Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Mafunzo ya Kompyuta (UCC), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ikiongozwa na Profesa Makenya Maboko, imetoa ufafanuzi kuhusu tuhuma za wafanyakazi zaidi ya 30 wa kituo hicho wanaomtuhumu Mkurugenzi Mtendaji, Dk. Ellinami Minja na menejimenti yake kukihujumu.

Katika taarifa iliyotolewa Oktoba 1, mwaka huu na bodi hiyo ambayo nakala yake Gazeti la JAMHURI limeiona, inasema kituo hicho kinafanya mabadiliko yanayolenga kuboresha na kuimarisha huduma ili kijiendeshe kibiashara bila kupoteza ruzuku.

Taarifa hiyo imeeleza mabadiliko hayo yanakuja ili kuondoa hasara ambayo kituo hicho kwa miaka ya karibuni kimekuwa kikipata, ikiwa ni pamoja na matokeo yasiyoridhisha kibiashara huku idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa katika kozi zake mbalimbali ikishuka kila siku.

 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, biashara ya mafunzo ya kompyuta katika kituo hicho imepungua kwa asilimia 56 ambavyo ni sawa na wastani wa asilimia 11 kila mwaka, tangu mwaka 2012 mpaka sasa.

Bodi hiyo imeeleza kuwa kwa kushirikiana na menejimenti ya kituo, imefanyika mikakati na hatua mbalimbali za kukiokoa, ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa rasilimali watu (Human Resource Audit) uliofanyika Agosti, 2015 kupitia sera ya motisha kwa wafanyakazi (Incentive and Bonus Scheme), sera ambayo ililenga kuongeza tija, mapato na faida.

Menejimenti chini ya usimamizi wa bodi wamefanya mapitio ya muundo wa utumishi (Scheme of Service) zoezi ambalo lililenga kuweka uwiano baina ya wafanyakazi wa kada hiyo kulingana na muda waliokaa kazini (seniority) na majukumu pasipo upendeleo na muundo huo unatajwa kuanza kutumika tangu mwaka juzi.

 

Vilevile taarifa hiyo inaeleza kuwa menejimenti ilifanya kazi ya kuupitia mpango mkakati na kutengeneza mpango mkakati mpya wa 2016/2017 mpaka 2020/2021 (Revised Strategic Plan), mpango ambao ulilenga kuwa na taasisi inayojiendesha kwa faida,  kwa kuandaa na kutoa huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) zenye ubora wa juu.

Kutokana na mpango huo, taarifa hiyo inaeleza kuwa menejimenti tangu Julai, mwaka juzi ilianza kuajiri na kuhifadhi (retain) wafanyakazi weledi na walioridhika.

Taarifa hiyo pia imejibu tuhuma za wafanyakzi hao kwamba menejimenti imehamisha baadhi ya mali zake kutoka kwenye majengo binafsi kwenda kwenye majengo ya umma na kusababisha uharibifu wa mali za mamilioni kutokana na kukosa sehemu ya kutunzwa mali hizo.

 

Kwenye taarifa hiyo imeelezwa kuwa menejimenti ilifanya hivyo ikilenga kupunguza gharama za uendeshaji ambavyo kodi ya majengo tangu wahame kwenye majengo hayo imepungua kutoka Sh bilioni 1.5 mwaka 2014/2015 hadi Sh milioni 400 mwaka 2018/2019.

Vilevile uendeshaji wa kituo hicho kutokana na mabadiliko hayo unatajwa kupungua kutoka gharama za pamoja za uendeshaji (central overheads) kutoka Sh bilioni 2.5 mwaka 2014/2015 hadi kuwa chini ya Sh bilioni 1 mwaka 2017/2018.

Hata hivyo, kwenye taarifa hiyo imebainishwa kuwa kituo hicho kimejipanga kuimarisha biashara za utengenezaji wa mifumo ya kompyuta (software) na miundombinu ya Tehama (ICT infrastructure) ambazo zimekuwa na mahitaji makubwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, serikali pamoja na taasisi zake.

 

Kituo hicho kimelenga kurekebisha biashara ya mafunzo na utumiaji wa rasilimali zilizoko katika matawi yake kwa kuhuisha mitaala yake na rasilimali watu kulingana na mahitaji ya soko na mabadiliko ya tasnia ya Tehama nchini na duniani kote.

Mabadiliko hayo yanayolenga kuboresha kituo hicho yanatajwa kuathiri sehemu kuu tatu ambazo ni pamoja na kufungwa kwa matawi ambayo yamekuwa yakijiendesha kwa hasara, ambayo ni pamoja na Tawi la Arusha ambalo litafungwa Oktoba 2018, Tawi la Mwanza na Mbeya yote yakitarajiwa kufungwa Machi 2019.

Huku matawi matatu yakitajwa kubakizwa ambayo ni makao makuu ya kituo hicho yaliyoko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tawi la City Centre (Dar es Salaam) na Tawi la Dodoma ambalo linatajwa kubaki kwa sababu ni eneo la kimkakati kwa kituo hicho.

Mabadiliko hayo yatawagusa baadhi ya wafanyakazi, huku baadhi wakitajwa kupunguzwa na kwamba mpango wa kutekeleza azima hiyo umeanza Juni mwaka huu baada ya menejimenti kutoa notisi ya kusudio la kufanya hivyo.

Gazeti la JAMHURI linafahamu kwamba kwa sasa menejimenti inafanya majadiliano na Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (THTU) ili kuona njia sahihi ya kufanikisha kupunguza wafanyakazi.

Kwa upande mwingine, wafanyakazi wa kituo hicho wameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba bodi ya wakurugenzi haijatenda haki katika taarifa iliyoitoa kwa umma, kwani kuna mambo yanayoihusu menejimenti ambayo hayajawekwa wazi.

Wakizungumza na JAMHURI, wafanyakazi hao ambao majina yao hawakupenda yaandikwe, wamesema bodi ilipaswa kumuwajibisha Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Dk. Ellinami Minja pamoja na wenzake, kwani hasara na utendaji mbovu unaotajwa katika taarifa hiyo umesababishwa na uongozi wake.

Wanahoji, kwanini taarifa hiyo hailezi hasara iliyopatikana kutokana na mali za kituo hicho zilizoharibiwa makusudi vikiwemo vifaa kama kompyuta, viti, viyoyozi (AC), vifaa vya kuzimia moto na meza ambavyo vimegharimu mamilioni ya fedha za umma?

 

“Wanawezaje kusema kituo hiki kinakosa wanafunzi wakati jina la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam linakibeba kituo hiki? Wanafunzi wanaotaka kujiunga na mafunzo ya kompyuta wako wengi.

 “Menejimenti imekuwa mbovu sana, wanashindwa kusema ukweli kwamba Minja ameshindwa kukiongoza vizuri kituo hiki, wao wasianze kusingizia mambo mengine,” wanasema wafanyakzi hao.

JAMHURI limemtafuta Dk. Ellinami Minja ili kupata ufafanuzi wa taarifa ya bodi hiyo lakini hakupatikana kuizungumzia taarifa hiyo.

Hata hivyo kupitia kwa katibu muhtasi wa ofisi ya Dk. Minja, alijibu kuwa endapo ratiba yake itamruhusu kuzungumza na Gazeti la JAMHURI, atamfahamisha mwandishi wa gazeti hili.

By Jamhuri