Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

CHAMA Kikuu cha Ushirika wa Wakulima (IGEMBEMBENSABO) kimeeleza kufurahishwa na mafanikio makubwa waliyopata wakulima wa zao la choroko na mazao mengine katika msimu uliopita na matarajio yao makubwa msimu huu.

Meneja Mkuu wa Chama hicho kinachosimamia wakulima wa Wilaya za Igunga na Nzega, Baraka Samwel Kiboye ameeleza kuwa mafanikio hayo yamechochewa na kazi nzuri inayofanywa na serikali ya Awamu ya Sita kuinua sekta ya kilimo.

Alieleza kuwa katika msimu uliopita wakulima walizalisha jumla ya tani 1,800 za choroko kati ya makisio ya tani 2,000 na kuziuza kwa bei ya sh 1,500 kwa kilo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani tofauti na ile ya kawaidia ya sh 800 hadi 1000.

‘Baada ya mauzo wakulima walilipwa zaidi ya shilingi bilioni 2.7 na zote ziliingia katika mifuko yao, haya ni mafanikio makubwa sana, na mwaka huu tunatarajia kupata kilo nyingi zaidi na zote zitauzwa kwa mfumo huo huo’, alisema.

 Kiboye aliongeza kuwa pia wameanzisha utaratibu wa wakulima kuuza mazao yao kwenye mnada wa hadhara kwa bei ya ushindani na kwa mwaka huu minada 5 imeshafanyika ambapo zaidi ya tani 2500 za mazao mchanganyiko zimeshauzwa.   

Alitaja mazao yanayolimwa na kuuzwa katika mnada huo kuwa ni dengu, ufuta, pamba, choroko na mpunga, na kuongeza kuwa umekuwa na manufaa makubwa sana kwa wakulima kwa kuwa wanauza kwa uwazi na kwa fedha taslimu.   

Meneja Mkuu aliongeza kuwa zao la pamba nalo limeendelea kuwa mkombozi kwa wakulima kwani msimu uliopita walizalisha jumla ya kilo 27,000 na kupata zaidi ya shilingi bilioni 33, na hizi ziliingia katika mifuko yao.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Chama hicho Joseph Mlemeja Ngelya aliishukuru serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya kilimo nchini na kuwapatia mbolea ya ruzuku wakulima.

Alieleza kuwa katika misimu 2 hadi 3 iliyopita uzalishaji wa mazao ya wakulima umeongezeka mara dufu kutokana na kuwezeshwa mbegu bora, kupata pembejeo ya bei nafuu kwa wakati na kupanua wigo wa masoko.

Aidha aliongeza kuwa msimu uliopita wameanza kuhamasisha kilimo cha zao la tumbaku inayokaushwa kwa upepo na hadi sasa vyama vya msingi 13 vimeishwa kulima zao la tumbaku.