Na Angela Kiwia
Balozi John Chagama amesema Tanzania inapoteza mabilioni ya shilingi
kutokana na viongozi wachache wenye uchu wa utajiri kuatamia fursa ya soko la
mtandaoni.
Mwaka 2012, Balozi Chagama na wenzake, walianzisha Kampuni ya Tanzania
Commodity Exchange (TCX) iliyopaswa kufanya kazi ya ya biashara kupitia soko
la mtandaoni, lakini kampuni hiyo inahujumiwa.
“Mwaka 2012 tulianzisha TCX, Rais pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara
waliniomba nisaidie kuwasilisha paper kwenye mkutano wa World Economic
Forum uliofanyika Mei, 2013 Cape Town, Afrika Kusini,” amesema Balozi
Chagama.
Rais Jakaya Kikwete aliwatuma watu wake wa Idara ya Uchumi kwenda
kuzungumza na Balozi Chagama baada ya kusikia kuwa ana mpango wa
kuandaa nyaraka (andiko) la masuala ya uchumi akamtaka kusaidia kuliwasilisha
kwa niaba ya Tanzania.
Amesema, baada ya kuombwa na Rais Kikwete, aliwasiliana na watu
waliomsaidia kuandaa mpangokazi (nyaraka) ambao ulikubaliwa na jopo la
wataalamu wa masuala ya uchumi duniani.
“Hii kazi niliifanya mwenyewe kwa kutafuta wataalamu wanne nje ya nchi ambao
waliandaa mpangokazi wa kuiwezesha Tanzania kupata soko la kielektroniki.
Wataalamu hao walikuwa ni Prof. Julius Nyang’oro (North Caroline), huyu ndiye
aliyekuwa team leader, Dk. Bharat Kullkarr (India/Nepal), Prof. Yohannes
(Caroline), Chief Mashudu Tshuantse (South Africa), Sisay Shimelis (Ethiopia) na
Dkt. Marcus (America).”
“Hawa niliwalipa kwa kazi ambayo waliifanya. Binafsi nilimweleza Rais Kikwete
kuwa hii kazi ni ngumu na hatari kwani inapigwa vita na wafanyabiashara
(makampuni) wanaonunua mazao nchini. Alinielewa, lakini nguvu kubwa nilifanya
mimi binafsi,” amesema Balozi Chagama.
Aliandaa nyaraka kwa miezi minne na alitumia kiasi cha zaidi ya dola za Marekani
200,000 (Sh milioni 500) kufanikisha kazi hiyo aliyokabidhiwa na Rais Kikwete.
Baada ya kuwasilisha mpangokazi katika mkutano huko Afrika Kusini, waliulizwa
ni kwa nini wanataka Tanzania ipewe kibali cha kufanya biashara kwa njia ya
mtandao; “Tulieleza na tukatetea andiko letu, wakakubali siku hiyo hiyo na kibali
kilitolewa siku hiyo hiyo.”
JAMHURI limefanya mahojiano maalumu na Balozi Chagama kama ifuatavyo:

JAMHURI: Unasema kibali kilitolewa siku hiyo, je, alikabidhiwa nani kibali hicho?
Balozi Chagama: Kibali alikabidhiwa Waziri wa Kilimo maana suala hili lipo chini
ya Wizara ya Kilimo pia. Ingawa katika mkutano ule tulikuwa na Katibu Mkuu
Wizara ya Kilimo, Naibu Katibu Mkuu Kilimo, watendaji kutoka Benki Kuu (BOT)
pamoja na baadhi ya maafisa wa Serikali.
JAMHURI: Baada ya hapo mlifanya nini?
Balozi Chagama: Ndiyo tukaanzisha Tanzania Commodity Exchange ambayo
tuliisajili kwa Msajili wa Makampuni (BRELA) mwaka 2012. Tuliweka wanahisa
watatu, kwa hisa tatu ambapo kila mmoja wetu alikuwa na hisa moja tu.
JAMHURI: Kwanini hisa tatu tu siyo zaidi, wakati nyie ndiyo wenye kampuni na
waanzilishi?
Balozi Chagama: Kwa sababu tulitaka kampuni hii iweze kumilikiwa na
Watanzania wengi. Maana tuliamini ya kuwa hisa hizo zingeuzwa kwa mwenye
uhitaji kisha kuongeza umiliki wa watu wengine.
Tulianzisha hiki kitu ili kiweze kuisaidia nchi kuuza bidhaa zake nje ya nchi na
kupata faida siyo kama ilivyo sasa. Unapouza bidhaa yoyote kupitia soko la
mtandao, nchi inapata faida ikiwa ni pamoja na mwenye bidhaa husika anauza
kwa bei nzuri ya soko bila kunyonywa na walanguzi.
JAMHURI: Umesema mlianzisha kampuni yenu miaka sita iliyopita. Mmefanya
nini kwa miaka yote hiyo?
Balozi Chagama: Wizara ya Kilimo ilituomba kufanya mafunzo kwa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Kilimo ili iweze kupata ufahamu wa biashara hii, tulifanya
hivyo na baada ya mafunzo mwaka 2013, wanakamati walikwenda Ethiopia
kujifunza na kuona tulichowafundisha.
Kule Ethiopia, walikuta kitu kinaitwa ECX wakabaini kile tulichowafundisha kina
faida kwa nchi ile. Waliporudi tulikutana na walitutaka kuleta andiko ili tuweze
kuanza kazi mapema.
Tuliwaeleza kuwa andiko lipo tayari na lilishapelekwa wizarani, ambapo wizara
iliunda kamati iliyokuwa na wajumbe kutoka wizara ya kilimo na wizara ya
viwanda na biashara.
JAMHURI: Kama mlifikia hatua hiyo, kwa nini useme kwamba Serikali
imewadhulumu?
Balozi Chagama: Nasema hivyo kwa sababu baada ya kuundwa kamati yenye
wajumbe kutoka wizara hizo mbili, waliandika ripoti ambayo ilipelekwa kwenye
Baraza la Mawaziri baada ya hapo BoT kupitia Wizara ya Fedha waliwasilisha
mapendekezo ya sheria bungeni ikaundwa sheria mwaka 2015 Sheria Na 5 ya
Masoko ya Mitaji na Dhamana ya Mwaka 1994.
Mwezi Julai 2015 sheria ilipitishwa baada ya Rais kuisaini na Januari 2016, kanuni

zilitoka. Lakini katika hali ya kushangaza Serikali ikaunda kampuni ya TMX bila
kutushirikisha kufanya kazi ambayo tunatakiwa kuifanya sisi TCX.
Kitu ambacho kinatakiwa kifanyike ni mazao yote nchini yanayouzwa ikiwamo
madini yanatakiwa yauzwe kupitia commodity exchange. Wafanyabiashara kutoka
nje ya nchi ikiwa ni pamoja na Wahindi wanaonunua mazao hawatowaibia tena
wakulima.
Vitu vyote vinatakiwa kuuzwa kupitia kwenye commodity exchange, na kama
Serikali ingetumia mfumo huu nchi ingeingiza fedha zake ikiwa ni pamoja na
wakulima.
Huwezi kuamini; pamoja na kutumia kiasi kikubwa cha fedha ambazo niliamini
zingeweza kurudi baada ya kuanza biashara, tulijikuta tunasikia kuna kitu kingine
kimeanzishwa na kinaitwa TMX.
Hii TMX ilianzishwa na Serikali baada ya sisi kufanya kazi kubwa na
hatukushirikishwa katika uanzishwaji wake wakati nyaraka zote za usajili wa
biashara hii tulihangaika kuziandaa sisi. Hii ni dhuluma ya wazi wazi.
Pamoja na kuanzishwa kwa kampuni hiyo, Serikali imeshindwa kufanya biashara
mpaka hivi tunavyoongea. Wakati sisi pesa tunazo na tuko tayari kufanya
biashara tumefanyiwa mizengwe ya makusudi.
JAMHURI: Unasema mna pesa za kufanya biashara! mmezitoa wapi wakati
umesema kwamba pesa za kugharamia andiko ulikopa?
Balozi Chagama: Ni kweli tuna pesa za kuanzisha biashara, lakini hatuna
mwongozo wa kufanyia kazi kwani tumetengwa na Serikali. Pesa tulizonazo
zinatokana na wadau ambao wako tayari kufanya kazi na sisi, hivyo Serikali
ikituruhusu tuko tayari.
Tulikuwa tumemwalika mwekezaji wa kimkakati ambaye alikuwa tayari kutoa
pesa, lakini alipoona kuwa hatueleweki alienda kuwekeza Rwanda ambapo
kumeanzishwa East Africa Commodity Exchange (EACX) ambayo inaendelea hivi
sasa.
Nchi ya Msumbiji walikuja kuomba kupitishia kwenye platform yetu nchini, lakini
imeshindikana kufanyika. Tumekosa soko la Msumbiji (korosho) kuuzwa kupitia
nchini kwetu maana walielekezwa na Benki ya Dunia kuuza kupitia kwetu.
JAMHURI: Iwapo Serikali itataka mfanye kazi na TMX, je, mpo tayari?
Balozi Chagama: Tuko tayari hata sasa hivi kufanya biashara nao maana sisi
pesa tunazo. Sisi tuko na timu ya wataalamu wa kujenga maghala yenye viwango
vya kimataifa yanayohitajika ambayo hayapo nchini, wataalamu wa kimataifa wa
viwango vya bidhaa (ubora) pamoja na timu ya masuala ya uchumi. Iwapo
tukiambiwa tupo tayari kuanza kazi kwani Tanzania ina mazao mengi ambayo
yanatakiwa kuuzwa kimataifa na kuubadilisha uchumi wa nchi kwa kuongeza soko
haraka. Muda umefika kwa Serikali kukuza uchumi wa nchi kupitia mazao. Kupitia

soko la mazao mtandaoni hatuna haja ya wafanyabiashara kuingia nchini
kununua mazao kwa wakulima kwa bei ya kutupa.
JAMHURI limefanya mahojiano na Afisa Habari wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji
na Dhamana (CMSA), Charles Shirima, kuhusiana na suala hilo ambaye alikiri
kuwa wakati TMX inaanzishwa kuna watu walikuwa wameanzisha kampuni
nyingine ya TXC.
Amesema hana uhakika kampuni hiyo iliishia wapi, bali wao wakati wanaanzisha
TMX walishirikisha sekta binafsi (TPSF) kutafuta namna ya kuwekeza katika
bidhaa nchini.
JAMHURI: Serikali inamiliki hisa ngapi katika kampuni ya TMX?
Shirima: Hisa 52 na zilizobaki ziko kwa watu binafsi.
JAMHURI: Mpaka sasa mmewekeza kiasi gani, na mmeshaanza kufanya kazi na
kama bado kwanini?
Shirima: Mpaka tunavyoongea hapa Serikali imewekeza zaidi ya Sh Bilioni 3.5,
lakini sekta binafsi haijawekeza chochote kile. Hatujaanza kufanya biashara
kutokana na ukata, lakini tunataraji tunaweza kuanza hivi karibuni baada ya
mambo kuwa sawa na tutakapoanza tutaanza na ufuta mwezi huu. TMX bado
hawajatoa pesa yoyote ile kila tukiwaeleza suala la pesa tunaona wanasitasita tu.
JAMHURI: Kama mnaona wanasitasita kwanini msifanye kazi na TCX ambao
wanasema wapo tayari na pesa wanayo?
Shirima: Tumeipa leseni TMX hiyo nyingine hatuitambui. TMX imeanzishwa
kutokana na uamuzi wa Security Committee ambayo wajumbe wake ni Katibu
Mkuu Ofisi ya Rais, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Katibu Mkuu
Kilimo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Msajili Bodi ya Maghala, na wajumbe
wengine wengi kutoka serikalini. Iliamuliwa ipitie TPSF ili kuondoa umiliki binafsi.
JAMHURI: Mtaji kiasi gani unahitajika kuanzisha soko hili la mtandao, ni kiasi
gani?
Balozi Chagama: Ni mpaka Serikali ikuamulie ni mazao yapi utayanunua ndiyo
utajua unahitaji kuwa na fedha kiasi gani, kwani inatokana na ukubwa wa biashara
unayotakiwa kufanya wakati huo.
JAMHURI: Kwa kuanzia yanahitajika maghala mangapi na yatajengwa wapi?
Balozi Chagama: Yanahitajika maghala 12 ambayo yatakuwa ni maghala ya
kununulia na kuuzia mazao. Maghala haya yatakuwa ya aina mbili ambapo ya
kununulia mazao yatajengwa kwenye maeneo ya kuzalishia nafaka na maghala
ya kuuzia yatajengwa kwenye mipaka ya nchi.
JAMHURI: Mazao yapi wanaweza kuanza nayo katika hili soko mtandao?
Balozi Chagama: Yapo mazao aina tano tu ambayo ni mahindi, mchele, mbaazi,
kahawa, korosho pia na bidhaa zote za madini. Mazao hayo matano yanajulikana

kama mazao ya wakulima ambayo yatauzwa kwa bei ya soko la dunia.
JAMHURI: Kwa sasa mkulima anapata Shilingi ngapi na wakiingia katika soko
mtandao atapata Shilingi ngapi?
Balozi Chagama: Bei ya soko la dunia kwa zao la korosho inafikia dola za
Marekani 30-35 kwa kilo moja, lakini hapa wanauza chini ya dola za 5 (Sh 12,500)
Marekani.
Wakulima wanapata hasara ya dola 25-30 (kati ya Sh 60,000 na Sh 70,000) kwa
kila kilo moja ya korosho, jambo ambalo ni hatari kwa uchumi wa nchi na mtu
mmoja mmoja. Iwapo mkulima atauza mazao yake kupitia soko mtandao ana
faida kwani atakuwa ameuza kwa bei ya soko hivyo itamsaidia kujinunulia
viuatilifu na kuzalisha zaidi ikiwa ni pamoja na kuboresha maisha yake binafsi.
Kuuzwa mazao kwa bei ya chini kunamfaidisha mlanguzi (mtu wa kati) ambaye
anapata faida kubwa huku akimnyonya mkulima.
JAMHURI: Rwanda wananunua maharage kutoka Mkoa wa Kigoma na kuuza
kupitia soko hili, hivi suala hili likoje?
Balozi Chagama: Ni kweli nchi ya Rwanda inanunua mazao kutoka Mkoa wa
Kigoma kwa bei rahisi, wanasafirisha kwa meli kisha wanaingiza kwenye soko la
kimataifa. Mazao hayo yakifika Rwanda yanasafirishwa kwa kutumia ndege za
mizigo mpaka kwenye soko la dunia. Nchi hii inapata faida kutokana na mazao
yetu yaliyotakiwa kuuzwa hapa hapa nchini. Pia chai ya Mufindi nayo imekuwa
ikisafirishwa na kuuziwa Mombasa nchini Kenya. Nchi yetu inapoteza mapato
kutokana na kuzembea kufanya biashara hii.
JAMHURI: Serikali itarajie kupata kodi kiasi gani soko hili likianzishwa?
Balozi Chagama: Serikali itapata faida kubwa kutokana na manufaa ya soko kwa
sababu kodi yote itakusanywa kupitia mtandao kwenda kwenye akaunti ya
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mkulima pesa zake zitaenda moja kwa moja benki kupitia akaunti yake. Pesa
zake zitakuwa salama na za uhakika, pia atalipwa kwa wakati huku Serikali
ikiepuka udanganyifu. Mkulima atakapouza mazao atapatiwa risiti (risiti ghalani)
ambayo itamsaidia katika malipo yake.
JAMHURI: Je, miundombinu ya kufikia soko hili ikiwamo barabara, magari, treni
za kusafirisha na internet ipo hapa nchini?
Balozi Chagama: Miundombinu ipo kwani barabara zipo, mtandao upo
kilichokosekana ni ujenzi wa maghala yenye viwango vya kimataifa kuboresha
mazao na kuepuka udanganyifu. Utakumbuka korosho iliyopelekwa sokoni
ikakutwa na michanga, mawe pamoja na pamba ambayo ilikutwa imewekwa maji
ni doa kwa nchi kibiashara.
Maghala yenye viwango yatakuwa na quality control ambayo yataangalia na
kutunza mazao yenye viwango vinavyokubaliwa kimataifa na kulinda soko. Hili ni

jambo muhimu kwa biashara hii na nchi kwa ujumla katika uchumi wa nchi na mtu
mmoja mmoja.
Soko la mtandao linahitaji uaminifu na kujituma (weledi). Nchi ya India inafanya
biashara hii na kuingiza dola za Marekani milioni 600 kwa siku moja tu kutokana
na kuuza mazao.
JAMHURI: Je, kuna watu wenye uwezo wa kuliendesha soko hili? Kwa maana ya
wafanyakazi?
Balozi Chagama: Sisi tulishasaini makubaliano (MoU) na Taasisi ya Kilimo nchini
ili ilete vyama vyote vya ushirika kuwa wanahisa wa kampuni. Hawa ndiyo
tulikuwa tunakuja kufanya nao kazi kwani tulishatoa mafunzo kwa taasisi hii.
Tuliwataka kukutana na vyama vya ushirika kisha tuweze kufanya kazi pamoja
ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wakulima kwa kuwapatia mbegu zinazohitajika.
Nchi ya Tanzania kwa sababu ina kila kitu, ilitakiwa kuwa kiungo cha biashara ya
mtandao katika nchi za Afrika Mashariki.
Katika nchi hizi hakuna nchi yenye bidhaa nyingi kama Tanzania. Tanzania ndiyo
inatakiwa kuwa na soko kubwa la kimtandao katika Jumuiya na kuileta dunia
Tanzania kimasoko.
Kama Rwanda wanachukua mazao ya Tanzania na kuyauzia huko kwao, kwanini
mzao haya yasiuziwe hapa hapa nchini na nchi ikaingiza fedha hizo?
Stakabadhi ghalani ni mfumo unaotakiwa kufanya kazi sambamba na soko
mtandao ukisaidiwa na hati ghalani. Kama mazao yote yakiwekwa ghalani
mkulima anapatiwa risiti yake itakayomsaidia kwenye malipo.
Mfano, kuna kitu mmekuwa mkikisikia kinaitwa unyaufu. Huu unyaufu wa mazao
ghalani ni udanganyifu unaofanywa na wafanyabiashara na kuwanyonya
wakulima. Hakuna mazao yanayoweza kupungua uzito baada ya kupokewa na
kutunzwa ghalani.
Kwa mwaka tunapoteza fedha nyingi kutokana na kutokuwa na kipaumbele katika
soko hili. Hizi ripoti ambazo zimekuwa zikitolewa na Benki ya Dunia kuhusu pesa
tunazopoteza ingekuwa historia.

1602 Total Views 2 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!