Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, amewataka viongozi wa dini kuwafichua walioua viwanda vilivyokuwa mhimili wa uchumi wa mkoa huo pamoja na viongozi waliohusika kufilisi mali za vyama vya msingi na ushirika.

Mghwira ameyasema hayo wakati akizindua kamati ya maridhiano ya  mkoa ambayo inaundwa na viongozi kutoka madhehebu mbalimbali ya dini pamoja na watendaji wa serikali wakiwamo wakurugenzi wa halmashauri za wilaya.

Amesema Mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa na viwanda vingi ambavyo licha ya kutoa ajira kwa wakazi wa mkoa huo vilikuwa ni chachu katika kuchangia pato la taifa lakini kwa sasa viwanda hivyo vimekufa. 

“Inakuwaje Kiwanda kama cha Kilimanjaro Machine Tools kilichokuwa kimeajiri watu 2,000 leo kimekufa na hakuna aliye tayari kumtaja aliyekiua, vyama vyetu vya ushirika na mashamba yake viko wapi kwa sasa?” amehoji Mama Mghwira.

Mkuu wa Mkoa huyo anasema baadhi ya walioviua viwanda hivyo walikuwa viongozi wa dini lakini hakuna mwenye uthubutu wa kuwataja na kuonya kuwa hali hiyo lazima ikomeshwe.

Mghwira anasema kuna wimbi la vijana kutokuwa na ajira, wakiwamo wahitimu wa vyuo vikuu, tatizo ambalo anasema lingeweza kutatuliwa kama viwanda vilivyokufa katika maeneo mbalimbali ya nchi vingekuwa vinafanya kazi.

Mkoa wa Kilimanjaro unapakana na nchi ya Kenya katika Wilaya ya Rombo, huku wilaya za Mwanga na Same ziki kabiliwa na wimbi kubwa la uingizwaji wa bidhaa za magendo, tatizo ambalo kwa muda mrefu limekosa ufumbuzi.

Mama Mghwira akizungumzia migogoro ya wawekezaji na wananchi katika Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na migogoro ya wafugaji na wakulima hasa katika Wilaya ya Same, amewataka viongozi hao kuwa chachu ya kuleta maridhiano baina ya makundi hayo. 

“Ni rai yangu kwenu viongozi wa dini muwe watu wa kutatua migogoro, muwe watu wa kuunganisha jamii, msiwe watu wa kuchochea migogoro, mkiyafanya haya naamini tutakuwa na amani ya kweli,” amesema. 

Katibu wa kamati hiyo, Mchungaji Elias Silayo, amesema ukosefu wa haki unasababisha ukosefu wa amani, hivyo kamati hiyo ina wajibu wa kuhamasisha jamii katika kupatikana kwa amani. 

Silayo amesema kamati hiyo pia ina jukumu la kuhamasisha jamii kuacha kujichukulia sheria mikononi, lengo likiwa ni kupunguza matukio ya vifo, huku pia akisisitiza kwa mamlaka za serikali kutenda haki ili kupunguza matukio ya watu kujichukulia sheria mikononi. 

Mchungaji Silayo ametaja malengo mahususi ya kuanzishwa kwa kamati hiyo kuwa ni kudumisha na kuendeleza amani na maridhiano nchini, pia kuzuia migogoro ya kidini, kijamii na kisiasa ili kudumisha amani.

“Nyakati za nyuma viongozi wa dini walikuwa wanatafutwa, leo viongozi wa dini wanaendesha kampeni  ili wachaguliwe, hii yote inatokana na ukosefu wa maadili, hivyo kamati yetu inao wajibu wa kutoa elimu ya maadili kwa viongozi wa kijamii, kuanzia viongozi wa serikali na viongozi wa dini,” amesema. 

Mwenyeki wa kamati hiyo, Alhaj Ibrahim Mollel, amesema kamati hiyo itajikita katika utatuzi wa migogoro na kuzuia migogoro kabla haijatamalaki, lengo ni kuleta maridhiano kwa pande zote mbili zinazosigana. 

Kamati hiyo ya maridhiano ilianzishwa mwaka 2015 na kusajiliwa Machi 3, 2016 chini ya sheria ya taasisi na ilizinduliwa rasmi Julai 13, 2016 na Rais John Magufuli.

By Jamhuri