Kiwango cha soka kinakua Tanzania

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeeleza kuridhishwa na ukuaji wa kiwango cha mpira wa miguu hapa nchini. Msimamo huo umetolewa na Ofisa Uhusiano wa TFF, Boniface Wambura katika mahojiano maalum na JAMHURI jijini Dar es Salaam, hivi karibuni.

Wambura amesema uwezekano wa timu za hapa nchini kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya soka ndani na nje ya Tanzania, ni mkubwa kama serikali na wadau mbalimbali wataongeza uwekezaji katika tasnia hiyo.

 

“Sasa hivi hata kwa upande wa ligi, improvement (uboreshaji) ipo, madaraka mengi yameondolewa TFF na kupelekwa kwenye kamati za klabu husika yakiwamo mamlaka ya kufuatilia wafadhili na kulipa wachezaji kwa wakati,” amesema Wambura.

 

Ameongeza, “Kiwango cha soka kinakua Tanzania, sasa hivi huwezi kukilinganisha na siku za nyuma, mimi naona kuna mabadiliko ya kutia moyo kwa sababu ukiona timu imefungwa 4-2 lakini bado inashabikiwa ujue kiwango chake kinaridhisha.”

 

Maelezo hayo ya Wambura yanailenga moja kwa moja Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) iliyofungwa na Ivory Coast kwa kiwango hicho cha mabao katika mchezo wa kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa Brazil, mwakani.

 

Timu hizo zilimenyana hivi karibuni katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, ambapo Taifa Stars licha ya kupoteza mchezo huo ilipongezwa na mashabiki kutokana na wachezaji wake kuonesha soka la viwango.

 

Kwa upande mwingine, Wambura amepongeza jitihada za serikali katika kuboresha soka nchini, lakini akatumia nafasi hiyo kuiomba iongeze uwekezaji zaidi katika tasnia hiyo.

 

“Serikali imejitahidi kuwekeza katika mchezo wa soka ikiwa ni pamoja na kugharamia ujenzi wa Uwanja wa Taifa,” amesema Wambura na kuendelea:

 

“Lakini bado kuna umuhimu wa serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza bajeti ya michezo. Nchi nyingine zinalea vizuri michezo ndiyo maana zimepiga hatua kubwa ya maendeleo katika michezo.”

 

Kuhusu uibuaji na ukuzaji wa vipaji vya soka hapa nchini, Ofisa Uhusiano huyo wa TFF amehimiza uwepo msukumo wa kuhakikisha shule zote za msingi, sekondari na vyuo vinakuwa na viwanja vya michezo.

 

“Ninalisema hili kwa sababu siku hizi shule nyingi hazina viwanja vya michezo… viwanja vingi vimevamiwa kwa ajili ya matumizi ambayo hayakukusudiwa, hii ni changamoto kubwa kwa serikali,” amesisitiza.

 

Mtazamo huo wa Wambura unaunga mkono mawazo ya wadau mbalimbali wa soka wanaohimiza serikali kujenga mazingira bora ya kuibua na kukuza vipaji vya michezo kwa watoto kuanzia shule za msingi, sekondari hadi vyuoni.

By Jamhuri