Misitu ina nafasi kubwa ya kukuza uchumi wa Watanzania ikiwa itatumiwa vizuri, amesema Balozi wa Finland hapa nchini, Sinikka Antila.

Antila ametoa changamoto hiyo katika mazungumzo maalumu na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi (pichani), alipomtembelea ofisini kwake Dar es Salaam, wiki iliyopita.


“Finland imetajirika kutokana na rasilimali za misitu, lakini tumejiimarishia teknolojia inayotusaidia kuwekeza kwenye misitu,” amedokeza Balozi huyo.


Akizungumzia wananchi wa mkoani Mtwara, Antila ameshauri nguvu zielekezwe pia katika uwekezaji kwenye misitu iliyopo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wengi.

Hata hivyo, amesema Watanzania wana haki ya kunufaika na rasilimali za nchi ikiwamo gesi ghafi inayopatikana mkoani Mtwara.


Katika hatua nyingine, Balozi huyo wa Finland ameeleza kuridhishwa na uhuru wa vyombo vya habari Tanzania ikilinganishwa na nchi nyingi za Afrika.


Dk. Mengi kwa upande wake ameunga mkono dhana ya wananchi kudai haki ya kunufaika na rasilimali za nchi, ingawa ameeleza kutofurahishwa na watu wanaotumia mwanya huo kutafuta umaarufu na maslahi binafsi.


Aidha, mtazamo wa Mwenyekiti huyo wa IPP kuhusu uhuru wa vyombo vya habari nchini, ni kwamba bado haujakidhi mahitaji ya misingi, maadili na utendaji wa tasnia hiyo.


3444 Total Views 20 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!