Na Mwandishi Maalumu- Dar es Salaam

Katika hatua muhimu ya kuimarisha mapambano dhidi ya saratani nchini wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wamekutana jijini Dar es Salaam kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha huduma za kinga, uchunguzi, matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa wa saratani.

Kikao hicho kilichoongozwa leo na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa ORCI, Dkt. Mark Mseti ni hatua ya kimkakati itakayochochea mageuzi ya utoaji huduma za saratani kwa kuongeza ufanisi, ubora na upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi.

Akizungumza kuhusu kikao hicho Dkt. Mseti alisema ushirikiano wa karibu kati ya ORCI na MNH ni muhimu katika kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma stahiki kwa wakati huku akibainisha kuwa mikakati iliyowekwa inalenga kuimarisha uratibu wa huduma, kuboresha mifumo ya rufaa na mapokezi ya wagonjwa pamoja na kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchunguzi na matibabu.

“Tunajenga mfumo imara utakaorahisisha huduma kuanzia uchunguzi hadi matibabu na ufuatiliaji huku tukihakikisha wataalamu wetu wanaendelea kujengewa uwezo kupitia mafunzo na kubadilishana uzoefu”, alisema Dkt. Mseti.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Faraja Chiwanga alisema ushirikiano huo unaimarisha zaidi uwezo wa taasisi hizo katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa huku ukichochea matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo.

Dkt. Chiwanga aliongeza kuwa juhudi hizo zinaweka msingi imara wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za saratani zenye viwango vya juu zinazokidhi mahitaji yao na zinazokwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia ya tiba duniani.

Kikao hicho kimejadili changamoto mbalimbali zinazoathiri utoaji wa huduma za saratani na kuweka mikakati ya kuzitatua ili kuhakikisha wagonjwa wanahudumiwa kwa viwango vya juu vya ubora, usalama na kwa wakati. Msisitizo pia umewekwa katika kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.

Katika kuimarisha huduma hizo ORCI inaendelea kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo PET/CT Scan, inayosaidia kubaini kwa usahihi hatua ya ugonjwa kufuatilia maendeleo ya matibabu pamoja na kuboresha uchunguzi wa magonjwa mengine.


Ushirikiano huu kati ya ORCI na MNH unaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha sekta ya afya hususan huduma za saratani kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kisasa, salama na zenye ubora wa hali ya juu.