Na Elisante John, JamhuriMedia, Singida

‎Ajali ya gari la Polisi imeua watu 12, wakiwemo askari watano na mahabusu saba, baada ya kugongana na lori la mafuta katika eneo la Mlima Sekenke, Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida. Ajali hiyo imetokea leo Jumatatu, Septemba 21, 2026, saa mbili asubuhi katika barabara ya Singida–Nzega.

‎Gari la Polisi lenye namba PT 1982, aina ya Toyota Land Cruiser, lililokuwa limebeba mahabusu wanane na askari watano, lilikuwa likipanda mlima huo wakati lilipogongwa na lori la mafuta aina ya Mark, lenye namba REF 245 X na trela RL 4255, lililokuwa likishuka mlima. Lori hilo lilikuwa likisafirisha mafuta kutoka Dar es Salaam kwenda nchini Rwanda.

‎Katika ajali hiyo, askari wote watano na mahabusu saba walifariki dunia, huku mahabusu mmoja na dereva wa lori wakinusurika. Walionusurika wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba, iliyopo Kiomboi. Mahabusu huyo ametajwa kuwa Petro Nkana (45), mkazi wa Kijiji cha Migela, Tarafa ya Shelui, ambaye amepata majeraha kichwani na mikononi.

‎Askari waliofariki ni Frank Mwasapili (45), ofisa wa Polisi katika Kituo Kidogo cha Polisi Shelui; dereva wa gari hilo Hussein Haji (54); Paul Gabriel (45); Ashiraf Salumu Heri (25) na Ramadhan Mushi, wote wa Kituo Kidogo cha Polisi Shelui. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Amon Daud Kakwale, amewataja mahabusu waliofariki kuwa ni Timotheo Kimaro (38), Frady Mazoa (55), Mariamu Hamisi (61), Alfred Amosi (65), Hussein Hussein, Vivian Said (67) na Casian Hassan, waliokuwa wakazi wa vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Iramba.

‎Kamanda Kakwale amesema dereva wa lori, Ndandalesa Alphonce (26), raia wa Rwanda, anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba akiwa chini ya ulinzi wa Polisi, akisubiri kuhojiwa kuhusu ajali hiyo.

Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha ajali hiyo ilitokea wakati lori lililokuwa likishuka Mlima Sekenke kuhama upande hadi sehemu ya gari la Polisi lililokuwa likipanda na kusababisha ajali hiyo mbaya. Kakwale amewataka watumiaji wa barabara hiyo kuzingatia alama za usalama na mabango ya tahadhari yaliyowekwa katika eneo lote la mlima.

‎Aidha, Kamanda Kakwale amesema Jeshi la Polisi linaendelea na maandalizi ya kusafirisha miili ya askari waliofariki katika ajali hiyo kwenda mbalimbali nchini. Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini kwa kina mazingira yaliyosababisha ajali hiyo.