…Ageuka pia kuwa shujaa barani Afrika

Mapema mwaka huu, Mario Balotelli aliachwa katika timu ya taifa ya Italia (Azzurri) iliyocheza na Marekani Jumamosi, Februari 29, lakini Alhamisi iliyopita ghafla aliichanganya Italia alipoipeleka kucheza mechi ya fainali za Euro 2012 hapo juzi, Jumapili, dhidi ya Hispania mjini hapa.

“Siwataki wachezaji wanaojibu mapigo na kutolewa nje ya uwanja,” alisema kocha wa Azzurri, Cesare Prandelli, wakati akitetea uamuzi wake huo kwa waandishi wa habari wa Italia na kisha akaendelea:

“Huwa ananiudhi. Ninaposema kuwa nataka tufike katika michuano ya Kombe la Ulaya tukiwa tumejiandaa vya kutosha namaanisha siwataki wachezaji wenye matatizo. Sitaki wanaocheza kwa hasira, kutolewa nje ya uwanja na kuacha wenzao 10 wakihangaika”.

Hata hivyo, Prandelli alibadili kauli yake miezi mitatu baadaye alipomwita Balotelli katika kikosi chake kilichoshiriki fainali hizo, safari hii akisema anamwamini.

“Niliposikia anasema kwamba hataiangusha Italia kwa kuiacha na wachezaji 10 uwanjani, nilimwamini kwa asilimia 100,” alisema kocha huyo, ukweli uliothibitishwa kwa vitendo na mshambuliaji huyo Alhamisi iliyopita alipoiwezesha Azzurri kucheza mechi ya fainali hizo za Euro 2012 Jumapili.

Lakini umuhimu wa Balotelli haukuanza katika mechi hiyo ya nusu fainali ambayo mabao yote 2-1 dhidi ya Ujerumani aliyafunga mwenyewe, la kwanza akilipachika kwa kichwa na baadaye akatamba: “Ninataka kushinda na sijali tunacheza na timu gani. Tutacheza kwa nguvu zetu zote dhidi ya Hispania”.

Alianza kutikisa nyavu katika mechi ya mwisho ya hatua za awali alipoifungia Italia moja kati ya mabao 2-0 dhidi Ireland mjini Warsaw, Poland. Antonio Cassano ndiye aliyefunga bao la awali katika kipindi cha kwanza, wakati huo Balotelli aliyeingia uwanjani dakika za mwisho akiwa bado benchi.

Awali, mshambuliaji huyo alikuwa ameteswa na vitendo vya ubaguzi wa rangi dhidi yake, vile ambavyo beki wa zamani wa kimataifa wa Chelsea na England, Sol Campbell, alionya mapema kuwa vingekithiri katika fainali hizo.

Hadi kufikia Juni 16, Balotelli alikuwa amefanyiwa vitendo hivyo mara tatu kwa kupigiwa kelele za nyani. Kwanza alizomewa akiwa mazoezini na timu yake, kisha akaitwa hivyo tena na mashabiki wa Hispania Juni 10, ubaguzi uliorudiwa baada ya siku tano baadaye.

Wakati Croatia ikipambana na Italia katika mechi ya mwisho ya Kundi C na kufungana bao 1-1, mashabiki wa timu hiyo walisikika wakimwita nyani kila anapopata mpira na hatimaye wakamrushia ndizi.

Pamoja na kuonya mapema kuwa angemwua mtu yeyote kama angemwona akimfanyia vitendo hivyo, Balotelli alizungumza vinginevyo kabla hajaanza kuonyesha makali ya kutikisa nyavu za timu pinzani awapo dimbani.

“Maneno yananifuata kila ninakokwenda, lakini ni suala la kawaida katika kipindi cha dakika 50, 60 au 90, hivyo wanaokukosoa wanakusaidia kuboresha kiwango,” alisema siku moja kabla ya mpambano wa robo fainali kati ya Italia na England katika mechi iliyochezwa kwa dakika 120 bila bao lolote.

Akiwa tayari amesema asingejali tena ubaguzi huo aliokuwa akifanyiwa ili kutuliza akili yake na kufanya vyema katika michuano hiyo, Balotelli ndiye aliyefunga mkwaju wa kwanza katika ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya England, baada ya Riccardo Montolivo kuanza kwa kupiga nje kabisa ya lango.

Lakini katika hali iliyokera wasomaji wake wengi, gazeti maarufu la michezo nchini humo, Gazzetta dello Sport lilimdhalilisha baada ya kuchapisha katuni inayomfananisha na nyani, ile ambayo alikuwa amedandia ghorofani, safari hii akibaguliwa kwa mara ya nne.

Mshambuliaji huyo mwenye vituko mbalimbali nje ya uwanja hata hivyo hakujali, badala yake akalijibu gazeti hilo kwa kuifungia Italia mabao yote mawili yaliyoipeleka fainali zilizochezwa juzi na kulazimika limuombe radhi.

Hadi kufikia hatua hiyo, Balotelli alikuwa akiongoza kwa kufunga mabao mengi akiwa ametikisa nyavu mara nne. Alikuwa akifuatiwa na washambuliaji watatu kutoka nchi tofauti waliokuwa na mabao matatu kila mmoja ambao ni Cristiano Ronaldo kutoka Ureno, Mario Gomez wa Ujerumani na Mrusi Alan Dzagoev.

Tayari amegeuka kuwa kipenzi na shujaa wa Italia na mashabiki wa soka Afrika kwa sababu ni Mtaliano mwenye asili ya huko. Alizaliwa Agosti 27, 1990 mjini Palermo, kisiwa cha Sicily nchini Italia na wazazi wake ni raia wa Ghana, Thomas na Rose Barwuah.

Alipelekwa kulelewa na familia ya Wataliano Wazungu – Francesco na Silvia Balotelli – baada ya wazazi wake kushindwa kumlipia fedha za matibabu. Alipata uraia wa nchi hiyo ya Ulaya Magharibi alipofikisha umri wa miaka 18 ili kukidhi matakwa ya kisheria.

Akiwa mchezaji wa timu ya Manchester City ya England alikohamia akitokea AC Milan ya Italia, Balotelli analipwa mshahara wa pauni 125,000 kwa wiki, na pia anapata fedha nyingi kutokana na mikataba yake ya kibiashara na kampuni tofauti.

Mbali na mshahara huo na matangazo hayo ya biashara, Balotelli pia anaingiza fedha nyingi kupitia mapato yake mwenyewe kutoka timu ya Manchester City kwa sababu inaitumia sura yake akiwa mchezaji wake kujipatia fedha.

Utajiri wake uliomfanya awe bilionea huku akiwa na umri wa miaka 21 tu, umemfanya amiliki jumba la kifahari lenye thamani ya pauni milioni tatu, lakini mwaka jana alidaiwa kulichoma moto kutokana na tabia za kitoto. Wakati likifanyiwa ukarabati uliomlazimu kwenda kuishi hotelini kwa wiki nane alipoteza kiasi cha pauni 55,000.

Kana kwamba hiyo haitoshi, utajiri wake pia unathibitishwa na gari lake la aina ya Bentley Continental GT lenye thamani ya pauni 140,000. Tayari ameshalilipia zaidi ya pauni 10,000 kama gharama za maegesho katika maeneo maalumu.

Amewahi pia kufanya kituko cha aina yake mwaka huu alipokuwa barabarani akiendesha gari lake hilo. Baada ya kusimamishwa na polisi na kuchungulia ndani alikutwa na bunda la pauni 15,000 za noti ambazo alipoulizwa kwa nini anatembea na kiasi kikubwa hivyo cha fedha alijibu: “Ni kwa sababu mimi ni tajiri”.

Huyo ndiye Mario Balotelli, mshambuliaji mwenye vituko lukuki kuanzia uwanjani hadi nje ya dimba, yule ambaye baada ya kupuuzwa na kocha wa Azzurri, Prandelli, mapema mwaka huu, ghafla aliichanganya Italia na kuchukuliwa kuwa shujaa katika bara zima la Afrika kwenye asilia yake.

 

1173 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!