“Mimi sifanyi siasa hapa, natekeleza jukumu langu kama mwenyekiti wa kamati, kwa hiyo hili ni onyo kwao, nipo tayari kunyongwa nikitetea maslahi ya umma.”

Maneno haya makali yalitamkwa na Zitto Zuberi Kabwe baada ya baadhi ya vyama vya siasa kikiwamo chama chake Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuzungumza na vyombo vya habari na kukanusha taarifa za awali zilizotolewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kupitia kwa Zitto ambaye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo.

 

Mvutano huo mkali wenye maneno makali kutoka kwa Zitto na vyama vya siasa, hususan Chadema na Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku kila upande ukishutumu upande mwingine, umenifanya nijiulize baadhi ya mambo kadhaa ikiwamo nafasi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, na vyama vya siasa vinavyotuhumiwa katika sakata hili, pia nafasi ya Zitto kama Mwenyekiti wa PAC na nafasi yake kama kiongozi mwandamizi wa Chadema.

Kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Zuberi Kabwe, juu ya kuagiza ruzuku za vyama vya siasa kusitishwa kwa kile kinachosemwa na kamati hiyo kupitia kwa Zitto kwamba hesabu za vyama hivyo hazijakaguliwa na CAG kwa muda wa miaka minne sasa.


Tumeshuhudia pia baadhi ya vyama vya siasa vikijitokeza kukanusha madai ya kamati ya PAC.

CCM, kupitia kwa katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, wameeleza kuwa chama chao kimekaguliwa na kwamba wana ushahidi wa nyaraka zinazothibitisha hilo, lakini pia akamalizia kwa kuilaumu Kamati ya Bunge ya PAC inayoongozwa na Zitto Zuberi Kabwe juu ya kauli na shutuma zake kwa chama hicho.

Baadaye Chadema kimeueleza umma kuwa kimewasilisha taarifa zake za fedha kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa, zilizokaguliwa kwa mwaka wa fedha 2010/2011 na 2011/2012. Chadema wakasisitiza kuwa majibu yao yanathibitishwa na barua ya Msajili wa Vyama yenye kumb. Na. CDA .112/123 /01a/ 37 ya Septemba 4, 2012.

Uthibitisho huo umetolewa kukanusha taarifa ya Mwenyekiti wa PAC kwa ajili ya kufanyiwa ukaguzi na CAG, kwa kipindi cha miaka minne mfululizo.

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Antony Komu, amekanusha madai ya PAC kwa kusema, “Taaifa za PAC si sahihi na hazina ukweli wowote, hususan kuhusiana na Chadema, labda kwa vyama vingine.’’

Pia Komu aliwaonesha waandishi wa habari barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ya Septemba 4, 2012 inayoonesha hesabu zilizokaguliwa kwake ni za Chadema na NCCR-Mageuzi.

Kwa mujibu wa barua hiyo, CUF waliwasilisha hesabu kwa Msajili bila kukaguliwa. Vyama ambavyo inadaiwa havikuwasilisha hesabu zao ni CCM, TLP, APPT-Maendeleo, UDP na DP.

Mkurugenzi huyu wa fedha wa Chadema akamalizia kwa kusema kwamba kama kweli tangu 2009 hesabu hazijakaguliwa, basi aulizwe CAG, ofisi yake inafanya nini ikiwa fedha zinatolewa mwaka wa kwanza mpaka wa nne hazikaguliwi?

Lakini na mimi nimuulize Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, kama majibu ya chama hicho ndiyo hayo, tena kutoka kwa Mkurugenzi wa fedha ambaye Zitto wa PAC ni bosi wake ndani ya Chadema, tumwamini nani kati ya Zitto na chama chake?

Na kama kwa mfano Chadema siyo wakweli, hawajawasilisha taarifa yao ya mapato na matumizi  kwa Msajili wa Vyama kwa miaka minne, na Zitto anasema kuwa yuko tayari kunyongwa kwa maslahi ya fedha za umma na bado amekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema ambacho kwa mujibu wa yeye mwenyewe, ni miongoni mwa vyama ambavyo havijawasilisha mapato na matumizi ya fedha za umma kwa miaka minne, sasa anamaanisha nini?

Kama yeye ndiye Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, zaidi ya miaka minne hakuona ubaya chama kutowasilisha mapato na matumizi ya fedha ya umma, anawezaje kuja kwenye kamati ya PAC akajipambanua kwamba yuko tayari kufa kwa ajili ya fedha hizo, kweli inaingia akilini?

Nadhani baada ya kubaini hili angepaswa aachie nafasi yake ndani ya chama kwanza ndiyo aanze kulipigia kelele hili, bila hivyo wenye akili timamu watamuona mbinafsi na mtu mwenye kutafuta ushawishi binafsi na hakuna ukweli wa dhamira yake.

Pia wengi wanaona Zitto anatumia nafasi yake kama Mwenyekiti wa Kamati ya PAC kwa ubinafsi zaidi na si kama kamati.

Kwa mfano, anaposema yuko tayari kunyongwa kwa maslahi ya umma anamaanisha kamati ina shingo?

Tunavyojua kamati haiwezi kunyongwa na hakuna anayeweza kumshutumu yeye binafsi kwa suala ambalo yeye ni msemaji tu. Mambo yote huamuliwa na kamati nzima ya PAC, sasa ni vizuri akalichukulia hili suala kama la kamati yeye kwanza kwa kauli na matendo.

Namaliza kwa kuhamishia mjadala kwa wasomaji wangu “Je, Zitto Zuberi Kabwe wa kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na yule Naibu Natibu Mkuu wa Chadema ni sawa, hasa kwenye usimamizi wa fedha za umma?

0713 246 764


1086 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!