Mohamed Suleiman (Osama) anayedai kumiliki eneo lenye mgogoro
Mohamed Suleiman (Osama) anayedai kumiliki eneo lenye mgogoro
Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa inahaha kuongeza mapato, kampuni moja ya mafuta inayolipa kodi ya wastani wa Sh bilioni 3 hadi Sh bilioni 4 kwa mwezi, imefungiwa ofisi zake kutokana na mgogoro wa ardhi usioihusu, JAMHURI limebaini.

Kwa hatua hiyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itapoteza kodi hiyo iliyokuwa ikilipwa na kampuni hiyo ya Petrofuel (T) Limited.

Petrofuel (T) Limited ni mpangaji katika kiwanja kinaachodaiwa kumilikiwa na kampuni ya Educational Books Publishers Limited, kiwanja namba 12B, sehemu ya E.P Lot 20, kilichoko Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam.

Kampuni ya Educational Books Publisher, inamilikiwa na mfanyabiashara Mohamed Suleiman Mohamed (Osama), anayetajwa kuwa na vitega uchumi kadhaa jijini Dar es Salaam.

Osama, ameingia kwenye mvutano wa umiliki wa kiwanja hicho na mfanyabiashara Hasham Kassam, ambaye anadai kuwa na umiliki halali wa kiwanja hicho chenye hati Na. 186074/21. Kassam ndiye aliyeingia mkataba wa kukodisha eneo hilo kwa kampuni ya Petrofuel.

Pamoja na kutolipwa kwa kodi hiyo, wakili wa kampuni hiyo ameiambia Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kuwa maelfu ya wananchi walio jirani na maghala ya kampuni hiyo wanakabiliwa na janga la moto ambao huenda ukasababishwa na matangi ya mafuta ambayo wataalamu wa Petrofuel wamezuiwa kuyasogelea ili kuhakiki usalama wake.

Kwa mujibu ya nyaraka ambazo JAMHURI limeziona, kampuni hiyo imejikuta ikiondolewa katika eneo hilo licha ya kuingia mkataba halali wa upangaji na mmiliki.

Nje ya Mahakama, imeelezwa kuwa juhudi za uongozi wa Patrofuel, za kuomba mamlaka za kidola zisaidie kuepusha hatari ya mlipuko huo zimegonga mwamba baada ya kukosa ushirikiano katika ngazi ya Polisi na Mkoa wa Dar es Salaam.

Pia kitendo cha kutumiwa kwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kwenye operesheni hiyo, nacho kimeelezwa kuwa si cha kawaida katika mazingira ambayo hayakuwa na ukinzani kutoka kwa anayehamishwa.

Hivi karibuni, kampuni ya udalali ya Yono ilikwenda kutekeleza amri ya kufunga ofisi za kampuni hiyo katika mazingira ambayo bado yanaibua maswali kadhaa.

Kwenye operesheni hiyo, Petrofuel wanalalamika kuibiwa mali kadhaa, vikiwamo vifaa na fedha taslimu.

“Operesheni ya kufunga ofisi za kampuni ya Petrofuel (T) Limited zilisimamiwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia, pamoja na watumishi wa kampuni ya udalali…hawakuonesha nyaraka zinazowaruhusu kufanya hicho walichokifanya,” kimesema chanzo chetu.

Walipotafutwa viongozi wa kampuni ya Petrofuel kuzungumzia sakata hilo , walielekeza JAMHURI kuzungumza na Mwanasheria wa kampuni hiyo, Dk. Masumbuko Lamwai, ambaye hata alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi, hakupokea.

Kampuni ya Petrofuel (T) Limited ilipeleka Mahakama Kuu hati ya kuomba kuzuia kuondolewa katika kiwanja hicho. Suala hilo lilifikishwa Mahakama Kuu. Katika shauri hilo, kampuni hiyo na nyingine ya Isa Limited, zimewashtaki Educational Books Publishers Limited, Wilson Ogunde na Yono Auction Mart and Court Brokers.

Kwa mujibu wa nyaraka za Mahakama, shauri hilo lilisikilizwa na Jaji Lugano Mwandambo, katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Julai 21, mwaka huu. Uamuzi wa, au kutoa, au kutotoa hati ya zuio unatajiwa kutekelezwa wiki mbili zijazo.

Kampuni hiyo inasema uvamizi na kufunga ofisi zao ulifanywa kwa nguvu na hivyo kusababisha hasara kubwa ya mali na fedha.

“Uamuzi wa kutuondoa katika eneo linalozungumzwa katika shauri hili litatusababishia hasara ya kati ya Sh milioni 200 hadi Sh milioni 400 kwa siku. Waliingia hapa na mashine zinazotumia gesi kukata milango pamoja na makufuli,” inasomeka sehemu ya shauri hilo.

Katika shauri hilo, kampuni ya Petrofuel (T) Limited inasema kuna matangi sita ya mafuta ya dizeli yenye lita 278,000 pamoja na vipuli vya mitambo na magari kwa ajili ya migodi ya madini.

Kampuni hiyo inasema endapo haitaruhusiwa kuokoa mali hizo, itafilisika kutokana na kutopewa fidia na taasisi za kifedha.

“Tunashauri kwamba namna bora ya kushughulikia hayo matangi ya mafuta kunahitajika utaalamu mahsusi ambao hao tunaowashtaki hawana, hivyo matangi hayo yanaweza kulipuka,” inasomeka sehemu ya shauri hilo.

Mmoja wa watumishi wa kampuni ya Petrofuel (T) Limited, ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, anasema lilikuja kundi la watu ofisini kwao na kuanza mabishano na mtumishi wa mapokezi, na baadaye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo alitaka kupatiwa ufafanuzi wa ujio huo, lakini hakujibiwa.

“Mkurugenzi Mtendaji alitaka kupatiwa maelezo ya kina pamoja na kuoneshwa barua zinazowaruhusu kutekeleza agizo hilo, hawakufanya hivyo na badala yake walimsukumia pembeni na kuingia katika ofisi zetu na kuanza kutoa vitu nje, baadaye wakaanza kutoa magari nje kwa kutumia winchi,” anasimulia mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Anasema walimpigia simu mwanasheria wa kampuni hiyo baada ya kuwauliza na kubaini kuwa hawakuwa na nyaraka zozote za kuwaruhusu kuiondoa kampuni katika ofisi hizo.

“Baadaye tukampigia Mkuu wa Kituo cha Polisi Chang’ombe, akamtuma mpelelezi wa kituo hicho, ambaye baada ya kuwauliza maswali kuhusu nyaraka zinazowaruhusu kufanya zoezi hilo, walianza kuondoka mmoja mmoja.

“Tulishangaa kuvamiwa hapa ofisini, huku wavamizi wetu wakiwa wamesindikizwa na askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia…walikuja hapa wakiwa wamesindikizwa na maaskari, tungependa kuona askari wanafuata taratibu za kazi zao, maana alipokuja mpelelezi wa Kituo cha Chang’ombe na kuwahoji walianza kuondoka mmoja mmoja,” anasema mfanyakazi huyo.

Akizungumza na JAMHURI, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Gilles Muroto anasema anafahamu kuhusu suala hilo, lakini hawezi kulisemea kwa kuwa liko mahakamani.

Jitihada za kumtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya udalali ya Yono, Yono Kevela hazikuzaa matunda kutoka na kutopatikana kupitia simu yake ya mkononi.

By Jamhuri