Na Deodatus Balile

Wiki iliyopita nilizungumzia wingi wa watu unaokuja duniani na hasa Bara la Afrika. Tanzania kwa sasa inakadiriwa kuwa na watu milioni 58. Mwaka 1950 nchi yetu itakuwa na watu milioni 138. Afika kwa sasa inatajwa kuwa na watu bilioni 1.2 na mwaka 2050 itakuwa na watu bilioni 2.5, huku mwaka 2100 ikiwa na watu bilioni 5.7 sawa na nusu ya watu wote duniani.

Idadi hii ya watu ni fursa na ni kilio. Tayari kwa sasa kutokana na hawa Watanzania milioni 58 tunashuhudia vita ya ajira. Ukitangaza nafasi ya kazi wanaomba watu wengi kuliko idadi ya kazi zilizotangazwa. Tukipita katikati ya miji tunaona vijana wengi wakifanya uchuuzi. Wengi wanauza sidiria mitumba, njiti za meno na vikombe vya plastiki.

Sitanii, haya si maisha. Wakifanya uchuuzi huo wanaishia kupata mlo mmoja kwa siku na wakati mwingine fedha wanazopata zinaishia kwenye nauli. Fikiria kijana anayeishi Mkuranga na anafanya “umachinga” Mwenge, Dar es Salaam. Nauli anayolipa kufika kazini ni kubwa kuliko “Muhindi” anayeshuka ghorofani juu Kariakoo akauza biashara yake ya duka chini ya ghorofa hilo hilo analoishi.

Kichwa cha makala hii kinasema “Bomu la watu laja Afrika -2.”  Ni mwendelezo wa nilichokiandika wiki iliyopita. Wiki tatu zilizopita Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa amezindua kitabu kiitwacho “Making Africa Work”. Tafsiri isiyo rasmi jina la kitabu hiki linamanisha “Mbinu za Afrika kujikwamua kiuchumi.”

Alitarajiwa pia kuwapo Rais (mstaafu) wa Nigeria, Olusegun Obasanjo. Hakufika ila alitumia ujumbe wa video. Kitabu hiki kimeandikwa na watu wanne amabo ni wabobezi katika utafiti. Waandishi hao ni Greg Mills, Olusegun Obasanjo, Jeffrey Herbst na Dickie Davis. Taasisi ya Brenthurst Foundation ya Johannesburg, Afrika Kusini ndiyo iko nyuma ya mpango huu wa kuikomboa Afrika kiuchumi.

Katika uzinduzi huo, Obasanjo alituma ujumbe ulioitaka Afirka ikiwa inataka kujikomboa ihakikishe inawekeza katika Uongozi bora, Umeme, miundombinu na chakula. Mimi naongeza na makazi bora. Inawezekana Obasanjo alijumuisha makazi bora kwenye miundombinu ila mimi nadhani ni vyema makazi bora yakatajwa bayana.

Sitanii tunapaswa kuodokana na kufanya kazi kwa mazoea. Ni ukweli usiopingika kuwa Serikali inaweza kubadili maisha ya wananchi wake kwa kuanzisha miradi aliyoitaja Obasanjo. Nchini Brazil, kwa mfano kuna mji unaitwa Curitiba. Mji huu mwaka 1974 ulianzisha ujenzi wa njia ya mabasi ya mwendokasi maarufu kama BRT. Mradi huu tayari umeingwa na miji 250 duniani, tukiwamo sisi Tanzania.

Wakati wanajadili kuanzisha BRT mwaka 1971, waliona kuwa gharama ya kujenga njia za chini (subways) zilikuwa juu kwa zaidi ya asilimia 90 ya gharama za kujenga BRT. Tangu wamejnga BRT, Curitiba uchumi wao umekuwa unakua kwa zaidi ya asilimia 7 kila mwezi na pato la mtu mmoja mmoja limekua likikua kwa asilimia 30. Hawa wameondoa umaskini kwa kuboresha usafiri pekee.

Sitanii, hapa kwetu Tanzania tunayo makazi holela. Kitabu hiki kinaeleza haki ya asili tuliyonayo ya kijiografia, ambao ni ukanda wa Bahari ya Hindi. Kitabu hiki kinailinganisha Panama na Dar es Salaam, jinsi tunavyolitumia eneo letu la kijiografia kufanya biashara na nchi zilizotuzunguka.

Hakika, kadri siku zinavyopita ndivyo mahitaji ya nyumba yanavyoongezeka. Iwe tunataka au hatutaki kuna watu wengi wanaishi katika mazingira hatarishi. Idadi ya nyumba haitoshi. Duniani kote Serikali inajihuisha na sera, na sekta binafsi inajihusisha na ujenzi wa nyumba.

Sitanii, kasi ya ujenzi wa viwanda tuliyonayo, inapaswa kwenda sambamba na ujenzi wa nyumba. Tukifanya hivyo, tutakuwa tunaweka maandalizi rasmi na halali ya kuhakikisha tunawahifadhi watu milioni 138 ifikapo mwaka 2050. Nitaendelea na uchambuzi wa kitabu hiki wiki ijayo.

995 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!