Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Adolf Kumburu, anachunguzwa na vyombo mbalimbali vya uchunguzi kuhusiana na madai ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma.

Kiini cha uchunguzi huo ni zabuni ya kuhuisha ya mashine ya mnada (upgrading) ambayo inagharimu fedha za Euro 324,396 sawa na Sh milioni 700 aliyotaka ipewe kampuni ya Auxcis ya Ubelgiji.

Tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Msajili wa Hazina; na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), zimeanzisha uchunguzi kuhusu kashfa hiyo.

Taarifa za uhakika pamoja na nyaraka ambazo JAMHURI inazo, zinaonyesha kuwa Februari 2014, Kumburu alianzisha mchakato huo wa zabuni bila kuhusisha kitengo cha ununuzi cha TCB.

Inadaiwa kuwa Kaimu Ofisa Ununuzi wa TCB, alikuja kufahamu mpango huo wakati Kumburu alipokuwa akimwagiza Mkurugenzi wa Fedha kuilipa kampuni hiyo malipo ya awali ya asilimia 15.

Mawasiliano ya barua pepe ambayo gazeti hili linayo, yanaonyesha kuwa Kumburu anadaiwa kumhamasisha mwakilishi wa kampuni hiyo kupokea malipo hayo kwa fedha taslimu, jambo ambazo mzungu huyo alikataa.

Ujumbe huo uliotumwa kwa Stefaan De Visser unasomeka: “I confirm the advance payment. If it can be possible to avoid costs, you could get it in cash on your arrival than bank transfers”.

Kwa tafsiri rahisi, ujumbe huo ulikuwa unamshawishi mtaalamu wa kampuni hiyo kupokea fedha taslimu atakapowasili Tanzania badala ya kuhamisha malipo hayo kwa njia ya benki.

Februari 11, 2014, mzungu huyo alimjibu Kumburu kuwa kwa sheria za Ubelgiji, hairuhusiwi kupokea malipo kwa fedha taslimu kwa kiwango hicho kikubwa cha pesa ambacho kilikuwa asilimia 15.

Mzungu huyo aliandika: “By Belgium law we cannot accept cash payment for that amount. It (is) also would be a great risk at the border customs. If Possible I would like to avoid this”.

Kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali, Kaimu Ofisa Ununuzi, Solis Kapinga alijaribu kumuuliza Mkurugenzi wa Fedha namna Auxcis alivyopatikana, na ndipo Mkurugenzi wa Fedha akasita kulipa.

Inadaiwa kuwa Aprili 13, 2014, Kumburu alimwita ofisini kwake Kapinga na kumweleza kwa vitisho jinsi mtambo huo wa mnada unavyosumbua na hadi kuamua kumpa kazi hiyo Auxcis.

“Maelezo yake yalikuwa ya vitisho ili kumjaza hofu ambayo ingepelekea (ingesababisha) kutoa maamuzi (uamuzi) yasiyo sahihi kwa kubariki njia ya single source na kutoa mkataba kwa Auxcis bila kufuata utaratibu,” imedokezwa taarifa ambayo JAMHURI ina nakala zake.

Inadaiwa kuwa Kumburu alishikilia msimamo wa kampuni hiyo kupewa kazi hiyo kwa vile ndiyo iliyoleta mtambo huo miaka 15 iliyopita, hivyo kampuni hiyo ndiyo inayostahili kupewa kazi hiyo.

“Ofisa Ununuzi aliwaulize watoe kiambatanisho cha kuhalalisha kwamba Aucxis ndiye pekee anaweza kufanya kazi hiyo na kama ana waranti inayozuia mtu mwingine kuikarabati mashine hiyo,” imeelezwa.

Inaelezwa kwamba baada ya kushauriana, wataalamu walishauri zabuni hiyo itangazwe kimataifa, lakini baada ya Kumburu kupewa ushauri huo inasemekana alikuwa mkali na kudai mashine inaweza kusimama.

Baadaye, Mkurugenzi Mkuu huyo inadaiwa alimwalika mwakilishi wa kampuni hiyo na kuja nchini kufanya upembuzi yakinifu kwa gharama za Bodi hiyo ambacho ni chombo cha Serikali.

Inaelezwa kuwa Machi 17, 2014 mtaalamu wa kampuni hiyo alifika nchini na kupangishiwa chumba katika Hoteli ya Park View na kulipiwa gharama zote na Bodi ikiwamo nauli, chakula na malazi.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, baada ya upembuzi yakinifu huo kukamilika, zabuni hiyo ilitangazwa katika gazeti la The East Africa pekee ambalo wakati huo lilikuwa limefungiwa nchini.

Kampuni ya Auxcis ya Ubelgiji iliomba zabuni hiyo kwa Euro 324,396 wakati SPA ya Uingereza ikiwa imeomba kazi hiyo kwa dola 420,000 za Marekani (Sh milioni 900).

Mchakato huo wa zabuni sasa umehamishiwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kutokana na maombi ya Kumburu baada ya kuona maofisa wake wanamkwamisha katika mipango yake.

Wiki mbili zilizopita, Msajili wa Hazina aliunda tume ya watu wanne ikiongozwa na Aisha Mponezya kuchungumza mchakato mzima wa namna Mkurugenzi Mkuu  huyo alivyoshughulikia zabuni hiyo.

Kwa upande wake, Kumburu amezungumza na JAMHURI na kusema Bodi yake haijatangaza zabuni yoyote kwa kazi inayozungumzwa.

Amesema suala hilo limefikishwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kupata baraka, na kwamba kazi itaendelea baada ya uamuzi wa ofisi hiyo.

Amepinga kuwasiliana na Mbelgiji huyo, akasema: “Mawasiliano ya e-mail siyo official communication (mawasiliano rasmi), mawasiliano kwa jambo kama hili ni barua.

“Nisingeweza kumwita huyo mtu kuja kuchukua fedha wakati suala lenyewe-zabuni ilikuwa haijatangazwa na hadi sasa haijatangazwa. Asingeweza kupewa pesa kwa kazi ambayo haijafanyika,” amesema Kumburu.

By Jamhuri