Shirika la Bima la Taifa (NIC) limetoa ufafanuzi wa malipo ya Sh milioni 826 kwa mdai wake, S & C Ginning Co. Limited. Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Justine Mwandu, amesema katika majibu ya maandishi kwa Gazeti la JAMHURI kuwa wamelipa fedha hizo kutekeleza amri halali ya Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara.

“NIC haikulipa malipo haya moja kwa moja katika kampuni husika, isipokuwa kwa amri ya mahakama. Yalilipwa kwenye akaunti ya mahakama ambayo nayo ingeyafikisha kwa mdai,” amesema Mwandu.

 

Malipo haya yametokana na dai lililofunguliwa na kampuni hiyo, ikidai kuwa ni Sh 134,908,850 Septemba 19, 1997.

 

NIC walikataa kulipa fedha hizi kwa maelezo kuwa ilikwenda kinyume na sera za Bima, inasema kuwa fedha zitalipwa ikiwa zimeibwa chini ya ulinzi au kwenye kasiki, lakini fedha hizi ziliibwa kwenye maboksi, hivyo hali hii iliwatia wasiwasi iwapo ziliibwa kweli.

 

Amesema mdai hakuridhika, ndipo akafungua kesi ya madai namba 2/2003, ambapo Mei 5, 2004 alishinda na mahakama kuiamuru NIC imlipe Sh 134,908,850 pamoja na riba ya asilimia 20 ya fedha hizo kwa mwaka tangu zilipoporwa hadi tarehe ya hukumu, na asilimia saba tangu tarehe ya hukumu hadi zitakapolipwa zote.

 

“NIC haikuridhika na hukumu hii na Februari 28, 2005 ilikata rufani (Civil Appeal No. 21/2005). Januari 15, 2010 rufaa hiyo ilitupiliwa mbali, hivyo uamuzi wa mahakama ukaendelea kusimama, kilichobaki ni utekelezaji.

 

“Kwenye maombi ya utekelezaji, mdai alitaka alipwe ‘compound interest’ ambapo NIC ilikataa na kutaka kulipa ‘simple interest’ lakini baada ya hoja za kisheria kutolewa Juni 1, 2012, mahakama iliamuru mahesabu yapigwe kwa ‘compound interest’ ambapo hadi Juni 2012 ‘decretal sum’ ilikuwa Sh milioni 826.

 

“Hivyo, ili mdai apate fedha zake aliiomba mahakama itoe ‘garnishee order’. Mahakama ilitoa ‘garnishee nisi’ Novemba 29, 2012 ikifuatiwa na ‘garnishee absolute’. Desemba 17, 2012 ‘garnishee absolute’ ilimwamrisha ‘banker’ wetu atoe kiasi tajwa kutoka akaunti ya NIC na kuhamishia kwenye akaunti ya mahakama ili izifikishe fedha hizo kwa mdai,” amefafanua Mwandu.

 

Kuhusu kuwapo kwa taarifa za kufukuzwa kazi kwa baadhi ya watumishi wa NIC kutokana na makosa ya uzembe na kulisababishia shirika hilo hasara ya mamilioni ya shilingi, Mwandu amesema:

 

“Katika kipindi cha ajira mpya ya NIC (mwaka 2010-2012), wafanyakazi wawili katika fani ya uhasibu walifukuzwa kazi kwa kulisababishia Shirika hasara. Shirika limewakabidhi kwenye vyombo vya sheria. Hawa hawahusiani na fedha tajwa hapo juu.”

 

Akizungumzia mikataba ya wafanyakazi wa NIC, Mwandu ambaye wakati huo alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji na ameteuliwa rasmi kushika wadhifa huo hivi karibuni, amesema watumishi wote waliajiriwa mwaka 2010 kwa mikataba ya miaka mitatu iliyoishia Desemba 31, 2012.

 

“Kutokana na kukosekana kwa Bodi ya Wakurugenzi wa NIC hadi tunafunga mwaka 2012, uongozi wa Shirika uliwasilisha mapendekezo ya nyongeza za mikataba yao katika Wizara ya Fedha kutoa mikataba mipya, na tayari imeshatoa nyongeza hiyo kwa kipindi kingine cha miaka mitatu kuanzia Januari 1, 2013 kwa wafanyakazi wote ambao mamlaka ya ajira zao si Bodi ya Wakurugenzi.

 

“Aidha, Wizara inaendelea kufanya tathmini ya utendaji kazi kwa watumishi ambao ajira zao ni za Bodi ya Wakurugenzi kwa kipindi kilichopita, ili nao waidhinishiwe nyongeza ya ajira zao. Hata hivyo, wafanyakazi hao wanafanya kazi kwa kibali cha miezi sita hadi Juni 30, 2013,” ameongeza.

 

Mwandu amesema kwamba ingawa kukosekana kwa Bodi ya Wakurugenzi wa NIC kunasababisha baadhi mambo kutofanyika kwa wakati, kwa sasa masuala ya dharura huwasilishwa Wizara ya Fedha kwa uamuzi.

 

Kuhusu ununuzi wa ‘servers’ za kompyuta za ofisi ya NIC, Mwandu amesema Shirika limetumia dola (za Kimarekani) 24,084 kununua ‘servers’ nne kuboresha utendaji kazi, ikiwa ni pamoja na kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu za Shirika na kwamba gharama hiyo ni ya kawaida katika soko la sasa.

 

Mwandu pia amesema katika kutimiza malengo ya kibiashara na kazi za kila siku, wafanyakazi husafiri kwenda mikoani kwa madhumuni mbalimbali likiwamo la kuhudhuria kesi zinazolikabili Shirika hilo.

 

Katika hatua nyingine, Mwandu amesema Wakurugenzi wa NIC hawakwenda Dubai kununua lifti za Shirika, ila ununuzi wa lifti zote 11 umetekelezwa na kampuni ya S.E.C (East African) Ltd (Mitsubish Lifts) iliyoshinda zabuni, baada ya lifti zilikokuwapo kuchakaa.

 

“Hivi sasa NIC inaweza kulipa malimbikizo ya madai mengi ya nyuma, ambayo ilishindwa kuyalipa katika miaka ya 1990 kutokana na kuyumba kifedha,” amesema Mwandu.

 

NIC wametoa ufafanuzi huu baada ya kufungua kesi katika Baraza la Habari Tanzania na baada ya pande zote mbili kusikilizwa, ilibainika wazi kuwa kulikuwapo udhaifu wa mawasiliano katika kutafuta habari hii. Pande zote zimekubali kupeana taarifa kila zinapokuwapo na kwa wakati.

1062 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!