. Uhamiaji yawanasa Mwananyamala Kisiwani

. Yawaokoa, wasimulia mateso makali ya jijini

. Walikuwa ni watu wa klabu tu, hawalijui jua

. Waliambiwa hapo Mwananyamala ni ‘Sauzi’

. Warejeshwa kwao, waliowaleta waadhibiwa

. Sasa waziponza klabu za Continental, Hunters

. Raha ndani ya klabu hizo sasa ‘zaota mbawa’

 

Kwa kipindi cha miezi mitatu ya mwisho wa mwaka jana (2014), wasichana 22 kutoka nchi za Nepal na India, walitumikishwa ngono na kufanyiwa vitendo vya kinyume na haki za binadamu.

Wasichana hao ambao umri wao ni chini ya miaka 20, walisafirishwa isivyo halali kutoka katika nchi zao na kufanyiwa unyama huo kwenye klabu za usiku za Continental iliyoko jirani na makutano ya Mnara wa Saa ‘Clock Tower’ katikati ya jiji na Hunters iliyoko karibu na Soko la Ma-TX, Kinondoni, Dar es Salaam.

Uchunguzi makini na wa kutuzwa uliofanywa na Idara ya Uhamiaji nchini, ndiyo hasa ulioibua madhambi hayo dhidi ya binadamu katika nyumba moja iliyoko Mtaa wa Ndonga, Mwananyamala Kisiwani ambamo mabinti hao 22 walifungiwa.

Wasichana hao wanakadiriwa kuwa na umri wa chini ya miaka 20. Na kwa mujibu wa taarifa hizo, wasichana 21 wanatoka Nepal wakati mmoja anatokea India.

Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili imethibitishiwa na Idara ya Uhamiaji na Hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wasichana hao waliajiriwa na mfanyabiashara raia wa India, Amar Omprakash Babu Singh (39).

Singh, maarufu kama Omprakash, ni mmiliki wa Kampuni ya Dhamakh Entertainment Limited iliyokuwa inaendesha klabu hizo za usiku.

Omprakash alikuwa akisaidiana kwa karibu sana mkewe, Rekha Sonkar Singh, ambaye taarifa za uhakika zinasema kwamba ni Mkurugenzi mwenza wa Kampuni ya Dhamakh Entertainment Limited.

Katika kampuni hiyo pia wamo Rama Singh, kaka wa Rekha, aliyepewa kazi ya umeneja wa Klabu ya Continental wakati Sarita Tamang, raia wa Napal, alikuwa ni meneja wa klabu ya Hunters.

Wasichana hao walikuwa na mkataba na kampuni hiyo iliyosajiliwa na Wakala wa Usajili wa Kampuni (BRELA) mwaka 2011, ambako baadaye wakaanza kuleta warembo waliowakusanya kutoka vijiji mbalimbali vya huko India na Nepal na kuwasafirisha kwa malengo ya kucheza dansi la asili.

Kwa mujibu wa wasichana hao, mawakala wa Dhamakh Entertainment Limited wanawaendea na kuwalaghai wazazi na walezi wao kwamba wanakwenda Ulaya na Afrika Kusini.

Wasichana hao ambao baada ya kunaswa na Idara ya Uhamiaji wametoa taarifa mbele ya maofisa wa upelelezi kuwa kabla ya kuondoka makwao hupewa angalau mshahara wa mwezi mmoja unaolipwa kwa wazazi au walezi wao.

Wanasema kwamba mawakala wa kuwakusanya hutoa fedha kati ya dola 800 na 1,000 za Marekani kutegemeana na mvuto wa wasichana katika unenguaji.

Mbali ya kuwapata kwa fedha hizo ambazo ni rahisi kuwashawishi wazazi, pia sababu nyingine ya kuwanasa ni ufukara katika maeneo wanakotoka kadhalika uelewa mdogo unaotokana na kukosa elimu.

“Wanaambiwa wanakwenda huko kucheza ngoma zenye asili ya makwao,” anasema Kamishna wa Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka wa Idara ya Uhamiaji, Abdullah Kh. Abdullah.

Anasema kwamba kwa wasichana walionaswa Mwananyamala wakidanganywa wanakwenda Afrika Kusini, wakiwa Mwananyamala pia walisisitiziwa kuwa wako ‘Kwa Mzee Madiba’.

Taarifa zinasema kwamba mmoja wa wasichana hao wahanga wa kusafirishwa isivyo halali, alipotoka nje ya nyumba hiyo alishangaa kuona jua akisema “Ni mara yangu ya tatu kuliona jua tangu nimetoka kwetu.”

Anasema kwamba kwa muda wote wanafungiwa na kwamba hawana nafasi ya kuiona dunia kwa upande wa pili, kiasi kwamba mmojawapo alipata hata hasira za kujichanja.

“Yaani ni hivi, mmoja wa wasichana alikuwa na majeraha ya kuchanja. Alikuwa anajichanja ili tu akiona damu moyo wake utulie kutokana na mateso anayoyapata. Mtu kama huyo alikuwa na hasira mbaya, lakini hakuwa na ujanja, amebanwa,” anasema.

“Mara ya kwanza niliona jua wakati natoka Kathmandu, mji mkuu wa Nepal, mara ya pili nilipotua Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam na mara ya tatu ni leo, hivi jua lipo?” Alihoji msichana huyo kwenye mahojiano na maofisa wa Idara ya Uhamiaji kabla ya kuchukuliwa na kwenda nyumba ya hifadhi iliyoandaliwa na Idara ya Uhamiaji.

Wasichana hao hawakuweza kufurukuta kwani waliishi kwenye nyumba ambayo Omprakash alifuga mbwa wakali wapatao 15 mbali ya walinzi wa kawaida.

Mara baada ya kufika kwenye nyumba hiyo, kila msichana hupewa dakika tano tu za kuwasiliana na wazazi au walezi wao kuwajulisha kuwa wamefika salama na kuanza kazi.

Kwa mujibu wa Kamishna Abdullah, baada ya hapo hunyang’anywa simu za mikononi hivyo kunyimwa haki ya mawasiliano na hati zao za kusafiria maana yake ni kwamba wananyimwa haki ya kusafiri na kutembea (right of movement).

“Hawawezi kuwasiliana, hawawezi kusafiri. Pia hawawezi kuwasiliana na watu wengine na zaidi ya hapo huingizwa mkataba wa ujanja wa kuwalipa dola kati ya 200 na 300 za Marekani, tofauti za zile walizoahidiwa wakiwa kwao dola 800 hadi 1,000 za Marekani, hii ni human trafficking and exploitation,” anasema Kamishna Abdullah.

Wasichana hao walikamatwa Desemba 18, mwaka jana na timu nzima ya operesheni ya Uhamiaji pamoja na wahusika waliowaleta akiwamo Mkurugenzi Omprakash.

“Humo kwenye jumba walimohifadhiwa tulikuta vituko. Kwanza wasichana wengi wanalala chini. Kuna vitanda  (double decker), lakini si vingi, ni kama seti tatu au tusema vitanda sita.”

Anasema kwamba wamekuta wasichana hao wakiwa katika mavazi yasiyostahili kwa heshima ya mwanamke. Walipowakamata waliwakuta wakiwa na uchovu wa kucheza dansi na kwenda kutumika kwenye ngono, kazi ambayo hawakukubaliana nayo tangu mwanzo.

“Katika mahojiano na maofisa wa Uhamiaji, karibu wasichana wote walitoa taarifa kwamba wanafanya kazi ambayo hawakuahidiwa, waliambiwa watafanya kazi nzuri, lakini si ya kutumika katika ngono,” anaelezea.

Anasema kwamba wakichukuliwa na wanaume, anayelipwa ni mwajiri na kwamba yeye anakwenda kutumika tu. Mwajiri alikuwa anavuna dola 100 hadi 200 kwa msichana mmoja anayekwenda kutumiwa.

“Sisi hii kitu hatuitaki kabisa. Kwa sababu hawa wasichana walikuwa wanachukuliwa kutumika kingono regardless of her consent (bila kujali ridhaa yake), hajui kama huyo mwanaume anatumia kinga, au hata kama hatumii ni mzima kiasi gani? Yaani mambo ni mengi na fedha inachukua Kampuni ya Dhamakh,” anasema.

Anasema kwamba mara zote bosi wao hawalipi wasichana hao ikiwa ni pamoja na fedha ya mwisho mara baada ya kumaliza mkataba wa kuwatumikisha kwa muda wote.

Baada ya Idara kufanya kazi hiyo kubwa, mara moja ikaandika maelezo ya kufungua kesi kwenda Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP), ambayo kwa sasa inaongozwa na Biswalo Mganga.

DPP aliona makosa ya usafirishaji wa binadamu kinyume cha Sheria ya Makosa ya Jinai namba 139A (1) (a) kinachosema mtu yeyote anayejiingiza katika biashara ya kununua, kuuza au kubadilishana mtu kwa fedha au njia nyingine yoyote amefanya makosa yanayoweza kumpeleka jela kutumikia kifungo kisichopungua miaka 20.

Kosa hilo linaenenda pia kifungu cha Sheria Namba 139A (1) (b) mtu yeyote kwa makusudi anawezesha biashara ya kununua, kuuza mtu kwa fedha kadhalika kinyume cha kifungu 140 kinachozungumzia kulazimisha ngono na 141 kinachoelezea kuhifadhi au kufungia watu kinyume cha ridhaa yao.

Omprakash kufikishwa Korti ya Kisutu na kushitakiwa kwa makosa matatu likiwamo la kuwasafirisha isivyo halali wasichana hao, ngono na kuwahifadhi.

DPP pia aliagiza uchunguzi wa mali za Omprakash zichunguzwe ambapo ilibainika kuna magari matatu ambayo ni Toyota Hiace lenye namba za usajili T111 CRZ, Toyota Vox lenye namba TCCS na Toyota Rav 4 lenye namba za usajili T540 CBN ambako Mahakama iliamrisha yabinafsishwe na kutumika kwenye shughuli za Serikali.

Hata hivyo, uchunguzi ulionesha kwamba fedha zote alizovuna alikuwa anatuma kwao India na kuwekeza huko.

Kesi ya Omprakash ilikuwa ni namba 227 ya 2014 ambako baada ya DPP kufanya kazi nzuri ya mashtaka, mtuhumiwa alikiri makosa mara moja na kuadhibiwa kulipa faini ya Sh. milioni 15 kwa makosa yote au kwenda jela miaka 10 kwa makosa yote aliyotiwa hatiani. Kadhalika Mahakama ilitoa amri ya mali zake kutaifishwa na Serikali, jambo ambalo lilitekelezwa.

Hii si mara ya kwanza kwa Omprakash kushitakiwa na kufungwa kwani Februari 11, 2007 alifungwa jela miaka minne huko India kwa makosa hayo hayo ya kusafirisha watu na baada ya kutoka, aliona Tanzania ndiko ‘kichaka’ cha kuendelezea kazi zake.

Kuhusu wasichana hao, Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) walifanikiwa kuwarejesha makwao wasichana hao

Taarifa zinasema kwamba Uhamiaji na IOM zilifanya hivyo kwa makusudi ili wasichana wasijikute wanaingia tena katika mikono ya wasafirishaji binadamu na kupelekwa nchi nyingine.

Pamoja na amri nyingine Mahakama iliamuamuru Omprakash kuwalipa mishahara yao kulingana na mikataba yao ambako zilifika dola 30,625 (sawa na Sh 55,125,000). Dola moja kwa sasa hubadilishwa kwa Sh 1,800.

Kwa sasa klabu hizo zimefungwa baada ya yeye pamoja na wakurugenzi wake kufukuzwa nchini kwa P.I.N na kurudi kwao.

“Idara haijalala, kila itapokuwa inapata taarifa zinazohusiana na makosa ya aina hii haitasita kuchukua hatua kama hii. Aidha tunaomba wananchi waendelee kutuunga mkono dhidi ya mapambano haya kwa kutupatia taarifa makini ili nchi yetu isigeuzwe kuwa ni kichaka cha maovu,” anasema Abdullah.

11303 Total Views 1 Views Today
||||| 10 I Like It! |||||
Sambaza!