*Mkurugenzi wa Ulinzi asimamishwa kazi kimyakimya
*Timu aliyounda Rais Magufuli yaendelea na upekuzi
*Wasiwasi watanda kwa watumishi, wafanyabiashara
*Mjumbe wa Bodi ataka NASACO irejeshewe udhibiti
Na Waandishi Wetu

Kuna kila dalili kuwa hali ya hewa imechafuka tena katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), baada ya Rais John Magufuli kuvamia na kubaini magari 52 yaliyotelekezwa bandarini hapo tangu mwaka 2015.
Wakati Rais Magufuli akisema magari hayo hayana mwenyewe ingawa yanayonyesha kuagizwa kwa jina la Ikulu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa naye amevamia Bandari na kubaini uwapo wa matrela 44 yaliyotaka kutolewa bandarini kwa jina lake.
Hayo yakiendelea, baadhi ya vyanzo vya habari vimeliambia JAMHURI kuwa hali ya hewa imechafuka Bandari, ambapo wameanza kutimuana kazi. Aliyekuwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Naibu Mkurugenzi Mkuu, Lazaro Twange ameondolewa. JAMHURI limemtafuta Twange bila mafanikio.
Novemba 26, mwaka huu, Rais Magufuli ametembelea meli ya Jeshi la China iliyokuwa inatoa huduma ya matibabu bandarini, lakini akachepuka hadi eneo la kuhifadhi magari alipoibua ‘madudu’ mengine bandarini hapo kwa kukuta magari 52 yaliyoingizwa nchini na watu wasiojulikana, kwa kutumia jina la Ofisi ya Rais.
Rais Magufuli amesema magari hayo siri yake ni kubwa kwani yamekaa tangu Juni, 2015 na yaliletwa pamoja na magari mengine ya serikali. Ameiagiza Takukuru kutoa taarifa kamili ndani ya siku saba kuhusu magari hayo. Siku saba zimeisha jana.
“Inakuwaje Rais nipate taarifa za magari kufichwa, lakini Waziri, TRA, TPA msijue? Mnatakiwa muwe na informers (watoa taarifa) wenu sio hadi mimi nije ndo mnaaza kusema sijui,” amesema.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango wote walitolewa jasho mbele ya Rais Magufuli kwa kuhojiwa iwapo wanataarifa za magari hayo wakasema hawana.
Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro alijaribu kueleza kuwa anafahamu historia ya magari ya polisi, lakini Rais Magufuli akamhoji iwapo anafahamu hayo magari ya Ikulu yalifikaje, na baada ya hapo akamtaadharisha asijiingize kwenye matatizo kwa kutetea asiyoyafahamu.
Rais ametoa siku saba kwa TRA, TPA, Takukuru na Wizara ya Fedha kuhakikisha inatoa taarifa ni nani alihusika kuagiza magari 52 kupitia mgongo wa Ofisi ya Rais.
Imekuwa kawaida sasa kwa Rais Magufuli na Waziri Mkuu kuvamia Bandari ya Dar es Salaam na kubaini kinachoitwa madudu ikiwamo upotevu wa makontena na mizigo mingine, hali iliyomfanya mmoja wa Wafanyakazi kusema hivi: “Kwa umuhimu wanaotoa viongozi wetu kwa Bandari, nadhani bora iundwe Wizara ya Bandari iwe na watendaji wanaoisimamia kila kukicha.”
Pia Rais Magufuli amekagua magari ya polisi yaliyoingizwa nchini mwaka 2015, lakini yakaendelea kubaki bandarini yakiwa yameegeshwa mita 700 kutoka yalipoegeshwa magari ya kubebea wagonjwa yaliyoagizwa na Ikulu.
Amemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kuhakikisha anayakagua magari hayo na kuyatoa bandarini yakafanye kazi iliyokusudiwa.
Novemba 29, mwaka huu, Majaliwa amefanya ziara ya kushtukiza bandarini, akamuagiza IGP Sirro kumkamata wakala wa kampuni ya Wallmark anayefahamika kwa jina la Samwel na mfanyabiashara anayefahamika kwa jina la Bahman kutoka kampuni ya NAS.
Wawili hao wakatuhumiwa kwa kosa la kutaka kutoa bandarini magari makubwa 44 `semi trailers’ bila kulipa kodi, kwa kutumia jina la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Mjumbe wa Bodi ya TPA, Renatus Mkinga ameliambia JAMHURI kuwa wakati umefika sasa ambapo Tanzania inapaswa kurejesha mdhibiti wa huduma za bandari na meli kama ilivyokuwa enzi za NASACO.
“Kwa sasa unakuta Ikulu hakuna wataalam wa masuala ya Bandari, hakuna mdhibiti wa masuala ya meli na hii yote inaifanya nchi kujikuta katika sintofahamu,” amesema Mkinga.
Amesema Bandari haiwezi kuendeshwa kwa utaratibu wa Rais au Waziri Mkuu kuvamia kugundua magari yaliyotaka kutolewa bila kulipa kodi badala yake iwapo mamkala ya usimamizi wa huduma za bandari na meli nchini itakayoamka asubuhi hadi jioni ikiratibu shughuli za bandari siku hadi siku.
“Lakini ikumbukwe tumedhibiti wafanyabiashara wengi hapa. Wengine wanapenyeza mkono na kupeleka taarifa za uongo kwa Mheshimiwa Rais. Unakuta wao hao hao ndiyo mawakala, wao hao hao ndiyo wasafirishaji, ndiyo wenye meli, hii ni hatari. Lazima awepo mdhibiti bila hivyo hatufiki popote,” amesema.
Mtoa taarifa mwingine amesema kinachoendelea sasa bandarini ni “kuchomana”. Ameliambia JAMHURI kuwa hayo matrela yalilipa kodi zote na kusajiliwa kihalali, isipokuwa kwa kuwa yalikaa muda mrefu bandarini walifika kuomba kupunguziwa gharama za kutunza mzigo bandarini (waver), ila wafanyabiashara wakachomana.
“Bandari sasa ilikuwa imeanza kusimama. [Injinia Deusdedith] Kakoko alipoingia alikuta ina mapato ya Sh bilioni 250 kwa mwaka. Sasa mapato yamenda na kufikia bilioni 900 na tunaitafuta trilioni,” ni vyema kwa kuwa ameishajifunza ameanza kuifahamu bandari angepewa muda.
“Kisulisuli ninachokiona na hii ahadi ya kuleta Naibu Mtendaji Mkuu, inaweza kuzalisha balaa. Anaweza kuondolewa Kakoko akaja mtu mwingine ambaye ni mgeni kabisa katika masuala ya bandari ikamchukua muda kujifunza, tutacheza sana shere,” amesema.
JAMHURI limemtafuta Kakoko, ambaye amesema: “Kwa sasa uchunguzi unaendelea na kuna kila chombo unachokijua hapa bandarini, hivyo kwa sasa sina la kuzungumza. Nitafute baada ya ripoti kutolewa wiki ijayo.”
Matukio na vitendo vya kuhujumu uchumi na ukwepaji kodi kwenye Bandari ya Dar es Salaam vimeripotiwa kutokana na ziara zinazofanywa na viongozi wakuu, Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Kumbukumbu ya matukio hayo inaanzia Novemba 27, 2015, Majaliwa, alipofanya ziara ya kushtukiza na kubaini upotevu wa makontena 349 na kuagiza waliohusika na kadhia hiyo kukamatwa kuisaidia polisi.

Majaliwa aliwafukuza kazi maafisa watano na kuwahamisha kituo wengine watatu huku hasara iliyosababishwa ikitajwa kuwa ni Sh bilioni 80.

Rais John Magufuli, alitangaza kumsimamisha kazi aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Rished Bade na kumteua Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango (wakati huo), Dk Philip Mpango kushika wadhifa huo.
Dk. Mpango aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge na baadaye Waziri wa Fedha na Mipango.
Ukiacha Bade, wengine waliosimamishwa kazi ni pamoja na Kamishna wa Forodha na Ushuru, Tiagi Masamaki na Habibu Mpozya wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, wakituhumiwa ubadhilifu wa fedha na upotevu wa makontena hayo.

Wengine waliosimamishwa ni Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari na Eliachi Mrema wakati waliohamishwa kituo na kupelekwa mikoani walikuwa ni Nsajigwa Mwandege, Robert Nyoni na Anangisye Mtafya.

KUVUNJWA BODI TPA

Desemba 7, 2015, Rais Magufuli alivunja Bodi ya Mamlaka ya Bandari (TPA) na kutengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka, Mwenyekiti wa Bodi ya Bandari Profesa Joseph Msambichaka na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Awadhi Massawe.
Kuvunjwa kwa Bodi hiyo kunatokana na utendaji mbovu wa Mamlaka kwa muda mrefu na kitendo cha kutokuchukua hatua katika vyanzo husika.
Waziri Mkuu Majaliwa akasema kutenguliwa kwa uteuzi huo kunatokana na ziara alizofanya bandarini na kubaini mianya ya ukwepaji kodi ikiwemo ya makontena 2,387 yaliyopitishwa kati ya Machi na Septemba, 2014.

WAKALA WA VIPIMO

Februari 9, mwaka 2016 Gazeti la JAMHURI lilichapisha habari iliyoambatana na mchoro jinsi wizi wa mafuta unavyofanyika bandarini. Wizi huo umetokana na kutokuwapo kwa flow meters za kupima kiwango cha mafuta yanayoingia nchini.
Februari 11, mwaka jana, Waziri Mkuu Majaliwa alitaka maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo na Mizani, Magdalena Chuwa kutokana na flow meter za bandarini kutofanyakazi.
Serikali iliwasimamisha kazi watendaji wawili kutoka Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta bandarini kutokana na zuio la matumizi mita hizo kwa zaidi ya miaka mitano.
Waliosimamishwa ni Mtendaji Mkuu wa WMA, Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bernadina Mwijarubi.
Waziri Mkuu pia aliagiza mfumo wa uingizaji mafuta nchini kwa kutumia flow meters urejeshwe na kutumika na ule upimaji wa kukadiria uache kutumiwa mara moja. Hata hivyo, hadi sasa mafuta yanayoingia nchini kwa kupimwa na mita ni dizeli na mafuta mengine yote bado Bandari wanatumia kijiti kuingiza mafuta hayo.
Rais Magufuli hakuficha hisia zake na akaamua kulipongeza hadharani Gazeti la JAMHURI kwa kufanya habari za uchunguzi uliotukuka kuiwezesha nchi kuokoa mapato yanayopotea kwa njia za wizi, rushwa na udanganyifu. Rais Magufuli alilitaja JAMHURI kuwa gazeti bora la kuigwa.

Marekebisho mkataba wa TICTS
Septemba 26, mwaka jana, Rais Magufuli aliagiza mkataba wa Kampuni ya TICTS inayopakia na kuondosha mizigo bandarini ufanyiwe marekebisho kulinufaisha taifa.
Rais Magufuli aliiagiza TPA kununua mashine nne za kukagulia mizigo inayoingia bandarini hapo. Miezi saba baada ya majadiliano TICTS walikubali kulipa kodi ya dola milioni 14 (Sh bilioni 30) kutoka dola milioni 7 (Sh bilioni 15) kwa mwaka na kodi ya makasha dola milioni 20 (Sh bilioni 44) kwa mwaka kutoka dola milioni 13 (Sh bilioni 28).
Machi 23, mwaka huu Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam, akifuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa nyakati tofauti juu ya kudhibiti udanganyifu wa mizigo inayoingia na kutoka nchini kupitia bandari hiyo.
Rais Magufuli alikuta makontena 20 ya mchanga wenye madini kutoka kwenye migodi iliyopo kanda ya ziwa ambayo yamezuiliwa kusafirishwa nje ya nchi tangu alipotoa agizo la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga nje ya nchi Machi 2, mwaka huu.
Rais Magufuli alimwagiza aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu na vyombo vingine vya dola kuhakikisha mchanga wa madini unashikiliwa popote ulipo, mpaka hapo uchunguzi wa kina utakapofanyika kubaini ukweli. Baadaye Mangu alitenguliwa uteuzi wake, akamteua Simon Sirro kuwa IGP mpya.
Akiwa bandarini hapo, Dk. Magufuli alishuhudia udanganyifu mwingine uliofanywa na wafanyabiashara wanaoagiza mizigo kutoka nje ya nchi.
Hiyo ilikuwa ni baada ya kuoneshwa makontena ambayo nyaraka zinaonesha yamebeba nguo za mitumba na viatu wakati ndani yake kila kontena lilikuwa na magari matatu ya kifahari.

1428 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!