Na Mwandishi Wetu , JamhuriMedia, Dodoma
Upatikanaji wa uhakika wa dawa na vifaa tiba nchini na kuwa na akiba ya kutosha kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita, umeiongezea sifa Bohari ya Dawa (MSD) licha ya kuwepo kwa mzozo Mashariki ya Kati.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari mkoani Dodoma katika kikao kazi kilichoandaliwa na MSD.
Amesema MSD imejipanga kuhakikisha upatikanaji endelevu wa dawa na vifaa tiba unaimarishwa ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mikakati thabiti ya kukabiliana na changamoto yoyote.
” Tayari kuna tathmini inayoendelea kufanywa na timu maalumu ya wataalamu ili kubaini hatari zinazoweza kujitokeza na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana nazo” amesema.
Mavere amesisitiza juhudi zinaendelea kuimarishwa, hasa katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi hauathiriki na mabadiliko ya hali ya usalama na uchumi wa kimataifa.
Amesema Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa hali hiyo ili kuhakikisha huduma za afya nchini haziathiriki na wananchi waendelee kupata huduma bora bila usumbufu.
Mganga Mkuu Hospitali ya Manyoni Dk Bwire Robert ameishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa Hospitali hiyo ambayo imepunguza msongamano katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na Hospitali ya Makole ambapo wananchi wanapata huduma bora huku vifaa tiba vikitolewa na MSD kwa wakati.
Amesema kuwa asilimia 99 ya dawa hutolewa na MSD ambapo huduma hut9lewa kwa njia ya mtandao ambayo imerahisisha huduma ukilinganisha na awali.
“Hivi sasa uagizaji dawa kuy9ka MSD hufanyika kwa njia ya teknolojia tofauti na awali, kumekuwa na mafanikio makubwa sana na hupatikana kwa wakati sahihi, haya yote ni mafanikio makubwa yanayofanywa na Serikali katika kuhakikidha huduma bora za afya zinapatikana nchini” amesema.
Amesema kutokana na mafanikio hayo hata baadhi ya huduma zimeongezwa na kuwarahisishia wananchi kupata huduma bora na zenye uhakika.
Meneja MSD Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa amesema kupatikana huduma bora kwa Hospitali hiyo imesaidia kupunguza sambamba kupunguza msongamano katika hospitali zingine .
Amewahakikishia Watanzania kuwa MSD itaendelea kupeleka dawa na vifaa tiba vya kisasa kwa wakati.
Mfamasia kutoka kitengo cha Mipango, Ufuatiliaji na Tathimini wa MSD, Lilian Bwiro, amesema kumekuwepo na mafanikio katika kipindi cha miaka minne 2021/22 hadi mwaka 2024/25.
Amesema katika kipindi cha miaka minne mapato ya MSD yameongezeka kwa asilimia 103 kutoka Sh.Bilioni 315.12 hadi kufikia kiasi cha Sh.Bilioni 640,5 mwaka 2024/25.
Pia mafanikio mengine ni kuongezeka kwa upatikanaji wa bidhaa za afya ashiri kutoka asilimia 42 mwaka 2021/22 hadi kufika asilimia 73 Machi, 2026.
“Hali ya utimizaji wa mahitaji wa vituo vya kutolea huduma za afya umeendelea kuongezeka kutoka asilimia 4l hadi kufikia asilimia 77 katika kipindi cha miaka minne.” amesema.
Pia amesema mafanikio mengine ni kuongezeka kwa mizunguko ya usambazaji wa bidhaa za afya kwenda vituo vya kutolea huduma za afya kutoka mizunguko minne kwenda mizunguko sita kwa mwaka ,huku ununuzi wa bidhaa za kuwezesha uzazi pingamizi ( CEmONO) ukifikia asilimia 100 ya MS.
Magesa ameongeza kuwa mafanikio mengine mashine 162 za kusafisha damu (dialysis) zimesambazwa kutoka mashine 60 mwaka 2021/2022 zilizogharimu Sh.bilioni 10.14
Pia kukamilisha ujenzi wa maghala ya kisasa yanayokidhi viwango vya uhifadhi na kuanza kutumika katika Kanda ya Dodoma na Mtwara -mita za mraba 12,000.
Aidha kuanza kwa ujenzi wa ghala la Chato mkoani Geita lilifikia asilimia 42 ya utekelezaji.
Mafanikio mengine ni uanzishwaji wa kampuni tanzu ijulikanayo kama MSD Medipharm Manufacturing Company yenye jukumu la kusimamia uzalishaji unaotekelezwa kibiqshara na kwa ufanisi mkubwa .
“Pia kiwanda cha mipira ya mikono -Idofi kukamilika na kuanza kazi rasmi ya uzalishaji Februari 2024 pamoja na ongezeko la thamani ya bidhaa zinazonunuliwa kutoka kwa wazalishaji wa ndani kutoka Sh.bilioni 15.90 zilizonunuliwa mwaka 2021/22 hadi Sh.bilioni 98.72 mwaka 20/2024/25.”








