Benki ya NMB imeanza kutoa mikopo ya pikipiki zinazotumia magurudumu matatu (bajaj) kwa wajasiriamali nchini.

Katika utoaji mikopo hiyo, NMB itashirikiana na Kampuni za Fair Deal Auto Private Ltd, Car & General Limited Ltd na TV’S King zinazosambaza bajaj. Mikopo hiyo yenye masharti nafuu, inatolewa kwa mteja anayetimiza vigezo vilivyowekwa ili kupata mkopo huo.

Mteja mwenye nia ya kupata mkopo huu, atatakiwa kuwa na uwezo wa kulipia asilimia 30 ya gharama au bei ya bajaj nchini.


Mikopo ya pikipiki hizo inatolewa kwa muda wa miezi 24, ambapo kwa kipindi hicho mteja ataendelea kurejesha makato yake kila mwezi kwa kulipa taratibu kulingana na makubaliano yatakayofanyika baina ya mteja na NMB.

 

Mikopo hiyo pia itawekewa bima inayomletea unafuu mkopaji, endapo atapata matatizo ya kiafya yanayoweza kumfanya asiwe na uwezo wa kufanya shughuli zake au kufariki.

 

Bima hiyo itachukua jukumu la kumalizia deni la mkopo huo na mteja ataendelea kumiliki pikipiki husika kama kawaida.

 

Mikopo hiyo kwa sasa inatolewa katika matawi tisa ya NMB yaliyopo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mikakati ya benki hii kuwezesha huduma hii kuwafikia wateja wake katika mikoa mingine kwa siku za usoni. Matawi ya NMB ambayo wateja wanaweza kuyatembelea kwa sasa ni Temeke, Tegeta, Ilala, Airport, Mlimani City, Mwenge, Mbezi, Magomeni na Msasani.

 

Hivyo wateja wa NMB wanaweza kutimiza ndoto yao ya kumiliki bajaj kwa kutumia mikopo hii.

 

Benki ya NMB inatoa wito kwa wateja kutumia fursa ya kupata mikopo hii kwa unafuu zaidi.


By Jamhuri