Biashara ya ngozi yaporomoka

Sekta ya ngozi imeendelea kuwa njia panda baada ya wadau wa ngozi kulalamika kuhusu kuharibika kwa ngozi na kukosa wateja, huku Chama cha Kusindika Ngozi nchini kikikabiliwa na uhaba wa ngozi; jambo ambalo linahatarisha uhai wa viwanda.
JAMHURI limezungumza na wafanyabiashara wa ngozi huku kila mmoja akiwa na sintofahamu kuhusu biashara hiyo na baadhi yao wakiwa katika hali mbaya kiuchumi, baada ya kuporomoka kwa bei ya ngozi kutoka sh 1,500 kwa kilo hadi kufikia sh 200 katika kipindi cha miaka miwili.

Hata hivyo, chama hicho kimeeleza kuwa kuna ukosefu wa ngozi unaofikia zaidi ya asilimia 80, na ngozi inayopatikana ni chini ya asilimia 20 kutokana viwanda vilivyopo kuwa na uwezo mdogo wa kusindika ngozi.
Viwanda hivyo vina uwezo wa kusindika ngozi ya ng’ombe vipande (pieces) 4,734,000 na mbuzi 12,820,000 kwa mwaka.
Imebainika kuwa hali hiyo imetokana na mgongano wa kimaslahi kati ya wanunuzi na wenye viwandani, hasa katika upande wa bei ya ngozi.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amelieleza JAMHURI kuwa sekta ya ngozi ina matatizo.

Mwijage amesema kuwa kutokana na hali ilivyo, atamwelekeza Mkurugenzi wa Viwanda aonane na Mkurugenzi wa Mifugo ili wafuatilie suala hilo kwa ukaribu na kulipatia majibu.
“Katika hilo wakurugenzi wangu watafuatilia ili kuelewa tatizo ni nini? Kwani kuna uwezekano kukawa na siri ndani yake ambayo hatuijui.
Tunapaswa kufahamu kwa nini wadau wanashindwa kuwauzia ngozi watu wa viwandani au kutokana na bei wanayopangiwa kuwa ndogo? Suala hili limejitokeza na tutawaita ili tuzungumze nao,” amesema Mwijage.
Hata hivyo, ameeleza kuwa taarifa ambazo amezipata hivi karibuni kutoka kwa wadau wa ngozi ni kuhusu ukosefu wa wateja katika biashara hiyo.

Amesema kuwa taarifa hiyo inaeleza kuhusu kiasi cha ngozi ambacho kimeharibika kwa kila mkoa baada ya kukosekana kwa wanunuzi.
“Kama kuna taarifa kuwa viwanda vinakosa ngozi za kutosha za kusindika, huku wadau wanalalamikia kukosekana kwa wanunuzi hilo ni tatizo,” amesema.
Katibu Msaidizi wa Chama cha Wanunuzi wa Ngozi Tanzania (WANGOTA), Lucas Lissu, amesema kuwa biashara ya ngozi kwa sasa imeendelea kuwa mbaya baada kushuka kwa bei kwa kiwango kikubwa, jambo ambalo limesababisha wawe katika hali ngumu kiuchumi.

“Ukiangalia katika maghala mengi ya kuhifadhia ngozi kuna mizigo ya ngozi ambayo ipo zaidi ya miaka miwili, huku wengine wakiwa na tani kati ya 30 na 40 zikiwa zimeharibika na ukizingati baadhi yao walichukua mikopo kwa ajili ya biashara hiyo,” amesema Lissu.
Amesema kuwa kutokana na hali ya kuharibika kwa ngozi, tayari wengine wameanza kuzikimbia kutokana kuharibika baada ya kukaa muda mrefu bila kupata wanunuzi.
Lissu amefafanua kuwa hali hiyo imetokana na kupanda kwa kodi kwa wanunuzi wa ngozi, kushuka katika soko la dunia, ubora wa ngozi na kusababisha na kushindwa kumudu gharama za uendeshaji.
Baada ya kupanda kwa kodi, Kampuni ambazo zilikuwa zinanunua ngozi zimesitisha kutokana na gharama kubwa wanazozitumia.
“Baada ya kufanya vikao kadha na wateja wameeleza chanzo cha kuporomoka kwa biashara hiyo ni kupanda kwa kodi, hivyo wameiomba Serikali ipunguze kodi ili waendelee kufanya usafirishaji ukiangalia makusanyo ya ngozi ni makubwa kuliko wanunuzi,” amesema Lissu.

Amebainisha kuwa hivi karibuni walikuwa na kikao ambacho kilifanyika mjini Dodoma ambapo walipeleka malalamiko yao kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, pamoja na wadau wengine kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Amesema kuwa miongoni mwa mambo ambayo yamejadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na kuangalia jinsi ya kupata ahueni katika kodi ili kutoa nafasi kwa wawekezaji kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika sekta ngozi.
“Bado hatujapata majibu sahihi mpaka sasa ila tunasubiri mwezi Juni mwaka huu katika bajeti ya Wizara ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambapo kuna uwezekano wa kupata masamaha wa kodi katika sekta ya ngozi” amesema Lissu.
Amesema kuwa imefika wakati Serikali inatakiwa kuwa na viwanda vyake ili inapotokea soko la dunia inaposhuka katika biashara ya ngozi waweze kusindika na kuzihifadhi kwa ajili ya kusubiri kupanda bei.
“Umakini unaitajika kwa Serikali ili kuhakikisha wanapiga hatua katika sekta ya ngozi ambapo kwa sasa imeonekana kuwa na fursa finyu licha ya kuwa na idadi kubwa ya mifugo,” amesema Lissu.
Akifanya mahojiano JAMHURI, Mwenyekiti wa Chama Cha Kusindika Ngozi Tanzania, Onorato Garavaglia, amesema kuwa Serikali inatakiwa kuwa makini katika kuhakikisha inadhibiti magendo ambayo yanaendelea kufanyika na kusababisha wafanyabiashara kukosa ngozi.

Amesema kuwa kukosekana kwa wateja wa biashara ya ngozi haina maana ngozi kwa sasa imekosa wateja, ila inatokana na kuwapo kwa wajanja wachache ambao wanataka kujinufaisha kwa maslahi yao binafsi.
Kwa sasa wananunua ngozi kwa kilo sh 400, lakini kuna wanunuzi wanawauzia bei kubwa na ukizingatia wao wanalipa kodi na kufuata taratibu nyingine zote katika kufanya biashara.
“Kuwapo kwa walanguzi tunashindwa kwenda moja kwa moja sehemu husika kununua ngozi kwa wafanyabiashara wadogo ambao wameonekana kunyonywa na walanguzi,” amesema Garavaglia.
Garavaglia amesema kuwa kuna viwanda tisa vya kusindika ngozi ambavyo vyote vinahitaji ngozi ‘material’ kwa ajili ya kusindika na ukiangalia bado kuna uhitaji wa ngozi katika viwanda.
Amesema kuwa viwanda hivyo vina uwezo wa kusindika ngozi ya ng’ombe (pieces) 4,734,000 kwa mwaka, huku ngozi ya mbuzi 12,820,000.

Amefafanua kuwa kwa sasa viwanda vya kusindika ngozi vina upungufu mkubwa wa ngozi kwa asilimia 80 na kusababisha baadhi ya viwanda kupunguza wafanyakazi kutokana na ukosefu wa ngozi.
Garavaglia amesema kuwa wanatumia asilimia 20 ya mahitaji ya ngozi kutokana na ukosefu wa ngozi za kutosha kwa ajili kuzindika katika viwanda.
Ameeleza kuwa miongoni mwa viwanda vinavyosindika ngozi hapa nchini ni pamoja Lake Trading Co. Ltd Kibaha, Himo Tanner & Planters Ltd Moshi, ACE Leather (T) Ltd Morogoro pamoja na Meru Tanneries Ltd kilichopo mkoani Arusha.
Garavaglia ambaye ni Mkurugenzi wa Kiwanda cha ACE Leather (T) Ltd, amebainisha kuwa zipo sababu kadhaa ambazo zimekuwa kikwazo kwa wafanyabiashara wa ngozi hasa walanguzi ambao wamekuwa chanzo cha kuiharibu sekta hiyo.
“Kuwapo kwa watu hao viwanda tumekuwa katika wakati mgumu baada ya kuuziwa ngozi kwa bei ya juu na kusababisha tuwe katika mazingira sio rafiki kiuchumi,” amesema Garavaglia.

Ameeleza kuwa mambo mengine ambayo yanaendelea ni propaganda ambayo yanazungumza na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakisafirisha ngozi kwa njia ambazo sio rasmi.
Ukiangalia kwa undani unaweza kubaini walanguzi hao wanasafirisha ngozi kwenda nje ya nchi bila kufuata utaratibu maalumu, kwani wapo wengi ambao wamekuwa wakikamatwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kukwepa kodi.
“TRA baada ya kuwakamata wamekuwa wakiwatoza faini na kuwaachia, kisha wakiendelea na shughuli zao kama kawaida ya kusafirisha ngozi,” amesema Garavaglia.
Amesema kuwa ili Tanzania ifanikiwe katika sekta ya viwanda, inapaswa kuangalia suala ilo kwa umakini hasa katika upande wa kodi ambapo kwa sasa wanalazimika kulipa asilimia 10.

Hata hivyo, ameeleza kuwa kuwa Serikali inapaswa kuzuia ngozi kwenda nje ya nchi (Ban export of raw material) kama ilivyokuwa nchi ya Uganda pamoja Zambia, ili kuwasaidia wawekezaji kupata ngozi kwa wingi.
Akizungumzia kushuku kwa bei ya ngozi Garavaglia amesema bei ya ngozi inategemea hali ya soko la dunia inavyokwenda na kupangwa kwa bei kwa kila nchi.
Makamu Mwenyeki wa Wafanyabiashara ya Mifugo na Mazao (UWAMIVI) katika Machinjio ya Vigunguti, Anatoli Lubeli, amesema kuwa katika Machinjio ya Vingunguti mwaka 2015 walikuwa wanauza kilo moja ya ngozi kuanzia 1,000 hadi 1,200; jambo ambalo lilikuwa ahueni katika kuendesha maisha yao.

Amesema kuwa kwa sasa hali ya biashara ya ngozi ni tete kwa wafanyabiashara kwa sababu ngozi imeonekana haina thamani kutokana na kushuka bei.
Ni vyema Serikali ikaangalia upya masuala ya kodi kwa wewekezaji ambao wamewekeza katika sekta ya ngozi.
“Ni vyema suala hili likaangaliwa kwa mapana yake kwa sababu kadri muda unavyozidi kwenda hali inakuwa ngumu, watu wa viwandani sasa hawanunui ngozi kutokana na ukubwa wa kodi wanazotozwa,” amesema Lubeli.
Anasema kuwa kuwa bei ya ngozi ya mbuzi kwa sasa ndiyo inaonekana kuwa na thamani kiasi chake kutokana na bei iliyopo ya sasa ni sh 2,500 hadi 3,000; kitu ambacho kinaleta ahuweni katika mazingira ya kibiashara.

Lubeli amesema kuwa ni vyema Serikali ikawa na mipango makini katika sekta ya ngozi kwa kuweka utaratibu wa kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa ngozi, hasa katika kutoa elimu ya kuongeza thamani ngozi ili waweze kuuza bei ambayo ni rafiki.
Amesema kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili kwa sasa ni ukosefu wa elimu ya kuchuna ngozi, kwani elimu hiyo inaweza kuleta matunda mazuri katika sekta ya ngozi.
Katibu wa Umoja wa Chama cha Wafanyabiashara katika Machinjio ya Ukonga Mazizini (UWANJUA), Michael Timbo, amesema kuwa hali ya bei ya ngozi kwasasa katika soko siyo nzuri.

Amesema kuwa mwaka 2015 walikuwa wanauza kilo moja ya ngozi sh 1,500 baada ya kuingia Rais mpya hali ya soko ilibadilika na kufika sh 100 hadi sh 70 kwa kilo.
Timbo amesema kuwa kutokana ugumu wa soko baadhi ya wafanyabiashara wameacha kufanya biashara hiyo kutokana na hasara wanayopata.
“Tatizo kubwa lililopo asilimia kubwa ya wafanyabiashara hatujui bei ya ngozi kwa sababu wateja wetu ni walanguzi ambao wananunua ngozi na kwenda kuwauzia watu wa kiwandani na hatuji nao wanakwenda kuuza shilingi ngapi” amesema Timbo.

Ameeleza kuwa biashara hiyo ilikuwa tegemeo kwa wafanyabiashara wa ngozi katika soko hilo, ambapo kwa sasa hali imekuwa tofauti na kusababisha asilimia kubwa kukata tamaa na baadhi yao kuachana kabisa na biashara hiyo.
“Kuna mambo mengi ambayo yanaendelea sio mazuri katika soko hili, tumejitaidi kufuatilia lakini ushirikiano umekuwa mdogo sana kutokana figisufigisu ambazo zimekuwa zikiendelea,” amesema Timo.
Amesema kuwa mambo ambayo yanaendelea hapa ni sawa na Vingunguti, kwani kuna baadhi ya watu wanajaribu kuvuruga umoja wa wafanyabiashara ili waendelee kufanya mambo yao ambayo sio rafiki kwa umma.
Serikali inatakiwa kutafuta ufumbuzi ili tupige hatua katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo na kuangalia uwezekano wa kutengeza mazingira mazuri.