Nianze kwa kuwaomba kila mbunge anayetambua kuwa amechaguliwa na wanyonge na maskini wa Tanzania ili atetee maslahi yao na ya watoto wao, asome kwa makini makala haya kisha achukue hatua.

Jumanne, April 30, mwaka huu, Mheshimiwa Yusuf Haji Hamisi, Mbunge wa Nungwi, alitaka kujua matumizi ya fedha za rada. Serikali, kupitia Naibu Waziri wa Fedha, ilijibu kwamba  fedha zitatumika kwa kuchapishia vitabu vya kiada na pia kwa kununulia madawati.

Kwa upande wa vitabu, msemaji huyo wa serikali alidai kuwa taratibu zote zimefuatwa katika uchapishaji wa vitabu hivyo.

 

Kwa bahati mbaya, mbunge mhusika aliridhika na jibu hilo la serikali. Kwa hiyo, hakuuliza swali la nyongeza ambalo lingetaka ajulishwe  ni taratibu zipi hizo zilizofuatwa katika uchapishaji wa vitabu hivyo.

 

Katika mazingira hayo, nimeamua kuwaandikia wabunge wenye uchungu na elimu ya watoto wa masikini wa Tanzania, ili kuwajulisha ukweli wa mambo.

 

Kwa jumla, suala la matumizi ya fedha za rada ni kashfa nzito kwa Wizara ya Elimu. Wameamua kugawana fedha za rada bila kufuata taratibu zozote katika uchapishaji wa vitabu vinavyohusika.

 

Kwa hiyo, Bunge lisifanye mzaha. Hili ni muhimu kwa Taifa letu ama sivyo litawekwa na wananchi katika kundi la mabunge dhaifu. Je, ni mambo yapi yangefuatwa katika uchapishaji wa vitabu hivi?

 

Izingatiwe kuwa vitabu hivi si vipya. Vimetumiwa na walimu kwa muda mrefu. Wamelalamika kwa muda mrefu kuwa havifai. Kwa hivyo, jambo la kwanza kabisa ambalo lingefanyika ni kukusanywa maoni ya walimu wa masomo mbalimbali. Hatua hiyo ingewezesha wizara kujua vitabu vipi viendelee kuchapishwa na marekebisho yapi yafanyike na vitabu vipi visichapishwe tena.

 

Jambo hili la msingi halikufanyika. Binafsi nimelipigia kelele katika Gazeti la RAI tangu mwezi Mei mwaka jana. Wakubwa wa wizara hawakusikia kitu. Kwa hiyo, wametumia mwaka mzima kupanga namna ya kugawana fedha za rada bila kufuata taratibu. Wameamua kuhujumu elimu ya watoto wa maskini kwa sababu watoto wao hawasomi shule za watoto wa maskini.

 

La pili, hakuna zabuni yoyote iliyotangazwa inayohusiana na uchapishaji wa vitabu hivi. Wachapishaji wa vitabu wamepewa kazi hiyo kirafiki na kwa kujuana, mradi tu wana uwezo wa kutoa rushwa.

 

La tatu, zabuni yoyote sharti ishindanishe vitu. Katika suala hili la vitabu, hakuna vitabu vilivyoshindanishwa ingawa tuna utitiri wa vitabu vya kila somo kwa kila darasa. Basi, mambo yanayotakiwa yafanyike ni mawili.

 

La kwanza, Bunge liunde tume mara moja ambayo itafuatilia ukweli kwamba vitabu hivi vibovu vinachapishwa upya bila kwanza kutafutwa maoni ya walimu, kwamba hakuna zabuni yoyote iliyotangazwa na kwamba hakuna vitabu vilivyoshindanishwa.

 

La pili, walimu wa masomo mbalimbali wapewe nafasi ya kuvipitia vitabu vyote vilivyoamuliwa kuchapishwa upya, ili wateue kitabu kimoja tu cha kiada kwa kila somo kwa kila darasa, ili kuondokana na utitiri wa vitabu vya kiada vinavyoshindana na kwa kupotosha mambo.

 

Hii inahitaji zoezi la uchapishaji wa vitabu hivi kusitishwa mara moja kabla wachapishaji hawajaingia gharama kubwa. Kwa mambo matatu haya, Bunge lisisite kusitisha uchapishaji wa vitabu hivi, ili kuokoa fedha ya rada iliyopangwa kutumika vibaya.

 

Kwanza, nimeendelea kuijulisha wizara maoni na matakwa ya  walimu kuhusu suala la uchapishaji wa vitabu hivi tangu Mei mwaka jana. Wa wizarani wakakaa tu kupanga namna ya kugawana fedha ya rada. Hawakutaka kusikia kitu.

 

Pili, utaratibu haukufuatwa katika wachapishaji kupewa kazi hiyo, bali wamepewa kwa misingi ya rushwa.

 

Tatu, kwa mujibu wa mahojiano aliyofanya Waziri Kawambwa na Gazeti la MWANANCHI, vitabu hivi vimepangwa kuingia shuleni mwezi Septemba mwaka huu. Kwa hivyo muda huo huo utumke upya.

 

Wakati huo huo, wananchi wanajua  tabia ya Bunge lao ya kupoteza wakati kulumbana katika mambo yasiyo na faida kwa Taifa letu. Suala la Bunge kuunda tume ya kufuatilia suala la uchapishaji vitabu, halihitaji malumbano.

 

Bunge linatakiwa lione umuhimu wa kuwatua walimu mzigo huu wa kufundishia vitabu vibovu, ambao Wizara inatakiwa kuendelea kuwatwisha walimu kwa manufaa ya watu wachache walioko wizarani.

 

Lakini pia,  wananchi wanajua wabunge wa chama tawala (CCM) wanavyoikingia kifua Wizara ya Elimu pamoja na ukweli kwamba ndiyo wizara inayoongoza Tanzania kwa kufanya mambo ovyo ovyo.

 

Katika mazingira kama hayo, wabunge wa chama tawala wakitumia wingi wao kupinga hoja ya kuundwa tume ya kutafuta ukweli wa mambo, basi wabunge wa upinzani watumie uchache wao kuitisha  maandamano ya wazazi maskini nchi nzima, ya kupinga watoto wao kuendelea kufundishiwa vitabu vibovu.

 

Maandamano kama hayo hayatakuwa tu halali bali pia yataungwa mkono na wazazi wote maskini wa Tanzania, bila kujali tofauti zao za kisiasa. Bunge lisifanyie mzaha suala hili.

By Jamhuri