Mpendwa msomaji, leo najadili mada ya mwelekeo wa kisiasa katika nchi yetu. Nimeijadili mada hii kwa kina katika Kipindi cha ‘Jicho la Habari’ kinachorushwa na Star TV kila Jumamosi asubuhi kati ya saa 1:30 na saa 3:00 asubuhi. Katika mjadala ule, nilijaribu kuangalia mustakabali wa taifa hili.

Nimeangalia mwelekeo wa taifa letu katika ulimwengu wa sasa. Nimeangalia mkondo wa dunia na vurugu zilizotokea Tunisia, Misri, Libya, Syria na sasa Brazil. Kwanza nikabaini jambo moja. Wananchi ni watulivu na wanapenda amani. Wananchi wanapenda amani ihubiriwe katika mazingira ambayo mipango inayotajwa inatekelezeka.

 

Ukiangalia karibu vurugu zote zinazotokea duniani, wananchi katika nchi hizo wanadai haki ya matibabu, haki ya elimu, haki ya kupata ajira na kujipatia kipato halali, haki ya nchi kuwa na uchumi imara, haki ya huduma za jamii kama maji, umeme, barabara, reli na viwanja vya ndege, haki ya mlo kamili na kuepusha watoto kuwa na utapiamlo.

 

Sitanii, nimeangalia Tunisia na Misri vurugu zilizofikisha mataifa hayo katika hatua ya kuangusha Serikali zilitokana na vijana waliomaliza vyuo vikuu kuuawa mikononi mwa polisi, hivyo wananchi wakapandishwa hasira na kukumbuka ugumu wa maisha wanayoishi, wakaamua kuandamana mitaani kudai serikali zile ziondoke wapate viongozi wapya wa kuwaendeshea mambo yao.

 

Ni kwa bahati mbaya tu katika nchi kama Misri, Libya na Tunisia, baada ya Serikali dhalimu kuondoka, wananchi wamejikuta wanaogelea katika shida kuliko ilivyokuwa awali. Ndiyo maana tunasikia viongozi ‘vipenzi’ wa wananchi wakitangaza hali ya hatari kila kukicha kwa maana ya kuwapo tishio la mapinduzi mengine yenye kutokana na nguvu ya umma.

 

Sitanii, pia nikaangalia nchi kama Uingereza na Marekani, ambako wanapinduana kupitia sanduku la kura (wenyewe wanaita uchaguzi huru), na mambo yao yanaendelea kwenda. Nasema wanapinduana pengine nieleweke maana ukiona chama cha George Bush kimeshindwa na cha Barrack Obama, basi ujue kuwa Wamarekani walikichoka chama cha Bush (Republican) wakaamua wakijaribu chama cha Obama (Democratic).

 

Nafuatilia kwa karibu siasa za mataifa makubwa na madogo kwa nia ya kujipa fursa ya kushibisha ubongo wangu na mawazo muwali. Sipendi kuingiza pumba kichwani mwangu. Ndiyo maana mara kadhaa nimesema napata shida na siasa zinavyoendeshwa katika nchi hii.

Ukiangalia siasa za mataifa niliyoyataja, utabaini kuwa wanasiasa wanauza sera kwa wananchi, zikikubaliwa wanachaguliwa, kisha wakibofoa wananchi wanawabwaga kupitia sanduku la kura, wanachagua chama kingine chenye kuwapa ahadi nyingine na kikazitekeleza.

 

Lakini pia kama tunafuatilia kwa karibu, tutabaini kuwa katika nchi hizi hawafanyi kosa la kukipa chama tawala ushindi wa asilimia 80 au zaidi. Ushindi unaopatikana katika nchi hizi unakuwa ni wa asilimia 52 kwa 48. Hii maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba katika Bunge kama una wabunge kwa uwiano huo, mambo ya hovyo hayatapitishwa.

 

Ikitokea Serikali ya chama tawala inayo hoja inayotaka kuipitisha bungeni, basi inapaswa kuhakikisha ni hoja kweli. Haitatoa fursa ya Spika kusema “Nadhani waliosema ndiyo wameshinda.” Kura zinapigwa kwa kuita jina la mbunge mmoja mmoja. Natamani tuelekee huko.

 

Najua msomaji utakuwa unashangaa mbona sifiki unakokutaka. Mimi nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kuchunguza Kutekwa na Kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda. Uchunguzi huu niliufanya hapa Tanzania na Afrika Kusini alikokuwa amelazwa.

 

Katika uchunguzi huu, Kamati yetu yapo kuna mambo iliyabaini na kuyatolea mapendekezo. Moja na kubwa tulilobaini ni kwamba nchi yetu ipo katika hatari ya kutumbukia kwenye vurugu na mauaji kwa sababu ya vyama viwili. Kwamba watu wanateswa na kuumizwa kwa sababu ya kutimiza malengo ya kisiasa.

 

Sitanii, Kamati yetu haikuwa na mamlaka ya kisheria sawa na ilivyo tume ya uchunguzi inayoundwa na rais, lakini matukio ya mabomu yanayotokea Arusha, yanathibitisha kila kitu tulichokisema. Kamati yetu imebaini kuwa CCM wanafanya kila mbinu Chadema ionekane ni chama cha kigaidi.

 

Chadema nao wanafanya kila mbinu CCM waonekane ni chama kilichoshindwa na hivyo kinatesa watu. Tulisema kwenye ripoti hiyo kuwa vipo viashiria kuwa baadhi ya maofisi ndani ya vyombo vya dola (polisi, usalama wa taifa, hatujui hata jeshini) wamejiingiza kwenye siasa. Hawa wanaingia kwa matamanio.

 

Nilisema hivyo Jumamosi, baadhi ya watu wenye matamanio wakanishambulia. Kwamba miaka miwili iliyopita nilikuwa nazungumza na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, nikamuuza ilikuwaje yeye Odinga na Mwai Kibaki wakashindwa kudhibiti vurugu hadi Wakenya karibu 3,000 wakauawa, alilonijibu lilinitisha.

 

Majibu ya Odinga yanathibitisha kinachoendelea leo hapa nchini. Odinga alisema unapokuwa kwenye upinzani, wapo watumishi ndani ya vyombo vya dola wanaokuletea taarifa za ndani ya Serikali. Hawa wanakuwa na matumaini kuwa ukishinda, hutawasahau.

Pia unapokuwa serikalini kwa maana ya chama tawala, wapo watumishi ndani ya vyombo vya dola ambao wanakuwa na hofu. Hawa Odinga anasema wanakuwa na hofu kuwa chama tawala kikishindwa huenda wakapoteza nyadhifa walizonazo. Kwa hiyo, hawa wanafanya kila mbinu kuhakikisha wanabaki madarakani.

 

Sitanii, Odinga anasema wenye imani na chama tawala wanakuwa wakiwaambia wakubwa kuwa hakuna tabu. Wanawaambia kama ni mabomu na risasi wanazo za kutosha, hivyo wasihofu mtu yeyote. Tena wanawahakikishia kuwa wasiwe na hofu. Wanazo nguvu, fedha na kila kinachotakiwa kuwabakiza madarakani.

 

Nao wenye matumaini kuwa upinzani ukiingia madarakani watateuliwa kuwa wakurugenzi wa Usalama wa Taifa, wakuu wa jeshi la polisi au Jeshi la Ulinzi la Wananchi  wa Tanzania wanakuwa wakiwahakikishia wapinzani kuwa taarifa sahihi walizonazo Serikali ni dhaifu, imegawanyika na kuiondoa madarakani ni sawa na kumsukuma mlevi.

 

Hapa ndipo Kamati yetu imebaini dhana mbili. Dhana ya kwanza kuwa CCM katika harakati za kuifanya Chadema ionekane kama chama cha kigaidi, wanapenyeza watu wao kwenye upinzani na watu hao wanaumiza watu kama akina Kibanda na Ulimboka, kwa nia ya kutumia matukio hayo kuiaminisha jamii kuwa Chadema ni chama cha magaidi.

 

Wanaojenga hoja kuhalalisha dhana hii wanatumia tukio kama la mkanda wa Wilfred Lwakatare na Joseph Ludovick. Wanasema mkanda huu ni mmoja kati ya mingi iliyorekodiwa na mawakala wa CCM kwa nia ya kuitangazia dunia kuwa Chadema ni chama cha kigaidi.

 

Hili likiaminika, matumaini ya dhana hii ni kuwa wananchi wataichukia Chadema sawa na walivyokichukia Chama cha Wananchi (CUF) kilivyopandikiziwa udini hadi kikadhoofika kwa kiwango tunachokishuhudia leo. Hii ni dhana ya kwanza.

 

Dhana ya pili ni ile inayosema kuwa Chadema kwa kusaidiwa na wenye matumaini ya kupata vyeo iwapo itaingia madarakani, wamebuni mpango mkakati wa kuwashughulikia watu mbalimbali katika jamii. Chini ya dhana hii inaelezwa kuwa mkakati wao ni kuwadhuru na hata ikibidi kuua watu maarufu katika jamii.

 

Tukio kama la Dk. Ulimboka, linatajwa kuwa lilitendwa na kundi la watu ndani ya Chadema, ambao hawana baraka za chama sawa na ilivyo kwa CCM kundi linaloivizia Chadema lisivyo na baraka za vikao vya chama, ila makundi haya yapo kazini.

 

Katika dhana hii wanatumia mfano ule ule kuwa maneno yanayotamkwa na Lwakatare ndani ya mkanda, yakilenga kuwa wamteke mmoja wa wahariri na kumdhuru kwa nia ya kuichonganisha Serikali ya chama tawala na wananchi kuwa Serikali inatesa wanaoipinga kama Kibanda na Ulimboka, Chadema ndiyo mpango wake wa dhati.

 

Sitanii, ukichukua maneno ya Odinga, ukayachanganya na mkanganyiko wa kauli zinazotolewa juu ya bomu la Arusha; CCM wakisema ni Chadema na Chadema wakisema ni askari polisi aliyetumwa na CCM, basi ujue tumefika. Mchezo huu sasa utahamia kwenye kisasi.

 

Tukifikia hatua ya visasi, basi ujue hata kwa nchi yetu yatakuwa yametimia. Ndiyo maana kwa busara kabisa, baada ya uchunguzi ule, tulipendekeza ziwepo juhudi za makusudi vyama vya Chadema na CCM kukutanishwa, vikazungumza na kuweka masilahi ya taifa kwanza.

 

Nahitimisha na busara hii. Si lazima CCM ibaki madarakani hata ikibidi kumwaga damu. Pia si lazima Chadema ipate fursa ya kuingia madarakani hata kama ikibidi kumwaga damu. Alichokipanga Mungu, huwa. Kama wakati wa CCM kuondoka madarakani umefika, hata wakiua watu kwa maelfu bado wataondoka tu. Kama wakati wa Chadema kuingia madarakani bado, hata wakiua watu kwa maelfu hawatafanikiwa.

 

Sitanii, 2015 haipo mbali. Mei 30, 2013 tukiwa Tanga nilisema tukiruhusu matendo yanayoendelea ya kuumiza wananchi yakaendelea bila kudhibitiwa, siasa zitalichana taifa hili katika vipande kabla ya 2015. Najua wapo wenye kuchukia wakiona navujisha mipango yao haramu, ila tusipojenga utamaduni wa kusema ukweli, tutaiteketeza nchi yetu.

By Jamhuri