Baada ya kuandika makala ya “Biashara za sasa zinahitaji u-sasa”, kuna jambo nililitazamia ambalo limetokea kama yalivyokuwa matarajio yangu. Kumekuwa na wasomaji wengi nchi nzima ambao wameleta maombi na ushauri wakitaka niwasaidie kusajili biashara zao katika mfumo wa kampuni.

Jambo hili si mara ya kwanza kutokea na ndiyo maana leo nimeamua kuandika barua hii kwenda kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni Tanzania (BRELA). Nakala ya waraka huu naipeleka pale Wizara ya Uwezeshaji, pia nampelekea Waziri wa Viwanda na Biashara. Hata hivyo, nianze kwa kuwapongeza BRELA kwa kazi wanazofanya.

 

Kama wote wakishindwa kutekeleza mbinu za kisayansi nitakazowapa, basi nitakwenda kumuona rais. Hata hivyo, sina shaka nao kwa sababu nina imani kubwa na serikali na ninajua watayafanyia kazi maudhui ya barua hii. Ninachoandika hapa si mawazo (opinions) ila ni utafiti (research) wa kitaalamu.

 

Miaka miwili iliyopita niliandika kwa kina makala (si katika gazeti hili) kuhusu biashara katika mifumo ya kampuni. Mwitikio wa wajasiriamali kutoka nchi nzima ulikuwa mkubwa. Kuna mamia niliowashauri kwa simu, lakini kuna wengine wengi waliosafiri kutoka sehemu mbalimbali na kuja kukutana nami Iringa.

 

Kuna bwana alisafiri kutoka Kibondo hadi Iringa akitaka nimsaidie kusajili kampuni yake akiwa na biashara za mambo ya karakana za mbao. Nilimshauri kufanya baadhi ya mambo yatakayosuka biashara yake ndipo twende BRELA tukasajili kampuni yake.

 

Mzee mwingine yuko Gairo akiwa anajishughulisha na kilimo, alinitumia nauli nikasafiri hadi Gairo na kuonana naye. Nilistaajabu mno kuona ana mtaji mkubwa, ana wafanyakazi wengi, lakini bado anaendesha biashara kienyeji kabisa. Nilishughulika naye na nikamwachia dhima fulani ya kukamilisha kabla hatujaenda BRELA kusajili kampuni.

 

Rafiki yangu mwingine kutoka Morogoro alisafiri hadi Iringa na nikashughulika naye kiushauri na tukaanza michakato ya kuzisuka biashara zake za usambazaji wa bidhaa na kilimo. Hii ilijumuisha kuandaa michanganuo ya kibiashara, kuandaa nyaraka za kampuni, kutengeneza mifumo ya kiutawala na kimenejimenti. Huyu anaendelea vizuri na ningali naendelea kumuunga mkono ili atimize ndoto yake.

 

Nimeanza kutoa mifano hiyo michache ili kuchanganua mambo kadhaa ambayo ni mzigo kwa wajasiriamali wengi. Ikumbukwe kuwa sehemu kubwa ya uchumi wa nchi hii ipo katika sekta isiyo rasmi. Tunaposema sekta isiyo rasmi tunamaanisha kuwa kuna shughuli nyingi za kiuchumi zinazoendelea pasipo kurekodiwa kwenye mwenendo wa uchumi wetu.

 

Ni pale mtu anapokuwa na mtaji labda wa shilingi milioni hata 500 na wafanyakazi zaidi ya 50 lakini wafanyakazi wake hawana mikataba ya ajira, hawalipiwi kodi, bima au kuchangia mifuko ya hifadhi ya jamii. Tunapogusia biashara kusajiliwa katika mifumo ya kampuni, ni sehemu ya kurasimisha biashara hizo.

 

Kimsingi gharama za usajili wa biashara BRELA ni ndogo. Mathalani, kusajili jina la biashara ni Sh 60,000. Kusajili kampuni yenye mtaji wa kati ya Sh 100,000 hadi Sh 5,000,000 ni takribani Sh 130,000. Hata biashara zenye mtaji wa kuanzia Sh milioni 5 na kuendelea usajili wake ni wastani wa Sh 250,000.

 

Lakini kuna mambo takribani manne yanayokwamisha. Mosi, BRELA ipo Dar es Salaam pekee. Pili, wajasiriamali wengi hawana taarifa kuhusu biashara katika mifumo rasmi. Tatu, viambata vya usajili vina milolongo yenye gharama; na nne, wajasiriamali wanakosa ushauri wa kibiashara na kisaikolojia kabla na baada ya kusajili biashara au kampunni zao.

 

Nianze na hili la ukosefu wa taarifa. BRELA ipo Dar es Salaam lakini mfanyabiashara anasafiri kutoka Kibondo kwenda Iringa kufuata usajili! Au mfanyabiashara anasafiri kutoka Morogoro kurudi Iringa badala ya kwenda Dar es Salaam. Au mjasiriamali anakuwa hajui pa kwenda, badala yake anaingia gharama kulipa nauli nifike Gairo.

 

Wajasiriamali hawa walionifuata wapo sahihi kwa asilimia 100 tukiitazama sababu ya nne ambayo ni ushauri wa kibiashara na kisaikolojia. Kazi kubwa ya BRELA ni kusajili. Haya ya kisaikolojia na ushauri wa kina wa kibiashara hayamo katika orodha ya kazi zao. Na hapa ndipo ilipo changamoto!

 

Ni vigumu kufikia lengo la kurasimisha biashara nchi hii kwa kasi kama tutaendelea na mbinu hizi hizi. Natamani BRELA wafungue kitengo au dawati maalumu litakalobeba jukumu la kuwashauri wajasiriamali kibiashara na kisaikolojia kwa kina. Liwe ni dawati au kitengo kitakachokaliwa na watu wenye uwezo wa kushauri na kuibua hamasa kwa wajasiriamali na wanaotamani kuingia kwenye ujasiriamali.

 

Naamini BRELA ina mikakati na mipango ya kufungua matawi mikoani. Lakini ninashauri hawa mameneja wa mikoani wasiajiriwe kwa kuangalia vyeti vyao, badala yake wapimwe kwa uelewa halisi wa biashara na ujasiriamali.

 

Tutakapokuwa na mameneja wa mikoani wa BRELA ambao mjasiriamali anapofika ofisini au wanapomtembelea ajisikie kufunguliwa, ajisikie kuona fursa mpya kibiashara na kisaikolojia pia. Nchi yetu ina tatizo moja kubwa sana nalo ni kuwa watu wanaohudumia wafanyabiashara wengi wao hawajui biashara (biashara kwa vitendo).

 

Ukitaka ujue hili kutana na polisi wa usalama barabarani anayekamata gari la biashara, na kulikwamisha kwa saa kadhaa bila sababu za msingi pasipo kujua hasara anayopata mmiliki wa basi pale abiria wanapokasirika kwa kucheleweshwa. Au kutana na ofisa wa serikali anayehamasisha ujasiriamali wakati yeye mwenyewe hana hata banda la kuku!

 

Au kutana na afisa mikopo wa benki anayekucheleweshea mkopo kwa makusudi ili umpe “cha juu”, wakati wewe unafukuzana na muda ukanunue mbolea za kupandia. Anaweza kuja kusaini mkopo wakati mvua za kupandia zimeshaisha!

 

Ndiyo maana ninapendekeza BRELA iwe na kitengo maalumu cha kuhamasisha, kuibua na kulea vipaji vya biashara. Wizara ya uwezeshaji inaweza kuunganisha nguvu pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara katika uibuaji ajira hasa kwa vijana kupitia ujasiriamali. Mara nyingi nimeandika tena kwa mifano kuwa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wa nchi hii si ukosefu wa mitaji.

 

Huu utaratibu wa kutenga bilioni kadhaa katika wizara zetu si mbaya, lakini kuna mambo madogo tu hayafanyiki ambayo yakifanyika vijana wengi wataokoka dhidi ya ukosefu wa ajira. Wakati mwingine tunachelewa mno kuwasaidia vijana. Tusisubiri waanze kurandaranda mitaani ndipo tuwafikirie.

 

Tunatakiwa tuwapike kwa programu maalumu wakiwa kule kule masomoni kabla hawajakabidhiwa vyeti “vinavyowazuzua”. Na katika hili naona BRELA ina nafasi kubwa mno kulifanikisha kuliko kitengo kingine chochote. Mbali na hilo, ipo haja ya kuwasaidia hawa wajasiriamali kumiliki biashara imara na zinazoelezeka katika mifumo rasmi. Haya ninayopendekeza hayahitaji fungu la bajeti, hata kwa kujitolea naweza kufanya kazi na BRELA kufanikisha haya.

Hapo juu nimechambua suala la ofisi za BRELA mikoani na hivyo nimeshagusia BRELA kujichimbia Dar es Salaam. Huku mikoani kuna ofisi za biashara na moafisa biashara. Kama tatizo ni fedha, BRELA inaweza kutumia hawa maofisa biashara. Kama tatizo ni ofisi, BRELA inaweza kutumia ofisi hizi za biashara kwa ajili ya mameneja wa BRELA wilayani na mikoani.

 

Nieleze sasa suala la gharama za viambatanisho vya usajili. Unaposajili kampuni unahitaji kuandaa nyaraka za kampuni (articles of association & memorandum of association) pamoja na kujaza fomu kadhaa za BRELA. Nyaraka hizi huandaliwa kwa lugha ya kibiashara na kisheria hivyo zinahitaji wataalamu. Hapa ndipo palipo na gharama kwa sababu mara nyingi waandaaji wa nyaraka hizi hutoza fedha nyingi.

 

Huu ni mzigo kwa mjasiriamali anayetaka kusajili kampuni yake yenye bodaboda moja. Lakini kama BRELA ikiamua inaweza kutoa bure huduma hizi katika ofisi zake, yaani wakawapo wataalamu wa mambo ya biashara na sheria watakaowaandalia bure wajasiriamali kwa gharama ndogo nyaraka hizi.

 

Nimeona siku hizi kuna mfumuko wa watu wanaojitangaza eti, “tunasajili kampuni” wakati wao si BRELA. Wamekuwa ni madalali wanaochuuza na kupandisha bei usajili wa kampuni pengine kutokana na mwanya wa changamoto zinazoikabili BRELA.

Kutokana na gharama za hizi nyaraka pamoja na michakato ya usajili wa kampuni kuonekana kuwa na sura ya kisomi sana, wajasiriamali wengi huwa wanakata tamaa kusajili biashara zao katika mifumo rasmi ukizingatia kuwa wanaona mambo yao yanaenda kama kawaida hata wasiposajili kampuni. Hii ni hatari.

 

Kwa utafiti wangu unaotokana na kukutana na kutoa ushauri wa kibiashara kwa wajasiriamali wengi, kuna mambo nimebaini. Kimsingi kuna mambo mengi mno ambayo mfanyabiashara anatakiwa kusaidiwa  kabla na baada ya kusajili kampuni. Anahitaji kuelimishwa uendeshaji, kupanuliwa mtazamo na maono yake, kuimarisha saikolojia yake pamoja na kutiwa moyo (motivational sparks).

Mafanikio mengine yote hufuata baada ya mambo niliyoyataja kuwekwa sawa. Hili ndilo ambalo BRELA hailifanyi na ninalowashauri waanze kufanya. Kwa kuwa mimi ndiye niliyetoa wazo hili (kwa BRELA na kwa waziri), kama wakiona linafaa, niko tayari kuwasilisha mchanganuo wa kina na kuisaidia wizara na BRELA kukaa nami katika meza ya usaili niwaelekeze watu sahihi wa kusimamia programu  hii kitaifa.

 

Wajasiriamali wanahitaji ushindi wa kiuchumi.

0719 127 90, [email protected]


By Jamhuri