Mfanyabiashara bilionea Dk. Philemon Mollel, anayemiliki kampuni ya Monaban Trading and Farming Co. Limited, amepokwa kinu kilichokuwa mali ya Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC) jijini Arusha.

Pamoja na kunyang’anywa kinu hicho, Dk. Mollel ambaye ni kada na mfadhili wa Chama Cha Mapindizi (CCM), ametakiwa alipe Sh bilioni 16 za malimbikizo ya ada ya pango kwa muda wote aliokuwa na kinu hicho kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka huu.

Analalamika kuwa kufungwa kwa kinu hicho kumevuruga mambo, kwani amewekeza mali za shilingi zaidi ya bilioni 12 ambazo ni mikopo kutoka benki mbalimbali.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, John Maige, anasema Mollel alitakiwa alipe Sh milioni 79 kila mwezi tangu mwaka 2013, lakini hakufanya hivyo na badala yake amekuwa akilipa Sh milioni 10 kwa mwezi.

Kwa upande wake, Mollel anasema ananyang’anywa kinu hicho kwa hila za wabaya wake wa kisiasa na kiuchumi, na anamtaja kiongozi mmoja wa kisiasa mkoani Arusha kuwa yuko nyuma ya shinikizo hilo.

Anasema barua ya “kufukuzwa” alikabidhiwa Juni 6, mwaka huu kwa kile kilichoelezwa kuwa ni maelekezo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

“Waziri Mkuu alituita Dodoma akatusikiliza na kisha akasema angetuma timu kuchunguza suala hili. Nilijawa na matumaini kwa sababu niliamini timu ingepata ukweli wote na ingenitendea haki.

“Ajabu ni kwamba hao watu walikuja kweli, lakini hawakufanya uchunguzi wowote wa kina wala kupata maelezo yangu. Wakawa wanakuja ofisini na kuondoka, mwishowe wakaja na kunitaka nichague moja kati ya mambo mawili – nisaini nyaraka za kuachia kinu; au nisisaini na hivyo nifunguliwe kesi ya uhujumu uchumi. Nikasaini ili nisifunguliwe kesi hiyo mbaya na ya kuonewa. Nikawa najiuliza nimehujumu uchumi gani? Mbona kila kitu kipo wazi?” anahoji Mollel.

Mvutano ulivyokuwa

Dk. Mollel anasema Agosti 23, 2007 kupitia kampuni yake ya Monaban Trading and Farming Co. Ltd alikodishwa na

NMC kinu cha Arusha kwa mkataba wa miaka mitano.

Mkataba huo ulifanyiwa marekebisho kwa kusainiwa nyongeza ya

mkataba (addendum to the lease agreement) Aprili 10, 2008. Nyongeza ya mkataba huo iliruhusu Monaban kuwekeza dola milioni

2.684 za Marekani kwa ajili ya ukarabati wa kinu cha kusagisha ngano. Anasema fedha hizo zingerejeshwa kupitia tozo iliyopaswa kulipwa.

Kati ya Februari 2010 hadi Juni 2012, ofisi ya Shirika Hodhi la Rasilimali za Mashirika ya Umma (CHC), kwa kushirikiana Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo na Chakula, Ushirika na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serekali walijadiliana na kampuni ya Monaban kuhusu mustakabali wa mali za NMC Arusha.

“Msingi wa majadiliano uilikuwa kuangalia jinsi gani kampuni yangu ya Monaban ingeweza kushirikiana (Joint Venture) na chombo cha Serikali kilichokuwa kimeundwa, yaani Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko.

“Katika majadiliano kila upande ulikuwa na vipaumbele vyake. Kampuni yangu ya Monaban ilikuwa na kipaumbele cha kuomba

kuuziwa mali hizo kwa kuwa tulikuwa tumewekeza kiasi kikubwa cha fedha katika kukarabati kinu..Majadiliano hayakuhitimishwa kwa kuwa muafaka haukupatikana.

“Hata hivyo, wakati majadiliano yalivyokuwa yanaendelea, Serikali iliagiza vyombo vyake kufanya tathmini (Mthamini Mkuu wa Serikali) na kutoa ushauri wa kisheria (Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali) kwenye suala husika..Mthamini Mkuu wa Serikali alifanya thamini ya mali ili kujua thamani halisi ya uwekezaji uliofanywa na mkodishaji.

“Uthamini ulibaini kuwa hadi Aprili, 2012 kampuni ya Monaban ilikuwa imewekeza Sh bilioni 6.23. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali nayo ilitoa maoni yake serikalini. Kimsingi,Monaban Trading and Farming Co. Ltd. ilionesha nia ya kununua mali zote za NMC Arusha kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika na endapo Serikali ingeamua kuwapatia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kinu na mali za NMC Arusha na kuvunja mkataba wetu, basi, kwa upande wetu (Monaban) tungepata hasara ya biashara,” anasema.

Anasema Januari, 2013 kupitia kampuni ya uwakili ya

CRB Africa Legal aliwasilisha barua ya mchanganuo wa hesabu ya uwekezaji na hasara ambayo Monaban wangeipata endapo mkataba ungevunjwa.

“Agosti 31, 2013 timu ya maofisa kutoka serikalini wakiongozwa na ofisi ya CHC walifika kiwandani Arusha na kwa mshangao mkubwa walisema wamekuja kukabidhi mali husika kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kama walivyoelekezwa na Serikali. Mimi kama mfanyabiashara na mwekezaji mzalendo niliyekodishwa mali hizo na

niliyewekeza kiasi kikubwa cha fedha ambacho kimethaminiwa na kuthibitishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali niliona sijatendewa haki.

“Niliamua kwenda mahakamani kuomba zuio la Mahakama na kuitaka CHC isikabidhi mali za NMC Arusha kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko. Uongozi wa Mkoa wa Arusha uliagiza mara moja kusitishwa kwa makabidhiano hayo mpaka hatma ya kampuni yangu itakapokuwa imejulikana.

“Kwa kuwa CHC walivyokuwa Arusha kwenye kinu cha NMC walisema wamepewa maelekezo na Serikali kukabidhi mali za NMC Arusha kwa

Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Oktoba, 2013

nilienda kumuona Mtendaji Mkuu wa Shughuli za Serikali,

Waziri Mkuu wa wakati huo, Mheshimiwa Mizengo Pinda ili

kufahamu hatma ya uwekezaji ambao kampuni yangu imefanya pamoja na maombi ya kuuziwa mali husika za NMC Arusha.

“Nilielekezwa kwa kuwa suala langu linahusiana na uwekezaji basi niende kumuona waziri mwenye dhamana Uwekezaji na Uwezeshaji, Mheshimiwa Mary Nagu. Alinisikiliza na akaahidi kulifanyia uchunguzi na kupata ushauri wa kisheria

kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Novemba, 2013 nilienda tena na kupewa taarifa kwamba suala langu limeshughulikwa ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwa Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji na wadau wengine niendelee na uwekezaji na nisibugudhiwe hadi hapo Serikali itakapotoa maelekezo rasmi kuhusu maombi ya kuuziwa mali za NMC,” anasema.

Mollel anasema Desemba 10, 2013 CHC walimwandikia barua

kuhusu uamuzi huo wa Waziri Mkuu na uamuzi wa Bodi ya CHC ambako maelezo yalikuwa Monaban ikabidhiwe maghala yote kwa ajili ya kuhifadhi nafaka na iwe mkodishaji pekee hadi uamuzi wa Serikali juu ya kinu hicho utakapotolewa.

“Kwa kuwa Agosti 31, 2013 CHC ilisitisha ajira za wafanyakazi

22 wa NMC waliokuwa wamebaki; Septemba 6, 2013 CHC, ilikabidhi rasmi shughuli za uzalishaji kwa kampuni yangu ya Monaban Trading and Farming Co. Ltd. Mishahara ya waendesha mitambo, malipo ya vibarua na makuli, matengenezo ya

mitambo, malipo ya umeme, maji na kadhalika ambayo hapo awali yalikuwa chini ya usimamizi wa NMC, yakawa chini ya Monaban Trading and Farming Co. Ltd,” anasema.

Januari 12, 2014 CHC na Monaban walihakiki mali za NMC Arusha na kukabidhiana.

Juni 24, 2014, CHC waliingia makubaliano na kuitaka Monaban Trading and Farming  Co. Ltd  iwe inalipa Sh milioni 10 kwa mwezi, na kiasi hicho kiwe kinalipwa kila baada ya miezi mitatu. Kiasi hicho kilikuwa kwa ajili ya ukodishaji wa mali zote za NMC Arusha. Malipo hayo yalitakiwa yaanze Julai Mosi, 2014.

Anasema Monaban imelipa tozo hiyo katika kipindi chote cha mikataba ya upangishwaji. Uwekezaji unaodaiwa kufanywa hadi sasa ni: Ukarabati na kufunga mashine (Sh milioni 570.5; kuweka paving blocks, mfumo wa maji taka na ukuta (Sh milioni 365), mashine mpya kusindika sharbati, maziwa na maji (Sh milioni 210), mashine ya kukamua alizeti (Sh milioni 170), jenereta (Sh milioni 230), mashine ya kisasa ya

kuoka mikate (Sh bilioni 2.42), kuchimba kisima (Sh milioni 18.535), mashine ya kutengeneza mifuko (Euro milioni 2.2 – Euro moja ni wastani wa Sh 2,600) na malori 70 (semi trailer).

“Kampuni ina wafanyakazi  zaidi ya 200. mbili (kati yao, 120 wameajiriwa na 80 ni vibarua). Pindi mitambo yote itakapoanza kufanya kazi ajira zaidi ya 500 zitapatikana.

“Hadi sasa, zipo mali za NMC katika mikoa mbalimbali ambazo  zilishauzwa kwa kampuni tofauti. Tunaomba tufikiriwe uwekezaji tuliofanya na kisha tupewe haki ya kununua mali za NMC Arusha. Mali za NMC zilizouzwa na wanunuzi wake kwenye mabano ni Kurasini, Dar es Salaam (Mohamed Enterprises), Tanga na Moshi

(Mohamed Enterprises),  Shinyanga (Mohamed Enterprises), Iringa (Mohamed Enterprises), NMC Plot No. 10 Dar es Salaam (Mohamed Enterprises), Buguruni, Dar es Salaam (Said Salim Bahkresa), Babati, Manyara (Export Trading),  Arusha

(Export Trading), Tabora (Export Trading) na Mzizima (Mohamed Babu).

“Mali zote hizi zimeuzwa, mimi mzalendo wa nchi yangu naomba kuuziwa nakataliwa, lakini mbaya zaidi nanyang’anywa hata kile nilichowekeza humu kwa mujibu wa mkataba. Nina mikopo ya mabilioni katika mabenki mbalimbali, nimefungiwa sifanyi shughuli yoyote. Kila kitu kimesimama, nitafanyaje?” Analalamika Dk. Mollel.

Kauli ya Bodi ya Nafaka

Kaimu Mkurugenzi Mkuu ameliambia JAMHURI, “Kiwanda hakijafungwa, bali kimekabidhiwa kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko. Monaban alikuwa mpangaji tangu mwaka 2007. Mkataba uliishi kwa sababu ule wa 2007 ulikuwa ni wa miaka mitano tu. Baada ya hapo ukafanyika ujanja ujanja kwa sababu ule mkataba ulikuwa unasema kwamba yeye analeta mazao yake pale na NMC wanamsagia. Baadaye ukafanyiwa ujanja ujanja ukaonekana kwamba yeye anapangishwa.”

Idadi ya mikataba

“Siyo miwili, mpaka mitatu maana kuna deed of variation pia – ambayo ndiyo iliyokuwa inamwongezea muda. Wale aliokuwa anaingia nao mikataba hawakuwa sahihi maana walikuwa wanapingana na uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa mwaka 2008 ambao uliamua kwamba mali zote za NMC ambazo zilikuwa hazijauzwa zikabidhiwe Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko.

“Hizo Sh bilioni 16 anazodaiwa ni madai mbalimbali kwa sababu mwaka 2012 baada ya kufanya tathmini ikaonekana huyu bwana awe analipa Sh milioni 79 kwa mwezi kama pango, lakini yeye akafanya ujanja ujanja akawa analipa Sh milioni 10. Vilevile alikuwa hatakiwi kupangisha maana yeye ni mpangaji, lakini yeye akawa anapangisha watu wengine. Hiyo unfair gain imebidi tumdai kwa sababu amepata mali ambayo hakustahili.

“Tuna vinu vinne – Mwanza, Dodoma (tunajenga), Iringa na hiki cha Arusha. Vingine vilibinafsishwa. Baada ya kumuondoa huyu tutaendesha sisi wenyewe. Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imeundwa ni ya kibiashara. Pure Commercial, kazi yake ni kununua mazao, kuyaongezea thamani na kuyauza. Inakuwa kama soko la wakulima.”

Kwanini mkataba uishe 2012 lakini ameendelea hadi mwaka 2019?

Maige anasema, “Kulikuwa na jitihada mbalimbali za kutaka kumwondoa au kukaa naye mezani, lakini jitihada hazikufanikiwa kwa sababu yeye mwenyewe kutokuwa tayari. Kwa mfano sisi tulipoingia 2010, mwaka 2013 zilifanyika jitihada. Mali za NMC zilikuwa zinashikiliwa na Msajili wa Hazina baada ya kuwa shirika limebinafsishwa kwa hiyo yeye ndiye aliyekuwa anahusika kukabidhi hizo mali kwenye chombo kingine kipya kilichoanzishwa baada ya uamuzi wa Baraza la Mawaziri.

“Mali zote zilikabidhiwa, lakini za Arusha zilikwama kwa sababu ya uwepo wa huyo jamaa (Monaban) na yeye kutumia misuli yake kutotaka hicho kitu akiwa anang’ang’ana kwamba Serikali imuuzie. Hakutaka kusikiliza. Mwaka 2013 kulifanyika jaribio la kukabidhi lakini kukawapo vurugu, ikashindikana.

“Mwaka 2016 tena ikafanyika attempt ya kukabidhi, ikafanikiwa kidogo lakini hakutala Bodi ipeleke watu wake pale wawe wanafanya uhakiki wa vitu vinavyofanyika. Kwa mwaka amekuwa akipata wastani wa Sh bilioni 4 kwa kutunza mazao tu, lakini sisi anatulipa Sh milioni 120 pekee. Sisi tuko tayari kwa mazungumzo endapo tu ataacha tabia zake za vurugu.”

Kwa upande wake, Dk. Mollel anakanusha madai ya Maige kwa kusema yote anayofanyiwa yanasababishwa na njama za kumdhoofisha kisiasa, kiuchumi na kwamba amepata taarifa kuna watu walioandaliwa kupewa kinu hicho.

Anahoji, “Ushahidi wanao? Zitoke wapi hizo Sh bilioni 4? Si ningekuwa nimeshalipa madeni ya benki. Muulize [Maige], Iringa wanapata hiyo hela? Dodoma na Mwanza wanapata hiyo hela? Hawa …(neno kali) sana. Hela hiyo utapata wapi? Wanaongea tu.

“Hata siku moja hawajaniita tuzungumze. Waulize wakuonyeshe barua waliyoniletea kuniita tuzungumze. Wamefanya uharamia tu.

“Kuhusu ujanja ujanja anaosema, si wanayo nakala ya mikataba? Mimi sijafanya ujanja wowote. Mkataba ni wao walionipa, tena ni wao wameutengeneza – Serikali yenyewe. Mimi sijaugusa. Walionao ni kama ule ule wa kwangu. Hakuna mkataba mwingine…Mimi niko tayari kuwapa mwaka mzima halafu watafute hiyo hela wanayosema ninapata.

“Hao wanaongopa, utaghushi vipi mkataba ambao tayari nimeshausajili Moshi? Utaghushi vipi? Ili nifanyeje? Deed of Variation nimepewa na TIC [Kituo cha Uwekezaji Tanzania] na Deed of Handover tulipewa na Hazina ambayo inaonyesha kuna mikataba mitatu. Hayo mambo mengine ya uongo si ya kusikilizwa. Unaenda kuvamia kitu cha mtu kama jambazi. Wamenivamia kama mhalifu wakati ni Mtanzania mtiifu.

“Waziri Mkuu alisema anatuma tume ihakiki halafu irudishe majibu anatuita. Wao badala ya kusubiri kwa sababu walikuwa wanasukumwa na (mmoja wa viongozi waandamizi Mkoa wa Arusha) wakafanya walichofanya. Wakaanza kuandika barua za uongo. Kwenye timu ya Waziri Mkuu walikuwa wanasema tulikuwa tunadaiwa Sh bilioni 12, kidogo tena wakasema tunadaiwa Sh bilioni 16. Nashangaa hawa watu hizi takwimu wanapata wapi na mimi nina rekodi za ukaguzi.

“Kuhusu malipo ya Sh milioni 79 kila mwezi, nikawaambia kuwa mimi ndiye ninayefanya biashara na kujua kinachoingia. Makadirio ya kodi huwezi kufanya hivyo wewe kwa kuamua tu. Hata rais juzi amesema hili jambo. Lazima ujue kinachoingia ili kama ni malipo, basi yawe malipo stahiki. Yote haya yamefanywa ili ninyang’anywe kinu na kunimaliza kabisa kibiashara.”

3986 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!