BiasharaNilivutiwa sana na mchango wa msomaji mmoja kutoka Arusha aliyeniandikia baruapepe ifuatayo, “Bw. Sanga nakupongeza sana kwa makala zako. Unaandika ujasiriamali na mambo ya kujitambua in unique style kiasi kwamba kila ninaposoma makala zako napata ladha na impact kubwa mno. Kwenye makala yako ya leo umeeleza vizuri mno kuhusu imani za fedha”


“Loo! Makala hii imenisaidia na kuniokoa mno kwa sababu nimekuwa na kawaida ya kushiriki gossiping kuhusu wenye fedha. Mfano hili la kuamini kuwa kuna makabila yanafanikiwa kwa sababu ya wizi ama ushirikina nimekuwa ninaamini pasipo kujua kuwa ninaathiriwa na imani hizo”.
“Hata hivyo Bw. Sanga ninaomba unisaidie nawezaje kuzalisha fedha za kunitosha? Kwa sababu mimi ni mwajiriwa lakini kadiri siku zinavyoenda ninaona majukumu yanaongezeka na mshahara naona hautatui mahitaji yangu vizuri, maisha ni magumu, nikitafiti naona biashara karibia zote zimeshafanyika, Je, nitafanya kitu gani ama namna gani ili niweze kuzalisha fedha? Narudia tena kukupongeza na ninaamini utanisaidia katika hili” Mwisho wa kunukuu.


Katika makala hii leo ninajibu swali la msomaji huyu aliyeniuliza, “Nawezaje kuzalisha fedha za kunitosha?” Hata hivyo kabla sijaeleza namna gani mtu unaweza kuzalisha fedha za kukutosha, ninapenda kueleza kidogo kuhusu dukuduku walilokuwa nalo baadhi ya wasomaji kuwa fedha siyo nzuri kwa sababu zinaharibu tabia za watu.


Kimsingi, fedha imebeba chembechembe nyingi za kisaikolojia zenye uwezo mkubwa wa kuamsha tabia za mtu hata zile ambazo hazijapata kuonekana. Mtu mchoyo akipata fedha uchoyo wake unaongezeka na unakuwa dhahiri. Mtu mwema na mtoaji akipata fedha wema wake huongezeka na ataonekana akitoa zaidi na zaidi.


Kwa jinsi hii tunaona kuwa kimsingi fedha haibadilishi wala kutengeneza tabia ya mtu isipokuwa fedha hudhihirisha tabia na hulka aliyonayo mtu ambayo alishakuwa nayo hata kabla hajaipata fedha. Fedha naweza kuifananisha na mfumo wa mashine za sauti – ‘amplifier’.
Kwenye amplifier ukitoa sauti yako kama ni sauti mbaya ubaya huo utakuzwa na kama sauti yako ni nzuri basi uzuri wa sauti yako utakuzwa vile vile. Kwa kuwa fedha zina mfumo wa kukuza tabia, ni vema sana mtu akatumia muda na rasirimali maarifa kujenga tabia na hulka zake ili fedha inapokuja isilete mushkeli.


Na ninapotaja habari ya mtu kuwa na fedha isidhaniwe kuwa ninagusia fedha nyingi sana, la hasha. Watu tunatofautiana sana linapokuja suala la mitazamo na hulka zetu katika fedha. Wapo watu ambao akiwa na elfu kumi tu mfukoni lazima ujue kwa maana ataleta vurugu na maujiko kibao.
Mtu mwingine akiwa na hiyo shilingi elfu kumi mfukoni haoni kama ana fedha, isipokuwa anaweza hata kukueleza kuwa “sina fedha kabisa”. Kwa mwingine milioni moja si fedha wakati kwa mwingine milioni moja ni utajiri!
Kinachofanya mtu mmoja aone kuwa elfu kumi ni fedha na mwingine aone kama si fedha inatokana na mtazamo wanaokuwa nao watu hawa katika fedha. Mtazamo huu hauanzi pale mtu anapoishika hiyo elfu kumi, isipokuwa ni kuwa mtazamo wao ulishajengeka mapema kabla hata ya kushika hiyo fedha.


Baada ya kusema hayo, sasa nigeukie upande mwingine kulijibu swali la msomaji yule, la “Je, nawezaje kuzalisha fedha?” Kwa wale wenye kumbukumbu bila shaka wangali wanaikumbuka makala niliyopata kuiandika wiki chache zilizopita iliyokuwa na kichwa, “Tumeamua kuichuuza thamani ya fedha yetu”.


  Katika makala hiyo nilieleza kwa kina dhana na maana ya fedha, lakini pia nilisema fedha si mafanikio zikisimama peke yake; isipokuwa fedha ni matokeo ya mtu kufanikiwa. Fedha inatakiwa kumjia mtu baada ya kuzalisha thamani fulani katika uchumi. Hapa tunaangalia maeneo kadhaa zinakopatikana fedha.


Kunapotokea mdororo wa uchumi, mara nyingi mitaani huwa tunasema fedha zimepotea,  fedha hazionekani, kitu cha kujiuliza ni “Je, fedha zinapopotea ama kutoonekana zinakuwa zimepotelea wapi?” Ukweli ni kuwa fedha zote zilizopo duniani zinazunguka miongoni mwa watu. Idadi ya fedha huwa haipungui, ila kinachopungua ama kuongezeka ni thamani ya fedha.

>>ITAENDELEA

1953 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!