Bomoa BomoaYalikumba Kanisa la Gwajima

Kufuatia zoezi la serikali la kupanua na kuboresha miundo mbuni mbalimbali nchini hususan ya barabara katika jiji la Dar es Salaam ambapo imelazimu baadhi ya maeneo kubomolewa ili kupisha zoezi hilo la upanuzi, Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima nalo limekumbwa na kadhia ya kubomolewa.

Kanisa hilo lililoko jirani kabisa na Barabara ya Morogoro ambayo serikali imepanga kuipanua ili kurahisisha usafiri na kupunguza foleni, lilitakiwa kubomolewa kutokana na kuwa ndani ya eneo la hifadhi ya barabara hiyo.

Mchungaji Biyagaza wa Kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko chini ya Askofu Gwajima, ameeleza kuwa serikali iliwapatia notisi ya siku 30 ili wabomoe kipande cha jengo la kanisa hilo kilichopo ndani ya eneo la hifadhi ya barabara.

Mchungaji Biyagaza alieleza japokuwa eneo la jengo limepungua, eneo lililobakia linaimarishwa ili kanisa hilo liweze kuendelea kutoa huduma za kiroho kwa waumini wake.

Aidha kufuatia zoezi hilo la upanuzi wa barabara ya Morogoro ambalo linaenda sambamba na ujenzi wa barabara za juu (fly-over) katika makutano ya barabara eneo la Ubungo, umepelekea kubomolewa kwa majengo mbalimbali ikiwemo majengo ya wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na jengo la Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania ambayo yamebomolewa kufuatia agizo la Rais Dkt. John pombe Magufuli.