigezo hivyo, kumekuwa na mijadala mingi hapa nchini inayoendeshwa na wasomi na wanazuoni wengi wakipendekeza kuangalia upya mfumo wetu wa elimu ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete amesema uwekezaji kwenye sayansi na teknolojia utazidi kuboresha elimu na kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana. Jumanne ya Mei 18, mwaka huu akifungua kongamano la elimu lililoandaliwa na mtandao wa elimu Tanzania (Tenment), Kikwete alisema kutokana na utafiti uliofanywa na Tume ya Taifa ya Elimu ambayo yeye ni mjumbe, elimu inayotolewa barani Afrika inapaswa kuboreshwa ili kutoa suluhisho la changamoto ya ajira
kwa vijana.

“Kumetakiwa kuwapo matumizi ya sayansi na teknolojia katika ufundishaji. Kila shule inatakiwa kuunganishwa na internet,” amesema.

“Ifikapo mwaka 2050 asilimia 50 ya kazi zitafutika kwa sababu ya kukua kwa sayansi na teknolojia, kwa hiyo tunapaswa kubadilika sana,” anasisitiza Kikwete.

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani Machi 19 amesisitiza juu ya mabadiliko ya mitaala kwa kuingiza mafunzo ya ujuzi kwenye mitaala hiyo ili kuwaweza wahitimu waweze kujiajiri.

“Mimi naomba tuangalieni mitaala yetu. Tuangalieni sisi ni Watanzania, tuangalieni mtaala unao tupeleka mbele na utakaokuza viwanda vyetu. Tuna viwanda vingi lakini ‘skilled labour’ hatuna,” anasema Rais Samia.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo, Profesa Joyce Ndalichako, anasema soko la ajira Tanzania na duniani limehamia kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vya ufundi. Hivyo
ni wakati muafaka sasa kuendelea kuboresha mitaala ya vyuo ili kuweza kupata wataalamu wabobezi wenye kusukuma gurudumu la maendeleo na uchumi wa taifa letu.

Akizungumza katika kongamano la ‘Kigoda cha Mwalimu Nyerere’ Julai mwaka huu, Askofu Dk. Benson Bagonza alisema si lazima kijana wa chuo kikuu apate ‘A’ kwenye masomo yake ndiyo apate ajira au mafanikio, bali ajitambue na kutambua mazingira yanayomzunguka.

“Watu wote waliofanikiwa kimaisha lazima wawe na ‘social intelligence’ (wamejielewa na kuwaelewa wengine) kwa hiyo si lazima kupata ‘A’ ndipo ufanikiwe unaweza kupata hata ‘C’ lakini kama una ‘social intelligence’ utafanikiwa tu,” anasema Dk. Bagonza.

JAMHURI Jumanne Desemba 28, 2021 – Januari 3 , 2022

0755-985-966