1-mhandisi mkazi(kulia)Dejene na MagufuliMheshimiwa Rais, nianze kwa kukupa pole kwa majukumu mazito uliyonayo ya kulijenga taifa letu. Wananchi wanyonge wamekuwa na imani kubwa na wewe kutokana na juhudi zako ambazo umeishazionyesha katika kuwaletea maendeleo tangu uingie madarakani. Tunakutia moyo na kukuombea uendelee na juhudi hizo na tunaahidi kuwa nyuma yako katika kulijenga taifa letu.

Mheshimiwa Rais, nina mambo muhimu ya kukueleza kuhusu mfumo wa elimu yetu. Nimeamua kukuandikia wewe kwa sababu wewe ndiye mkuu wa nchi yetu na mambo yote yako chini yako. Serikali yako ikifanya vizuri, wewe ndiye utakayepongezwa, na ikifanya vibaya wewe ndiye utakayebebeshwa mzigo wa lawama.

Jambo la pili lililonifanya nikuandikie ni umuhimu wa elimu katika maendeleo ya taifa. Elimu ndiyo injini ya taifa lolote duniani. Taifa lililoelimisha wananchi wake kwa kuwapa elimu bora, huwa na maendeleo makubwa. Mataifa mengi duniani yameendelea kutokana na kuwekeza katika elimu bora kwa wananchi wake. Elimu hiyo bora imewasaidia kupata wataalamu mbalimbali waliochangia kuleta maendeleo katika nchi zao na hata nje ya mipaka ya nchi zao.

Mheshimiwa Rais, elimu bora inaundwa na mafiga matatu, yaani walimu bora, mazingira bora na vitabu bora. Nimetumia neno “mafiga”, kuonyesha kutegemeana kwa mambo hayo matatu. Ili mpishi aweze kupika chakula chake hadi kiive vizuri, hana budi kutumia mafiga matatu yenye ukubwa na ubora sawa. Ngoja nikupe mchapo mmoja uliowahi kutokea kijijini kwetu wakati nikiwa bado mdogo. Kuna mkulima mmoja aliondoka nyumbani kwake asubuhi na mapema kwenda shambani kulima, ulipofika muda wa mchana alihisi njaa, aliamua kurudi nyumbani kuandaa chakula.

Alipofika nyumbani kwake alitafuta mafiga matatu kwa ajili ya kupikia chakula. Mafiga mawili kati ya hayo yalikuwa na ukubwa sawa, na figa moja lilikuwa dogo kuliko yale mawili. Majirani zake walimshauri atafute mafiga yanayolingana, lakini yeye hakusikiliza ushauri wao. Aliwasha moto na kuweka sufuria la chakula kwenye mafiga, sufuria liliinama upande lakini yeye hakujali. “Unajua nini kilichotokea?” Chakula kilipoanza kuchemka kilimwagikia kwenye moto na kuuzima. Majirani zake walimcheka, alitokea jirani mmoja msamaria mwema aliyemuonea huruma na kumpa chakula alichokuwa nacho kutokana na njaa kali aliyokuwa nayo. Baada ya kukupa mchapo huo, naomba nianze kuelezea figa moja baada ya jingine.

Walimu bora. Hawa ni watu muhimu sana katika kutoa maarifa kwa wanafunzi. Walimu wakiandaliwa vizuri huweza kutoa maarifa sahihi kwa wanafunzi. Nchini Tanzania kazi ya ualimu inaonekana kupewa hadhi ya chini ukilinganisha na kazi nyingine, hii inatokana na sababu zifuatazo: kwanza, ni kipato kidogo wanacholipwa walimu ukilinganisha na kazi wanazofanya; pili, ni ufaulu wa kiwango cha chini kwa wanafunzi wanaoenda kusomea taaluma ya ualimu. Asilimia kubwa ya wanafunzi wanaoenda kusomea ualimu kwa ngazi ya cheti na stashahada ni wale ambao hawakufanya vizuri katika mitihani yao ya kuhitimu elimu ya sekondari. Kutokana na ufaulu huo wa kiwango cha chini, wengine hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu na hivyo kulazimika kujiunga na vyuo vya ualimu kama kimbilio pekee. Utaratibu huu wa vyuo vya ualimu kuchukua wanafunzi ambao hawakufanya vizuri katika mitihani yao ya kuhitimu elimu ya sekondari, umeifanya jamii iione kazi ya ualimu kama ni ya watu waliofeli na kukosa njia nyingine ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu.

Siku moja nilimsikia baba mmoja akimuuliza jirani yangu, “vipi matokeo ya kijana wako?” Jirani alijibu, “hajafanya vizuri sana”, yule baba aliuliza, “hawezi kupata hata nafasi ya ualimu?” Hii inaonyesha wazi kwamba, jamii inaiona taaluma ya ualimu kama ni ya watu waliofeli katika mitihani yao ya sekondari. Kutokana na mtazamo huo, wanafunzi wengi wanaofaulu vizuri kwenye mitihani yao ya mwisho katika elimu ya sekondari hukataa kwenda kusomea ualimu. Tujiulize, kama vyuo vya ualimu vinachukua wanafunzi ambao hawakufanya vizuri katika mitihani yao, tunaandaa taifa la wataalamu wa aina gani?

Tukitaka kupata walimu bora watakaojitoa kufanya kazi kwa ufanisi, hatuna budi kuzingatia mambo yafuatayo:

1. Kuboresha maslahi ya walimu, kuwapa stahiki zao zote na kuwapandisha madaraja kwa wakati. Kisheria mwalimu anapomaliza miaka mitatu kazini tangu aajiriwe anastahili kupandishwa daraja na kuongezewa mshahara, lakini hilo halifanyiki kwa walimu walio wengi, jambo ambalo linawavunja walimu moyo wa kujitolea kufanya kazi kwa bidii;

2. Kuwapa wathibiti ubora wa shule mamlaka ya kupendekeza wakuu wa shule pamoja na wasaidizi wao kulingana na sifa na utendaji kazi wao tofauti na ilivyo sasa, ambapo wakuu wa shule huteuliwa na maafisa elimu wa wilaya ambao hawako karibu na walimu na hawawajui vizuri ukilinganisha na wathibiti ubora wa shule ambao wako karibu zaidi na walimu na wanafahamu vizuri uwezo wa kila mwalimu;

3. Kuboresha maslahi ya wakuu wa shule na wasaidizi wao ili waifanye kazi ya kuwasimamia walimu kikamilifu; 4. Kuboresha idara ya uthibiti ubora wa shule kwa kuipatia mahitaji yote muhimu yanayotakiwa katika kazi yao pamoja na vitendea kazi kama vile magari ya kutosha ili waweze kuzungukia shule zote na kukagua utendaji kazi wa walimu pale inapotakiwa.

Nina imani kuwa walimu wakisimamiwa vizuri na kupandishwa madaraja kwa wale watakaoonekana kuifanya kazi yao vizuri, watafanya kazi kwa ufanisi mkubwa; 5. Kuwajengea walimu nyumba za kuishi karibu na mazingira ya shule ili wawe karibu na vituo vyao vya kazi; 6. Kuboresha mazingira ya shule za vijijini kwa kuhakikisha kuwa kuna huduma za afya, maji, miundombinu mizuri na umeme wa jua kama umeme wa gridi ya taifa haujafika huko;

7. Kuwa na mgawanyo sawa wa walimu kati ya shule zilizoko mijini na zile zilizoko vijijini tofauti na ilivyo sasa, ambapo shule nyingi za mijini zina walimu wengi ukilinganisha na shule zilizoko vijijini, mfano mzuri ni shule ya msingi Mahina iliyopo Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza ina jumla ya walimu 45 na shule ya msingi Tandari iliyopo Kata ya Bunduki, Mkoa wa Morogoro ina walimu wawili (2) tu wanaofundisha kuanzia darasa la kwanza hadi la saba;

8. Vyuo vinavyoandaa walimu wa shule za msingi, vianzishe utaratibu wa kuandaa walimu watakaofundisha masomo yasiyozidi matatu ambayo waliyafaulu vizuri kwenye mitihani yao ya kuhitimu elimu ya sekondari, kuliko utaratibu uliopo sasa unaowaandaa walimu kufundisha masomo yote hata yale waliyopata daraja “F” kwenye mitihani yao ya elimu ya sekondari;

9. Kuongeza idadi ya vyuo vinavyofundisha elimu ya awali ili tupate walimu wengi watakaokidhi mahitaji, tofauti na ilivyo sasa ambapo katika shule nyingi, walimu wanaofundisha elimu ya awali, wengi wao hawajasomea taaluma hiyo. Elimu ya awali ndio inayomjengea mtoto msingi bora wa elimu. Tukumbuke kwamba, mtoto anapokuwa hajaanza shule, ubongo wake huwa hauna mambo mengi na hupokea kwa haraka na kuyashika yale anayoyaona na kuyasikia.

Kama tukiziboresha shule zote za awali kwa kuwa na walimu waliosomea taaluma ya kufundisha na kulea watoto na kuzipatia vifaa vyote vya kufundishia na kujifunzia, tutawajengea watoto wetu msingi bora wa elimu na kuwafanya waipende shule na pindi watakapoanza darasa la kwanza, watakuwa wanafunzi wenye mwanga mzuri;

10. Kuwaimarisha walimu kiutendaji kwa kuchukua hatua zifuatazo: kuwapatia mafunzo kazini kwa nia ya kuwaimarisha katika masomo yao, kuwapanga katika makundi ya masomo yao (specialization) mfano masomo ya Sayansi na Hesabu; Kiswahili na Kiingereza; Historia, Jiografia na Uraia; 11. Kuanzisha taasisi za mikopo kwa walimu (sacoss) ili wapate mikopo ya kuboresha maisha yao.

Tukizingatia yote hayo, tutawavutia hata wale waliokuwa hawapendi kusomea ualimu, na hivyo kupata walimu wengi bora na si bora walimu. Je, ni mazingira yapi yatamfanya mwalimu kutoa elimu bora? Ni vitabu vipi vitamfanya mwanafunzi kupata elimu bora? Usiikose nakala ya JAMHURI wiki ijayo kwa mwendelezo wa ujumbe huu mahususi kwa Rais John Pombe Magufuli.

 

Barua hii imeandikwa na Ndugu:-

KALISTI MJUNI

Mdau wa elimu (msomaji wa JAMHURI) 0762488763

Email: [email protected]

By Jamhuri