Kama ni mvutaji wa sigara, basi pia unapaswa kufahamu ni kwa kiasi gani uvutaji wa sigara ulivyo na madhara kwa afya yako. Nimejaribu kufanya utafiti mdogo ikiwa ni pamoja na kuongea na ‘wavutaji mahiri’ na asilimia 90 ya wavutaji,  45 wanakiri kwamba wasingethubutu kujiingiza katika tabia ya uvutaji wa sigara  kama wangekuwa na uwezo wa kurudisha muda wao nyuma.

c unachochea mazingira hatarishi ya magonjwa ya moyo, saratani ya mapafu, kifua kikuu, saratani ya damu na pia kupoteza nguvu za jinsia hususani kwa wanaume. Na cha kuhuzunisha zaidi magonjwa hayo ni rafiki wa karibu wa wavutaji wa sigara na tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya nusu ya wavutaji wa sigara, wanakufa mapema kutokana na kitendo hicho.

Kwa bahati nzuri, madaktari na Serikali hususani kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wana ufahamu wa kutosha kwamba ni vigumu kiasi gani kwa mtu kuacha kuvuta sigara, hasa pale ambapo tayari imeshakuwa tabia.  Na huenda umeshawahi kufikiria kuacha kutokana na kugundua madhara yake ambayo yanaweza kukupata siku za mbele, na ndiyo maana hujawahi kuona ni upi wakati sahihi kwako wa kuacha kuvuta sigara, lakini hata kama uliwahi kujaribu hapo awali, ufanye wakati huu ufanikiwe kuacha kabisa kuvuta sigara.

Bado hujachelewa sana kuchukua uamuzi wa kuacha kuvuta sigara na utapata manufaa makubwa kiafya kutokana na kuacha kuvuta sigara ndani ya mwaka wa kwanza kabisa. Na hata kama utakuwa umeshaathirika na magonjwa yatokanayo na uvutaji wa sigara, kuacha uvutaji wa sigara kutasaidia kuzuia hali ya afya yako kuwa mbaya zaidi.

Hatua za mwanzo

Hongera kwa kusoma makala hii ya jinsi ya kuacha kuvuta sigara. Ni hatua ya mwanzo na tayari umeshaanza kuichukua. Kinachofuata ni kutafuta mtu anayeweza kukusaidia katika kampeni hii binafsi ya kuacha kuvuta sigara, ambaye atakusaidia zaidi kukushauri.

Siku hizi kuna maelfu ya huduma za kusaidia kuacha uvutaji wa sigara. Wahudumu wa afya hususani madaktari na wafamasia wapo mstari wa mbele katika hili; wanatoa tiba na ushauri pia.

Tunaanza kufuatilia hali ya tabia yako ya uvutaji, ndipo tunapojua tiba sahihi itakayokufaa lakini ni baada ya kukufanyia vipimo kujua ni kwa kiasi gani tatizo hili limekuathiri kimwili na kiakili pia.

Uhitaji wa ushauri? Uvutaji wa sigara ni vyema ikatambulika kuwa ni ulevi kama vilivyo vilevi vingine na wakati wote siyo rahisi kuacha kwa kuwa jambo hilo ni la ‘kiakili’ (addiction).

Hivyo, ni vyema kwenda kwenye vituo vya magonjwa ya akili ambavyo sasa vinapatikana katika hospitali nyingi kubwa nchini, zikiwamo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Mwananyamala na kwingineko.

Hapo utakutana na washauri wa magonjwa ya akili na dawa za kulevya ikiwamo hili la uvutaji wa sigara ambao wamepatiwa mafunzo ya kutosha kufuatilia mazingira yako yanayokushawishi uendelee kuvuta sigara na ni kwa namna gani kukufanikisha uweze kuachana nayo. Watakusaidia pia kukupa ushauri wa kisaikolojia namna ya kupambana na matamanio ya kukufanya uanze tena uvutaji wa sigara.

Unahitaji msaada?

Ndiyo. Unahitaji zaidi msaada, familia na marafiki wanaweza kuwa msaada pia lakini watoa huduma za afya watakusaidia kukupatia tiba ya kukusaidia kuacha kabisa uvutaji wa sigara.

Rafiki wa karibu

Kama nilivyotangulia kusema hapo awali, kwamba suala la kuacha  uvutaji wa sigara ni gumu kulichukua kwa sababu ni jambo ambalo lipo kiakili zaidi ‘addiction’. Ni jambo ambalo pamoja na kupatiwa tiba, bado msaada wa kisaikolojia unahitajika kutoka kwa watoa huduma za afya.

Na msaada huu wa kisaikolojia unaohitajika mara kwa mara kwa mwathirika wa sigara, hivyo ni vyema kutengeneza ukaribu wa hali ya juu kati ya mtoa huduma na mwathirika wa uvutaji wa sigara. Habari njema ni kwamba siku hizi watoa huduma za dawa hasa wafamasia ambao kwa kushirikiana na madaktari na wanasaikolojia, wapo tayari kukusaidia kwa namna yoyote wakati wowote, mahali popote.

Pamoja na kuendelea kutumia aina tofauti za dawa tajwa hapo juu ili kuhakikisha unaacha kuvuta sigara, wataendelea pia kukupa huduma tofauti zikiwamo: dawa stahiki ambazo zitahitajika wakati ukiendelea na tiba na kuhakikisha dawa hizo unazipata kwa wakati.

Nyingine ni kukupima mwenendo wa shinikizo lako la damu mara kwa mara, kiasi cha lehemu mwilini (cholesterol), na kiasi cha sukari katika damu, kukupa ushauri jinsi ya kujikinga na matamanio ya kuendelea kuvuta sigara na  kukupa chanjo za mafua na magonjwa mengine yanayoambatana na kukohoa ambayo kwa kawaida ni rahisi kuyapata wakati wa tiba.

Na zaidi ni kuendelea kukupa ushauri tiba ambao ni  rafiki jinsi ya mwenendo mzima wa namna ya kuacha kabisa kuvuta sigara.

By Jamhuri