Leo kutenda ubaya ni sifa, na kutenda wema ni chukizo, leo kutenda dhambi ni sifa na kuishi kitakatifu ni chukizo katika jamii, leo katika jamii karibu yote mmomonyoko wa maadili ni kitendawili kisicho na jibu, leo karibu jamii yote ya kibinadamu inaunga mkono nguvu ya ubaya.

 

Ninajiuliza inawezekanaje baba wa miaka 55 na kuendelea kuitwa ‘baby’ na binti wa miaka 23 halafu baba huyo akatabasamu na kucheka?

 

Je, inawezekanaje mama wa miaka 45 kuitwa beby na kijana wa miaka 23 halafu mama huyo akatabasamu na kucheka?  haaaaaaa, unaweza kucheka lakini ni kwa sababu nguvu ya ubaya inafurahiwa na wengi na inashabikiwa na wengi.

 

Leo wanaoshabikia sheria ya utoaji mimba ipitishwe ni wengi, kuliko wanaoipinga. Leo kuna wanatamani ndoa za jinsi moja [Homosexuality] zihalalishwe.

 

Mwelekeo wa ukengeufu unazidi kuchukua sura mpya miongoni mwa mwanadamu kila kukicha.  Mataifa makubwa duniani yanazidi kuyanyonya rasilimalin za mataifa madogo, hali ambayo inayafanya mataifa madogo kuendelea kuwa tegemezi kwa mataifa yalioendelea.

 

Matajiri wanazidi kuwatumia masikini kama vibaraka, hali ambayo inaonesha dhahiri kwamba kuna matabaka katika jamii, katika taasisi, na katika mataifa.

 

Mwanafalsafa kutoka Ujerumani, Albert Einstein aliandika hivi,  “Ulimwenguni pamekuwa mahali pa hatari sana kuishi binadamu, hali hii haitokani na wale wanaoufanya uovu, bali inatokana na wale wanaouangalia uovu ukifanyika na hawachukui hatua yoyote’’.

 

Na mwalimu wa kanisa katoliki Origen alipata kuandika hivi, “Palipo na dhambi ndipo ulipo utengano, ndipo ulipo uzushi, ndipo yalipo mabishano’’.

Leo kuna baadhi ya wazazi wanashiriki kuvunja ndoa za watoto wao, kuna baadhi ya wazazi wanashiriki kutoa mimba na huku wako kwenye ndoa.

 

Katika jamii yetu sasa kuna ukosefu wa haki, tofouti za kiuchumi na kijamii zinazopita kiasi, dalili zote hizi zinaonesha dhahiri kabisa kwamba hali ya maisha  ya mwanadamu ni tete.

 

Dunia inapita katika kipindi cha mabadiliko makubwa sana.  Kasi ambayo dunia inaenda nayo ni kubwa sana kuliko tunavyoweza kufikiri na kasi hii inagusa nyanja zote zinazomhusu mwanadamu.

 

Mambo yanayotokea humu ulimwenguni inabidi tuyafikirie sana. Kila mahali tunaona ghasia na misukosuko. Bahari, maziwa na mito kuchafuliwa, miti inakatwa, na watu maelfu kwa maelfu wanazikimbia nchi zao ili kuondokana na hatari za maafa na baa la njaa.

 

Tunahitaji kujenga jamii adilifu, yenye hofu ya Mungu, jamii yenye mshikamano, jamii yenye sauti moja.  Ama hakika jamii yetu inahitaji mabadiliko, familia zetu zinahitaji mabadiliko,  tunahitaji mabadiliko ya kiroho na kimwili.

By Jamhuri