Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeingia katika mwaka wa fedha 2026/27 likiwa na rekodi ya faida ya Shilingi bilioni 72.98, huku shughuli zake za mafuta na gesi asilia zikiendelea kuongeza mapato ya Serikali na kufungua fursa za ajira, biashara na uwekezaji kwa Watanzania.
Mkurugenzi mtendaji wa TPDC Mussa Makame amezungumza hayo leo, Septemba 21, 2026, kwenye mkutano wake na Waandishi wa habari Jijini hapa ambapo amesema pamoja na faida hiyo, TPDC ililipa kodi za jumla ya Shilingi bilioni 50.04, huku ikichangia Shilingi bilioni 142.61 kupitia mgawo wa faida ya gesi na mrabaha kwenye mfuko wa mapato ya mafuta na gesi.
Mbali na hayo, ameeleza kuwa Shirika hilo lililipa gawio la Shilingi bilioni 15.118, hatua inayoifanya shughuli za kibiashara za mafuta na gesi kuwa sehemu muhimu ya mchango wa sekta ya nishati katika uchumi wa Taifa na utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Amesema TPDC kwa kushirikiana na waendeshaji wa Vitalu vya Songosongo na Mnazi Bay, imeendelea kuzalisha wastani wa futi za ujazo milioni 170 za gesi asilia kwa siku, ambapo sehemu kubwa ya gesi hiyo inatumika katika uzalishaji wa umeme, huku nyingine ikienda viwandani, taasisi na majumbani.
Wakati uzalishaji ukiendelea, Serikali kupitia TPDC imefikia hatua kubwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwamo Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ambalo Tanzania inamiliki asilimia 15. Mradi huo umefikia asilimia 92.7 ya utekelezaji na tayari umezalisha ajira 10,000, ambapo 7,500, sawa na asilimia 75, zimenufaisha Watanzania.
“Ushiriki wa Watanzania katika EACOP umeenda sambamba na ushiriki wa kampuni za ndani, ambapo zaidi ya kampuni 200 za Kitanzania zimepata kandarasi za kusambaza bidhaa na huduma zenye thamani inayozidi Shilingi trilioni 1.325,
Mradi huo umewezesha Serikali kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 100 kupitia kodi, ada, ushuru na tozo mbalimbali,”amefafanua.
Hatua nyingine inayosubiriwa katika EACOP ni kuanza kwa safari ya mafuta kutoka Uganda kuelekea Tanzania, ambapo Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa tone la kwanza la mafuta linatarajiwa kuingia Pump Station Number One nchini Uganda Desemba 2026.
Amesema baada ya kusafirishwa kwa takribani miezi miwili, mafuta hayo yanatarajiwa kufika Chongoleani, Tanga, Februari 2027, huku upakiaji wa shehena ya kwanza kwenye meli ukitarajiwa kuanza Machi 2027.
Katika sekta ya gesi, Mkurugenzi huyo amesema TPDC imeendelea na maandalizi ya Mradi wa Uchakataji na Usindikaji wa Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG), huku Serikali ikikamilisha mazungumzo na kampuni za kimataifa kuhusu maeneo ya kibiashara, kikodi na ugawanaji wa mapato.
Mradi huo unatajwa kuwa miongoni mwa uwekezaji mkubwa unaolenga kuongeza nafasi ya Tanzania katika biashara ya gesi asilia kikanda na kimataifa.
“Uendelezaji wa gesi ya Mnazi Bay, Ruvuma-Ntorya na upanuzi wa miundombinu ya gesi nchini umeendelea kuwa sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji na kukidhi mahitaji yanayoongezeka,
Katika Mnazi Bay, visima viwili vipya vya uzalishaji vina uwezo wa kuongeza takribani futi za ujazo milioni 65 za gesi kwa siku, wakati bomba la Ntorya-Madimba lenye thamani ya Shilingi bilioni 122.7 limefikia asilimia 67 ya utekelezaji,”ameeleza.
Pia ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2026/27, TPDC imeweka mkazo katika kuongeza uzalishaji wa gesi, kuendeleza utafutaji wa mafuta na gesi katika vitalu vya kimkakati, kupanua matumizi ya gesi majumbani, viwandani na kwenye usafirishaji, pamoja na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa nishati.
“Mikakati hiyo inakwenda sambamba na miradi ya Kinyerezi-Chalinze, Mini-LNG, CNG na mipango ya kusafirisha gesi na mafuta kwenda nchi jirani,”amesema




