Na Mwandishi Maalum

Katika makala haya tunakuletea maelezo kuhusu Bandari ya Mtwara, ambayo ni miongoni mwa bandari kuu tatu (3) za mwambao wa Bahari ya Hindi zilizo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA). Bandari nyingine kuu ni za Dar es Salaam na Tanga. Bandari ya Mtwara ambayo inasimamia Bandari ndogo ndogo za Lindi na Kilwa ni lango la biashara kitaifa ambalo linategemewa kuwa kichocheo muhimu kwa uchumi wa viwanda kwa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.

Bandari ya Mtwara ilijengwa mwaka 1950, ikiwa na uwezo wa kuhudumia tani 400,000 kwa mwaka na ina gati yenye urefu wa mita 385 ikiwa na kina cha mita 9.5 (chart datum). Kulingana na aina ya meli zilizokuwa zikija Mtwara kipindi hicho, gati iliweza kutumika kuegesha meli tatu (3) kwa wakati mmoja zenye urefu kati ya mita 70 hadi 100 kila moja. Hivi sasa, meli zinazokuja zina urefu kati ya mita 150 hadi 210 kila moja, ambazo huegeshwa moja tu kwa wakati mmoja.

Lango la kuingilia meli katika bandari hii lina upana wa mita 250 na kina cha mita 20. Meli zinazoruhusiwa kuingia bandarini ni zenye urefu wa mita 175. Hata hivyo, kuna meli zenye urefu wa zaidi ya mita 175 zimeshaingia bandarini na kuhudumiwa.

Bandari ya Mtwara kwa kiasi kikubwa inategemea zaidi kuhudumia shehena ya korosho kutoka katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma katika Wilaya ya Tunduru. Katika mwaka 2016/ 2017 bandari ilihudumia shehena ya korosho tani 216,000 na mapato yatokanayo na kuhudumia shehena hiyo yalikuwa ni Sh Bilioni 20.266 sawa na asilimia 74 ya mapato mwaka huo ya Sh Bilioni 27.549. Mapato yatokanayo na kuhudumia shehena ya korosho yamekuwa yakiongezeka kwa wastani wa asilimia 20 kwa mwaka. Ongezeko hilo la mapato limechangiwa na ongezeko la shehena ya korosho inayozalishwa katika mikoa ya kusini mwa Tanzania.

Katika kuhakikisha tija inaendelea kuongezeka katika kuhudumia shehena ya korosho katika bandari ya Mtwara kwa mwaka 2017/ 2018, uongozi wa bandari hiyo kwa kushirikiana na wadau wake ulifanya maandalizi ya hali juu ambayo yalisaidia kufanikisha usafirishaji wa shehena ya korosho kutoka bandari hiyo.

Mipango iliyofanikisha usafirishaji wa shehena hiyo ya korosho ni pamoja na kuhakikisha bandari inafanya kazi saa 24 kwa siku 7 za wiki (24/7) na kufanya vikao vya kufanya tathimini na kupanga utendaji wa shughuli za meli na shehena mara 3 kwa wiki kwa siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa na kila mahitaji ya dharula yalipojitokeza.

Maandalizi mengine yaliyofanywa na bandari ni kuongeza eneo la kufanyia stuffing pamoja na eneo la kuhifadhia makasha. Pia bandari iliongeza eneo la kuegesha meli kutoka mita 285 hadi mita 385 ikilinganishwa na msimu uliopita.

Aidha maandalizi mengine yaliyochangia kuongeza tija ni uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo milango ya kupitishia shehena na maeneo ya ukaguzi (checkpoints) kwa lengo la kutumia mageti mawili ili kupunguza msongamano wa malori. Hatua nyingine iliyochukuliwa ni ununuzi wa vifaa ili kuboresha utendaji kazi wa karakana, kuimarisha ulinzi na usalama ikiwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya hujuma kwa bandari na taifa kwa jumla. Pia kuboresha mawasiliano na wadau wa bandari na kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana wakati wote.

Ili kuhakikisha Bandari ya Mtwara inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kwa mafanikio makubwa, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa kuipanua bandari ya Mtwara kuwa ya kisasa zaidi iweze kuhudumia shehena kubwa kwa kujenga gati namba 2. Gati hiyo inajengwa na Kampuni ya China Harbour Engineering ambapo uwekaji wa jiwe la msingi uliwekwa tarehe 4 Machi, 2017 na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

 

Ujenzi wa gati hiyo ambayo itakuwa na urefu wa mita 350 utakapokamilika utaongeza uwezo wa Bandari ya Mtwara katika kuhudumia shehena kubwa kama vile simenti kutoka kiwanda cha Dangote, makasha na mafuta kwa kutumia meli kubwa zaidi. Pia kukamilika kwa ujenzi wa gati hiyo kutafungua milango ya kiuchumi na hasa kwa nyakati hizi ambapo Tanzania ipo katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

 

Aidha uboreshaji wa miundombinu ya barabara na reli, utachochea matumizi ya Bandari ya Mtwara hususan kuongezeka kwa shehena itakayopita kwenye bandari hiyo. Kukamilika kwa miundombinu hiyo kutafungua uchumi wa Ukanda wa Mtwara na hasa ukuwaji wa viwanda ambavyo vitapata malighafi ya makaa ya  mawe kutoka Mchuchuma kwa ajili ya uzalishaji wa umeme.

 

Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara ndiyo unategemewa kuwa chachu ya uboreshaji na upanuzi wa bandari ya Mtwara kwa kufungua milango kwa nchi za Malawi, Zambia na Msumbiji kwa shehena ya madini. Katika nchi ya Malawi karibu migodi yote mikubwa iko Kaskazini mwa nchi hiyo. Hivyo bandari ya Mtwara ndiyo njia fupi zaidi kuliko bandari za Kusini mwa Afrika ikiwemo Bandari ya Durban, Afrika ya Kusini.

 

Serikali kupitia TPA imedhamiria kuboresha bandari ya Mtwara kunufaika na fursa kubwa zilizopo za kuhudumia shughuli za watafutaji wa mafuta/gesi, uzalishaji wa gesi asilia, bidhaa zitokanazo na gesi, bidhaa za viwanda vinavyojengwa mikoa ya Lindi na Mtwara, mazao mbalimbali yapatikanayo mikoani humo na maeneo ya jirani pamoja na bidhaa za madini na viwanda mbalimbali katika Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara (Mtwara Development Corridor) na nchi jirani za Msumbiji, Malawi na Zambia.

 

Aidha kwa upande wa Bandari ya Lindi, TPA imekamilisha ujenzi wa gati pamoja na uondoaji wa mchanga uliokuwa umetuama na kuzingira maeneo ya maegesho ya meli. Kukamilika kwa mradi huu ambao ulikuwa unatekelezwa na kandarasi Comfix & Engineering kutawezesha meli kuegeshwa moja kwa moja gatini na kuhudumiwa kwa urahisi.

2518 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!