* Bodi yakatisha mkataba ghafla

* Afika ofisini akuta kufuli mlangoni

* Mwenyewe adai umri wa kustaafu

Mkurugenzi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Justine Peter Mwandu, sasa ameondolewa kazini akiwa amebakiza mkataba wa zaidi ya mwaka mmoja wa utumishi wake, imefahamika jijini Dar es Salaam.

 

Taarifa zinasema kwamba Mwandu aliondolewa kazini tangu Februari, mwaka huu, baada ya Bodi ya Wakurugenzi kukatisha ghafla mkataba wake kwa tuhuma mbalimbali za uendeshaji mbovu.

Aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete Aprili 28, 2013 na taarifa zake kutangazwa Ijumaa, Mei 3, 2013 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue. Kabla ya uteuzi huu, Mwandu alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu katika shirika hilo.

Taarifa zinasema kwamba Mwandu hakujua taarifa za kuondolewa kwake kazini, lakini alikuta mlango wa ofisi yake umefungwa, hivyo kulazimika kuondoka kwenye ofisi hizo zilizo Mtaa wa Samora, Dar es Salaam.

Ameondolewa kazini huku taratibu za mwisho kufanyika ilikuwa ofisi yake ifanyiwe uchunguzi kwa tuhuma za madai hewa ya bima yanayofikia Sh bilioni 17, lakini kabla ya ukaguzi huo, bodi imemwondoa ghafla.

Mwenyewe Mwandu amezungumza na JAMHURI na kusema, “Nimestaafu. Japo nina nguvu za kufanya kazi, lakini umri umefikia kikomo kwa mujibu wa sheria. Sipo kazini tangu mwanzo wa Februari hii,” anasema.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dk. Edmund Mndolwa, alipotafutwa hakupatikana lakini taarifa zinasema kwamba kuondolewa kwake kazini mapema kunalenga kumkwepesha na tuhuma na ubadhirifu huo.

Oktoba 23, mwaka jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, alitoa maagizo maalum kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Sh 17 bilioni zinazodaiwa kulipwa kama madai hewa na shirika hilo.

Tayari Zitto ametiwa shime na wadau wa Bima wakiwamo wafanyakazi wa sasa (majina tunayo), wanaomtaka asilegeze msimamo wa kuiokoa NIC wakisema mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini historia itamkumbuka.

“Sisi wengine tumewahi kusema huko nyuma na kuandika kwamba NIC inamalizwa na ulipaji wa madai hewa kuanzia mikoani mpaka makao makuu, lakini hatukusikika,” anasema ofisa mmoja wa Bima anayedokeza gazeti hili kwamba “Bima kuna madudu.”

Anasema kwamba kwa mtu ambaye amewahi kutembelea mikoani kwenye matawi ya NIC akaona wateja wanavyojichotea pesa kutoka kwenye shirika hili, hana budi kumuunga mkono Zitto kwa kutoa maagizo yake.

Anasema kwamba uongozi wa shirika hili uko tayari kukataa kulipa madai halali na kuchangamkia kulipa madai hewa ili wajineemeshe. Chanzo hicho cha habari kinafafanua kwamba CAG ana kibarua kigumu kuchunguza madai hewa hasa katika maeneo ya bima za maisha, mali na ajali.

Taarifa zaidi zinasema kwamba mbali ya madai hewa, pia kuna tuhuma kwenye manunuzi hewa bila kufuata taratibu zozote sambamba na kutengeneza kesi hewa za wateja na wafanyakazi au waliokuwa wafanyakazi.

“Kwa waliokuwa wafanyakazi wanakataa kuwalipa haki zao halali, wanasema twende mahakamani ili wachote pesa kwa kusingizia kuwalipa mawakili na au kuhonga mahakimu ambao si waaminifu,” anasema mtoa taarifa.

Mtoa habari huyo anasema kwamba CAG hana budi kuangalia maeneo hayo yote. “Yaani ayamulike atashangaa atakachokiona. Sh 17 billioni ni fedha ndogo sana.”

Anasema kwamba mwisho wa ukaguzi mashirika mengine ya umma yasilazimishwe kuchukua bima kutoka shirika hili, kwani lilipewa miaka mingi kujirekebisha na kuingia kwenye ushindani, lakini mpaka leo wanalilia upendeleo.

“Fikiria kampuni mpya zilizokuja zinaongoza soko, huku NIC waliokuwako tangu 1963 walilia nini? Wanataka wabebwe mpaka lini?” Anasema mtoa habari huyo na kuongeza:

“Waliokuwa wafanyakazi waadilifu walifukuzwa kwa visingizio mbalimbali. Wakaletwa wapya eti ili kuokoa shirika, kumbe waliokuja siyo mchwa ni viwavi. CAG afanye pia ukaguzi ya uongozi.”

Mtoa habari anawatuhumu baadhi ya wafanyakazi wenzake kuwa ni dhaifu mno. “Nao waangaliwe huko walikotoka walifanya nini? Hapa walipo ni kwa upendeleo tu na ndiyo maana sasa wanaumbuka.”

Mfanyakazi mwingine aliyekuwa tayari kuzungumza hilo kwa sharti la kutotajwa jina, anasema kwamba ni afadhali ya utendaji wa wakurugenzi wa zamani kama Octavian Temu au Mama Margaret Ikongo.

Anasema kwamba vyombo vya dola visaidie kueleza historia ya watu hawa, kwani mathalani mmoja wa viongozi wa juu wa shirika hili anatuhumiwa kuwa tangu ameingia NIC pia alikuwa na hisa Shirika la Bima la Tudor (Tudor Insurance Corporation Limited) miaka hiyo ya 1990.

Taarifa zinasema kwamba kampuni hiyo ilifilisika katika muda mfupi na mkurugenzi wake mkuu akakimbia na madai (premium) kibao za wateja.

Gazeti hili lilifuatilia zaidi habari za Bima ikiwamo ya kampuni hiyo kulumbana na mmoja wa waliokuwa wafanyakazi wa shirika hilo, Rose Roezer, anayelalamikia shirika kukiuka taratibu za uuzwaji wa nyumba na kumnyanyasa.

Mwandu alijitokeza kufafanua shutuma za taasisi hiyo kuuza nyumba zake kwa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na kukwepa kuwauzia wafanyakazi wanaoishi humo.

Amesema uuzwaji wa nyumba na kuachishwa kazi kwa wafanyakazi wa shirika hilo, ilikuwa ni mikakati ya Serikali kuliunda upya shirika hilo na hakukuwa na ukiukwaji wa taratibu wala unyanyasaji kama inavyodaiwa.

Nyumba zinazolalamikiwa ni zile zilizopo katika viwanja namba 75-78, Kitalu 45 B, Kijitonyama kandokando ya Barabara ya Bagamoyo, Dar es Salaam.

Vilevile, Rose anadai kuwa hata kutoendelea kwa ajira yake ulikuwa ni unyanyasaji uliofanywa kwa makusudi na uongozi wa shirika dhidi yake.

Katika mawasiliano ya Mwandu na mwandishi wa habari hii yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam kupitia barua yenye Kumbukumbu Namba: NIC/MD/1/2014 ya Oktoba 27, 2014 ilielekezwa kwa mwandishi.

Mwandu anasema: “Mlalamikaji Rose alikuwa mfanyakazi wa shirika akiwa na mkataba wa ajira ya mkataba wa miaka mitatu yaani kuanzia mwaka 2010 hadi 2012 ambapo mkataba wake wa ajira ulimalizika.

“Kama unavyofahamu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kulifanyia marekebisho makubwa Shirika la Bima la Taifa na kuliunda upya,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Katika moja ya mikakati ya kuliunda upya shirika ilikuwa ni kuwaachisha kazi wafanyakazi wote. Hivyo Februari 2009 Serikali iliwaachisha kazi wafanyakazi wote 506 ili kupisha uundwaji huo.

Barua hiyo ya Mwandu inasema kwamba Rose alikuwa ni mmoja wa walioachishwa kazi na kuomba upya na baadaye kufanikiwa kuajiriwa katika masharti ya ajira ya mkataba wa miaka mitatu mwaka 2010 kwenye NIC mpya.

Anasema wakati Rose akiwa mfanyakazi wa NIC, alikuwa akiishi katika mojawapo ya nyumba za wafanyakazi wa shirika zilizoko Kijitonyama. Baada ya mchakato wa kurekebisha shirika kuanza, nyumba hizo za wafanyakazi pamoja na nyinginezo zinazomilikiwa na NIC nchi nzima, ziliuzwa kwa mashirika na taasisi za umma kwa maagizo ya Serikali.

Baadhi ya wafanyakazi wa iliyokuwa NIC ya zamani walioachishwa kazi mwaka 2009 akiwamo Rose, walifungua kesi mahakamani kupinga kuuzwa kwa nyumba hizo pamoja na madai mengine ya wao kupewa kipaumbele cha kuzinunua nyumba hizo walizokuwa wanaishi.

“Kesi waliyoifungua bado iko mahakamani katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi. Namba ya kesi hiyo ni 64/2013. Katika kesi hiyo, wadai ni Evans Buhire, Rose na wengine,” anasema.

Mwandu anaongeza kuwa madai ya Rose ya kuwa uuzwaji wa nyumba hizo ni ukiukwaji wa taratibu, pamoja na kutoendelea kwa ajira yake kuhusishwa na unyanyasaji, hayana msingi na ni upotoshaji.

Wakati huo huo, Rose naye akizungumza na JAMHURI, anasema mauzo ya nyumba hizi hayakufuata utaratibu na sheria za kuuza nyumba za umma. Kuna uchakachuaji wa hali ya juu uliofanywa katika mauzo ya nyumba hizi.

“Kwanza inashangaza tamko la Serikali la kuuza nyumba lilitoka Oktoba 15, 2009. Tamko hilo lilitoka wakati ambao nyumba zimeshauzwa. Nyumba ziliuzwa Oktoba 8, 2009. Kingine hapa ni kwamba nyumba hizi ni mali ya umma hivyo zilitakiwa ziuzwe kwa zabuni, kitu ambacho hakikufanyika,” alilalamika.

“Hakukuwa na zabuni yoyote iliyotangazwa, walipeana nyumba kimya kimya. Wakazi tuliomo ndani ya nyumba hizi tulitaarifiwa tu kuwa nyumba zimekwishauzwa, kitu ambacho si utaratibu na ni kinyume cha sheria za nchi.

Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1993 (Public Corporation Amendment Act, 1993), Kifungu cha 43 kifungu kidogo cha 1 (a) na (b) havikuzingatiwa, anaeleza Rose kuhusiana na madai yake hayo kwa shirika hilo.

Taarifa zinaeleza kuwa Agosti 3, 2011, NIC ilitoa notisi ya siku saba ikiwataka wafanyakazi wake waliokuwa wakazi kwenye majengo hayo akiwamo Rose, kuhama kumpisha mnunuzi wa majengo huku ikiwatahadharisha kuwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya watakaokaidi agizo hilo. Taarifa zinaainisha kuwa notisi hiyo ilifutwa na shauri lililofunguliwa mahakamani.

Katika kuthibitisha madai yake, Rose ameionesha JAMHURI nyaraka kadhaa zikiwamo barua alizoandikiwa na NIC. Moja ya barua hizo iliyoelekezwa kwake ni ile yenye Kumb. Na NIC/ADM/PF/104 ya Septemba 9, 2011 iliyosainiwa na Anne Mbughuni kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Justine Mwandu.

Barua hiyo ilimweleza Rose kuwa “Ulishauriwa, kama unataka kuendelea na mashtaka ya mwajiri usikubali ajira ya NIC, ila wewe ukatoa kauli kuwa umejitoa katika kesi hiyo. Barua yako kwa M.M and Associates Advocates na barua ya M.M and Associates Advocates kwa NIC zinaonesha kuwa hujajitoa katika hiyo kesi. Hivyo uliudanganya uongozi, na wakati huo huo, umekaidi agizo la mwajiri wako la kukutaka uhame katika nyumba ya shirika ndani ya muda uliotajwa.”

 

By Jamhuri