Tanzania ni nchi yenye bahati. Bahati yake inafahamika si kwa nchi yetu tu bali hata kwa wakoloni waliopata kututawala. Tanzania imetokana na Muungano wa nchi za Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Katika mkutano wa Berlin, wa mwaka 1884/85, Wajerumani waliokuwa wenyeji wa mkutano huo, waliichagua Tanganyika kama koloni lao.

Ujerumani haikuichagua Tanganyika kimakosa. Uchaguzi huu haukuwa kwa bahati mbaya. Walijua maliasili zinazomilikiwa na taifa hili. Moja ya maliasili hizo ukiacha madini, gesi na mengineyo ni Bandari. Tanzania imezungukwa na nchi nane; Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Zambia, Malawi na Msumbiji.

Nchi hizo, hata ukichanganya na Zimbabwe, zinaweza kuwa wateja wetu wa Bandari. Yapo maeneo ya Kenya yanayoweza kuhudumiwa vyema na Bandari ya Tanga kuliko Bandari ya Mombasa. Msumbiji pia, baadhi ya maeneo ya Kaskazini mwa nchi hiyo yanaweza kuhudumiwa vyema na Bandari ya Mtwara, kuliko Beira ya kwao.

Bandari hii ni mgodi wa kudumu. Ina uwezo wa kutoa huduma ya kusafirisha mizigo ndani na nje ya nchi kwa miaka nenda rudi. Yapo mambo inatupasa kuisadia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kama nchi iweze kufanya kazi kwa ufansi. Kati ya mambo hayo ni pamoja na miundombinu. Bandari haiwezi kutegemea malori tukazihudumia nchi hizi zilizotuzunguka.

Mwaka 1906 Mkoloni alijenga Reli ya Kati. Leo tunafurahi kuwa Reli ya Kati imetengewa fungu. Ni kwa bahati mbaya kuwa mipango ipo mingi katika nchi hii, ila utekelezaji ni sifuri. Hatutarajii hata Serikali ya Rais Dk. John Pombe Magufuili kuwa itatumbukia katika mtego huo. Kwamba imetuahidi katika Bajeti ya mwaka huu kuwa inajenga reli hii, mwakani inakuja na sababu.

Ukiacha reli, tunasema lazima Serikali ikiwa kweli imedhamiria kuingia kwenye viwanda ifute mpango wa sarafu ya Tanzania kutegemea dola ya Marekani. Wapo wafanyabiashara Zambia hawafahamu kontena gharama ya kulitoa bandarini ni shilingi ngapi kwani viwango vinabadilika kadri dola inavyocheza. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ianzishe kitu kinachoitwa controlled exchange rate.

Serikali itamke kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 au mwaka unaofuata dola itabadilishwa kwa Sh 1,500. Tusiache uchumi wetu mikononi mwa walanguzi, kisha tukalalamika kuwa wateja wanapotea Bandari. Wenye Bureau de Change wanachezea shilingi yetu, tuseme sasa hapana.

Ukiacha hayo matatizo ya nje, watendaji bandarini nao sasa waamke. Wajue kuwa wanalo jukumu la kujenga uchumi wa nchi yetu. Tabia ya watendaji na viongozi wa Bandari kuwaza rushwa na kupata wao binafsi ikome. Lengo na shabaha iwe ni kuongeza ufanisi wa Bandari na hatimaye kuongeza mapato kwa taifa letu. Tukishirikiana na tukaiwezesha Bandari, nchi yetu itajenga uchumi imara.

By Jamhuri