Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Wakati Serikali ikiendelea kutekeleza uwekezaji wa mabilioni ya shilingi katika reli ya kisasa (SGR), usafiri wa anga, majini na barabara, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimejipanga kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kisasa watakaohakikisha miradi hiyo inaendeshwa kwa ufanisi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mkuu wa Chuo hicho Mhandisi Dkt. Prosper Mgaya, amesema hayo Jijini hapa Agosti 3,2026 wakati akizungumza na Waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya habari Maelezo.

Amesema Serikali imeendelea kuimarisha chuo hicho ili kiwe kitovu cha kuzalisha wataalamu wanaokidhi mahitaji ya sekta ya uchukuzi, sambamba na kasi ya uwekezaji unaoendelea kufanyika nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dkt. Mgaya alisema NIT kilianzishwa mwaka 1975 kama kitengo cha Shirika la Usafirishaji la Taifa kabla ya kupandishwa hadhi mwaka 1982 kuwa taasisi ya elimu ya juu yenye jukumu la kutoa mafunzo, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu katika sekta ya uchukuzi.

Ameeleza kuwa baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, Tanzania ilikumbwa na upungufu mkubwa wa wataalamu wa sekta ya usafirishaji, hali iliyochochea Serikali kukiimarisha chuo hicho ili kizalishe wataalamu wa usafiri wa barabara, reli, anga na majini.

Dkt. Mgaya ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika sekta ya uchukuzi, akitaja ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ununuzi wa ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ujenzi na ukarabati wa meli pamoja na maboresho ya viwanja vya ndege.

Alisema miradi hiyo imeongeza kwa kiasi kikubwa mahitaji ya wataalamu wenye ujuzi maalumu, jambo lililoifanya NIT kupanua programu zake za masomo ili kuandaa wahitimu watakaoweza kusimamia, kuendesha na kutunza miundombinu hiyo kwa viwango vinavyohitajika.

“Kadiri Serikali inavyoendelea kuwekeza katika sekta ya uchukuzi, ndivyo mahitaji ya wataalamu wenye ujuzi yanavyozidi kuongezeka. NIT imejipanga kuhakikisha taifa linapata wataalamu watakaokwenda sambamba na maendeleo hayo,” alisema.

Amesisitiza kuwa sekta ya uchukuzi ni mhimili muhimu wa maendeleo ya uchumi wa taifa kwa kuwa inaunganisha shughuli za uzalishaji, biashara na uwekezaji, hivyo uwekezaji katika elimu na maendeleo ya wataalamu wa sekta hiyo ni nguzo muhimu ya kuhakikisha miradi mikubwa ya kimkakati inaleta manufaa kwa Watanzania na kuongeza ushindani wa uchumi wa nchi.