Kabla ya kuendelea, niwapongeze viongozi wote wakuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Nampongeza mno Waziri Anna Tibaijuka, na Katibu Mkuu Patrick Rutabanzibwa (PR).

Nawapongeza kwa ujasiri wao. Hivi karibuni wamechukua uamuzi mgumu wa kumweka pembeni mmoja wa viongozi wabovu kabisa wa Mipango Miji. Huyu amevuruga mambo mengi mno. Alikwenda Kwembe akaongoza upokaji ardhi ya wananchi. Leo kawekwa pembeni, huu ni ushujaa wa hali ya juu sana uliofanywa na uongozi wa Wizara. Hongereni sana .

 

Katika Hotuba ya Bajeti ya Mwaka 2011/2012, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwa namna pekee ya uzalendo, ilipendekeza kwa Serikali haja ya kuifanyia marekebisho Sheria ya Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999.

 

Sheria hiyo inatoa mamlaka kwa Halmashauri ya Kijiji kusimamia  ardhi yote ya kijiji, na imepewa mamlaka ya kugawa ardhi isiyozidi ekari 50 baada ya kuruhusiwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji.

 

Mapendekezo ya Upinzani yalitokana na ukweli kwamba wananchi pamoja na uongozi wa vijiji vingi hawana ufahamu mpana wa sheria. Tunaweza kuwa na sababu nyingine za kuwapuuza wapinzani, lakini si kwa hoja za msingi kama hizi.

 

Aidha, Mabaraza ya Ardhi ya Kata yamekuwa chanzo kingine cha migogoro mingi sana katika Taifa letu. Mabaraza haya ni vijiwe vya mapato vya baadhi ya watendaji wabovu. Haya nayo yanapaswa kufumuliwa kisheria.

 

Matajiri wenye ukwasi wamekuwa wakitumia fursa hii ya kisheria kuwarubuni viongozi wa vijiji, na hatimaye kutwaa maeneo ya vijiji kwa watu wachache wenye ukwasi na ushawishi wa kisiasa.

 

Matokeo ya mwanya huu yamewafanya wanavijiji wengi sasa wajikute kwenye migogoro, ama na wawekezaji, wafugaji kwa wakulima au wenyewe kwa wenyewe kutokana na uhaba wa ardhi.

 

Hali imekuwa mbaya zaidi baada ya wageni wengi kujipenyeza na kujitwali ardhi kinyemela, ilhali sheria ikizuia kabisa suala hilo . Ardhi imetolewa kwa matajiri na watu wasio raia kwa nguvu, ushawishi wa fedha na ubabe wa viongozi wa vijiji na wilaya. Rushwa imekuwa mtego mkubwa wa kuwashawishi viongozi wa vijiji na wanavijiji.

 

Manabii wa utwaaji ardhi wanatumia zawadi za kijinga kuwapumbaza wananchi na viongozi wa vijiji ili wajitwalie ardhi kubwa. Haishangazi kuona baaadhi ya viongozi wakihongwa pikipiki na kuwa radhi kutoa mamia, kama si maelfu ya ekari za ardhi kwa mabwanyenye hawa.

 

Utwaaji huu wa ardhi ni mbali na ule unaofanywa na wawekezaji matapeli walioingia nchini kwa kibwagizo cha kuanzisha kilimo cha mibono.

 

Utwaaji huu wa ardhi ni mbali kabisa na ule uliofanywa na mabepari akina Chavda. Hawa walijitwalia maelfu kwa maelfu ya ekari kwenye mashamba ya mkonge, wakazitumia kupata mabilioni ya shilingi kama mikopo na kisha wakayatelekeza mashamba hayo.

 

Ndugu zangu, kasi ya utwaaji ardhi Tanzania ni kubwa mno. Hali hii inaendelea kutokea huku tukishuhudia mapigano ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji.

 

Chanzo kikuu kikiwa ni uhaba wa ardhi nzuri kwa malisho na kilimo, na pia vyanzo vya maji.

 

Serikali inatambua na Watanzania wengi wanatambua pia kwamba majirani zetu wanamiminika nchini kujitwalia ardhi.

 

Kwao ardhi yote wameshagawana. Katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni Tanzania pekee iliyobaki na ardhi nzuri inayomezewa mate. Wapo raia wa kigeni walioamua kuukana uraia wao, wakawaoa dada na mama zetu kwa nia tu ya kupata ardhi. Hii ni hatari kubwa.

 

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1958 wakati Tanganyika ikiwa haijapata Uhuru, aliona hatari hii ya kutapanya au kuuza ardhi.

 

Mwalimu alisema, “Katika nchi kama yetu ambayo Waafrika ni maskini na wageni ni matajiri, kuna uwezekano mkubwa kwamba Mwafrika akiruhusiwa kuiuza ardhi, katika miaka themanini au miaka mia ijayo, ardhi yote ya Tanganyika itamilikiwa na matajiri wageni, na wenyeji watakuwa watwana. Lakini hata kama wageni wasingekuwa matajiri, litaibuka tabaka la Watanganyika matajiri wajanja. Tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu, katika muda mchache, kutakuwa na kundi dogo la Waafrika wakiwa na ardhi, na walio wengi watakuwa watwana” – Mwalimu Nyerere, 1958.

 

Miaka 55 baada ya kauli ya Mwalimu, ukweli huo unafutwa kwa hoja gani? Mweledi gani asiyejua athari za wazalendo kukosa ardhi? Je, si kweli kwamba vita nyingi katika Bara la Afrika na kwingineko duniani, zimesababishwa na ukosefu wa ardhi? Tanzania ya leo ambayo watu wengi tu masikini, bila ardhi tutakuwa na maisha ya aina gani?

 

Pamoja na tofauti zetu za kiitikadi, kilio cha wapinzani kinabeba uhalisia wa kilio cha Watanzania wengi. Sheria ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999 ina sababu zote za kubadilishwa. Suala la ardhi halipaswi kuwa la kiitikadi. Ni ukweli ulio wazi kwamba katika vijiji vingi, wananchi ni mbumbumbu wa sheria. Hawa, pamoja na watendaji kadhaa wahuni ndani ya Halmashauri na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, wamekuwa chanzo kikuu cha balaa hili.

 

Wanasiasa hawawezi kukwepa lawama katika hili. Tumeshuhudia migogoro inayosababishwa na wanasiasa na NGOs kama kule Loliondo ambao wanazuia Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi. Hatua hii imeendeleza migogoro kwa wakulima na wafugaji kupigana mara kadhaa. Mfano mzuri ni wa Wasonjo na Wamasai. Vurugu kama hizo tumezishuhudia katika Mikoa ya Morogoro na Pwani. Hakuna matumizi bora ya ardhi.

 

Ndugu zangu, jambo jingine tunalopaswa kuliutazama kama Taifa, ni la kuwa na kiasi. Ukitazama kando ya barabara kuu zote nchini, ukiacha maeneo ya hifadhi, zimetwaliwa. Matajiri wamejilimbikizia maelfu ya ekari, huku wananchi wengi wakikosa maeneo ya malisho na kilimo.

 

Hatari hiyo imebisha hodi Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani. Mwaka jana, nilizungumza na Mkuu wa Wilaya hiyo, Ahmed Kipozi, akaeleza hofu yake juu ya uuzwaji ardhi. Akawataka wananchi wawe makini katika uuzaji ardhi kutokana na wimbi la Watanzania na raia wa kigeni wanaojitwalia ardhi kubwa wilayani humo.

 

Akakiri wazi kwamba kasi ya wananchi wakazi wa wilaya hiyo kuuza ardhi imefikia kiwango cha kutisha.

 

Ushauri wake ukawa kwamba kama mwananchi ana ekari mia moja, basi auze na kubakiza japo ishiriki au thelathini kwa ajili yake na kwa kizazi chake.

 

Alizitaka taasisi za fedha ziende Bagamoyo zitoe semina za kweli kweli ili wananchi wajue namba ya kuitumia ardhi yao , vinginevyo watauza ardhi yote na kuwaacha wao na vizazi vyao wakiwa masikini.

 

Maneno haya ya Kipozi yawezekana kabisa yakawa ndiyo maneno ya wakuu wa wilaya wengi. Ardhi inahodhiwa kwa kasi ya kustaajabisha. Ardhi inahodhiwa na wachache, ilhali ukubwa wa ardhi ukiendelea kubaki ule ule. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba ndani ya kipindi kifupi, ardhi itakuwa imetwaliwa na wachache, ilhali kundi kubwa la Watanzania likiwa halina ardhi. Ukichanganya ukosefu wa ardhi pamoja na ukosefu wa elimu, ni wazi kwamba mwananchi mnyonge atakuwa amepoteza uhalali wa kufaidi maisha katika Taifa lake. Tukifika hapo, kitakachofuata ni mapigano ya wanyonge kudai kwa nguvu ardhi kutoka kwa mabwanyenye wachache. Nchi itaingia kwenye migogoro itakayohitaji gharama kubwa kuitatua.

 

Niwaombe viongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wawe radhi kwa lolote alimradi tu walinde ardhi ya Watanzania wanyonge.

 

ahakikishe ulipaji fidia unakuwa wa haki, na gharama za upatikanaji viwanja kwa watu wa kipato cha chini ziwe ndogo.

 

Mwisho kabisa, nawahusia vijana walioamua kuendesha bodaboda. Wasiweke akili zote kwenye pikipiki wakati huko vijijini matajiri na wawekezaji uchwara wakijitwalia ardhi. Siku wakitambua kuwa pikipiki hizi si lolote wala chochote kwa maisha yao , watakuta ardhi yote imeshatwaliwa. Utajiri wa kweli upo kwenye ardhi, na si kwenye hizi bodaboda.

 

Vijana wasitelekeze wala kuuza ardhi kupata mtaji wa kununua pikipiki kwa nadharia kwamba biashara ya bodaboda inaweza kuboresha maisha yao. Ardhi ndiyo nguzo ya maendeleo yote ya kweli.

 

1168 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!