Wafanyakazi turudi, tutafakari, tuamue, tujitambue

Kwa muda mrefu nimekuwa nikifuatilia hali ya mambo ndani ya mashirikisho ya vyama vya wafanyakazi Tanzania, baadhi yanafurahisha na mengine yanatia simanzi.

Nianze kwa kutangaza kuwa nami ni mdau wa vyama hivi nikiwa mwajiriwa wa Serikali Kuu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, katika nafasi ya mwanasheria wa sekrataieti ya mkoa na pia nikiwa nakaimu nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Mkoa wa Lindi kwa kitambo kidogo.

 

Wapendwa wasomaji, naomba nieleweke vizuri kuwa hapa natoa mtazamo wangu kama mfanyakazi na wala siwasilishi maoni na matakwa ya kundi au chama (trade union) fulani.

 

Katika Gazeti JAMHURI toleo namba 100 la Jumanne September 10-16, kwenye sehemu ya barua/kauli za wasomaji niliandika nikiwaasa TUGHE na TALGHWU kumaliza changamoto inayowakabili na kweli nilipata simu nyingi toka Mwanza na hata Zanzibar na wengi wa walionitafuta ni wenye kukerwa na hali ya mambo ndani ya vyama vya wafanyakazi na wengine walitaka niwape elimu zaidi. Niseme asante JAMHURI kwani hambagui mtu mwenye maoni ya kujenga.

 

Nimeanza na maneno kuwa wafanyakazi turudi na kutafakari, tuamue na kujitambua kutokana na hali ilivyo sasa, kama si mfuatiliaji waweza usijue kabisa kuwa yupo mdudu anayeitwa (divide and rule) anaendelea kuondoa MSHIKAMANO.

 

Kwa wiki kadhaa kwenye magazeti na mitandao ya kijamii, habari zimekuwa zikielezwa juu ya sintofahamu kwenye vyama vya wafanyakazi, hasa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ambako nilisoma kwenye blogu ya Wananchi kwamba walimu mkoani Mbeya walikutana na kupitisha maazimio na kilichojiri zaidi ni juu ya makato ya asilimia mbili bila idhini ya mwanachma kwa mjibu wa Waraka wa Utumishi wa Umma Namba 1 wa mwaka 2013 uliotolewa na Katibu Mkuu wa Utumishi, George D. Yambesi, Mei 6, 2013.

 

Vile vile nikasoma kwenye blogu ya Kalulunga Media, Sauti ya Wasiosikika, habari iliyowekwa Julai 2013, yenye kichwa ”Serikali yatoa waraka wa kuua vyama vya wafanyakazi.” Mwandishi kaeleza kiuweledi yanayojiri ambapo alieleza kwamba sasa walimu wameamua kuendelea kukatwa bila idhini na hata wengine wameanzisha vyama vyao kwa mjibu wa sheria.

 

Mfano, huko Kigoma wameanzisha chama kinachoitwa Chama cha Walimu Huru na Mbeya wameanzisha chama cha kutetea Maslahi ya Walimu Tanzania.

 

Na kwa kuhitimisha, gazeti la Habari Leo toleo la Septemba 18,  2013 kuna habari liyosomeka ”Walimu wapanga kujitoa CWT”, na hii ilitokea huko Ukerewe, Mwanza suala likiwa ni hayo makato ya asilimia mbili bila kuwa wanachama.

 

Kwangu mimi, hizi ni nyakati za hatari kwa vyama vya wafanyakazi, kama hujui fumbua macho mfanyakazi uone, inawezekana vyama vingine vimenyamaza, lakini nako moto utawaka muda si muda.

 

Sasa nani alaumiwe? Je, ni viongozi wa vyama vya wafanyakazi? Waraka wa Serikali au wafanyakazi? Hapo lazima tusaidiane.

 

Kwa wale wakubwa zaidi yangu waliokuwepo kabla na baada ya uhuru achilia mbali sisi wa miaka ya themanini na ushee, wanatambua harakati walizokuwa wanafanya wafanyakazi enzi za NUTA, JUWATA, OTTU ambapo kwa takwimu walikuwepo wafanyakazi zaid ya 182,000 waliokuwa wanapambana na ukandamizaji wa waajiri.

 

Ikumbukwe wakati huo vyama hivi vilikuwa na bahati ya kupata ruzuku kutoka serikalini hadi mwaka 1988 hadi ilipotungwa Sheria ya Vyama vya Wafanyakazi (trade Unions Act No.10) ambayo iliondoa ruzuku na kuvifanya vyama vya wafanyakzi kuwa huru na vyenye kujiendesha vyenyewe.

 

Mwaka 2004 ikapitishwa sheria Namba 6, Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini na kanuni zake za mwaka 2007. Hapa nikushauri mfanyakazi ukizipata kanuni hizi ni msaada mkubwa.

 

Kwa mjibu wa sheria hii ya Ajira na Uhusinao Kazini kila kitu kiko wazi kwani kifungu cha 9 kinatoa uhuru wa mfanyakazi kujiunga na chama chochote na ukisoma kifungu cha 46 (d) cha sheria hiyo kinataka idadi ya wanachama wanaoweza kuunda chama iwe kwa namba ya chini wafanyakazi 20. Kwa haraka hiyo ni namba ya walimu wa shule moja au wafanyakazi wa ofisi moja ya Mkuu wa Mkoa, n.k.

 

Kwa mantiki hii, kumbe alichokifanya Katibu Mkuu wa Utumishi kwa kutoa waraka ni kutafsiri sheria na kutoa mwongozo ambao kwao hatakiwi hata kulaumiwa kwani ni sehemu ya majukumu yake ya kazi na kweli ukisoma waraka huo utaona kuwa alifikia hatua hiyo baada ya mkanganyiko mkubwa kujitokeza miongoni mwa wafanyakazi.

 

Nisitake kuhisi kuwa vyama vya wafanyakzi havikupata kusoma Sheria Namba 6 ya 2004, na kama walisoma utaratibu huu wa kuwajumuisha watumishi bila idhini yao ulitoka wapi na kwa hili ilaumiwe serikali?

 

Naamini vyama vya wafanyakazi vina nia njema ya kupigania maslahi kama wanavyofanya na mimi ni shahidi, nimeona Mwenyewe CWT Wilaya ya Lindi Vijijini wakiwalipia walimu wawili gharama za utetezi waliokuwa na shauri mahakamani.

 

Pia nimeona TUGHE Mkoa wa Lindi ikipigana mpaka mfanyakazi aliyekosa kupandishwa cheo miaka nane anapandishwa na waliofukuzwa wanarejeshwa kazini, yumkini hata wewe umeona hayo au labda viongozi wetu wanasahau wajibu wao kuwa ni kueleza yale wanayoyafanya? Lazima kubadilika.

 

Niseme ninayo mengi ila nafasi haitoshelezi kuyadadavua ila wafanyakazi lazima turudi tutafakari. Je, kuanza kuunda utitiri wa vyama ndiyo tiba ya matatizo yetu? La hasha, hii ni kujigawa na kukosa nguvu kabisa. Natamani viongozi wa vyama vyote vya  wafanyakazi chini ya mwamvuli wa TUCTA wakae na kutafakari, hili ni pigo kwetu wafanyakazi. Je, tutashinda kwa kujitenga?

 

CWT tafakarini mtatue yote yanayowakwaza wanchama. TUGHE na TALGHWU jadilini ni nini nafasi ya watumishi wa afya, si nyakati za kudanganyana na mikopo hapana, ni nyakti za uwazi na ukweli na viongozi wa vyama vya wafanyakazi acheni siasa ndani yenu, zingatieni sheria na taratibu zetu.

 

Na wafanyakazi tuache kujitenga, tujaze hizi fomu za uanachama ili tuwe wenye sauti ya kuleta mabadiliko ndani ya vyama vyetu. MSIHIKAMANO DAIMA

 

Albert Mwombeki (Advocate),

Kaimu Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Lindi

Simu: 0688 405 748, 0766 421 108

 

2338 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!