• • Ni baada ya OPEC kugoma kuongeza uzalishaji

WASHINGTON, MAREKANI

Bei ya mafuta katika soko la dunia ilifikia dola 79 kwa pipa wiki iliyopita, kikiwa ni kiwango cha juu tangu mwaka 2014. 

Hali hiyo iliyoshitua nchi nyingi duniani ilitokana na hatua ya jumuiya ya wazalishaji mafuta duniani, OPEC, kukataa kuongeza uzalishaji licha ya mahitaji ya bidhaa hiyo kupanda katika miezi ya hivi karibuni.

Nchini Marekani, bei ya mafuta ghafi iliongezeka kwa asilimia 1.4 na kufikia dola 78.93 kwa pipa. Kwa sehemu kubwa siku hiyo bei ya mafuta ilikuwa juu ya dola 79 kwa pipa, kiwango ambacho kilikuwa hakijawahi kushuhudiwa tangu Novemba 10, 2014. 

Kwa ujumla, bei ya mafuta mwaka huu imepanda kwa asilimia 63 na kusababisha mfumuko wa bei katika uchumi wa dunia.

Kupanda huko kwa bei katika soko la dunia pia kumeongeza bei ya rejareja katika vituo vya mafuta nchini Marekani na kwingineko.

OPEC imegoma kuongeza uzalishaji licha ya bei kuongezeka. 

Kundi hilo linaloongozwa na Saudi Arabia limesisitiza kuwa litaongeza uzalishaji kwa mapipa 400,000 kwa siku mwezi ujao na si sasa hivi.

Uamuzi huo wa OPEC uliwasukuma wafanyabiashara wengi wakubwa wa mafuta kununua bidhaa hiyo kwa wingi ili kuihifadhi kwa sababu wanaamini kutakuwa na uhaba katika miezi ya Novemba na Desemba.

Kwa miezi kadhaa sasa maofisa wa Ikulu ya Marekani wamekuwa wakiihimiza OPEC kuongeza uzalishaji kwani janga la corona lililosababisha kupunguza uzalishaji limeanza kudhibitiwa.

Uongozi wa Rais Joe Baden wa Marekai umeonyesha wasiwasi wake kuwa kupanda kwa bei ya mafuta duniani kutapunguza kasi ya ufufuaji wa uchumi uliodidimia kutokana na COVID-19.

“Tutaendelea kutumia kila silaha iliyo chini yetu, hata kama si wanachama wa OPEC kuhakikisha kuwa bei za mafuta zinakuwa chini kwa ajili ya umma wa Marekani,” amesema Msemaji wa Ikulu, Jen Psaki.

Psaki alibainisha kuwa kuna hatua kadhaa zimechukuliwa na serikali, ikiwamo kufufua viwanda vya kuzalisha na kusafisha mafuta vilivyobomolewa na kimbunga Ida, kutoa mafuta kutoka katika hifadhi ya taifa na serikali kudhibiti bei ya mafuta katika soko.

801 Total Views 8 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!