Alhamis, Novemba mosi, 2018 inastahili kuwa siku ya kukumbukwa kutokana na lile tukio la Rais John Magufuli kushiriki kikamilifu mdahalo muhimu pale Chuo Kikuu cha Dar es salaam (Mlimani), katika ukumbi wa Nkrumah.

Nafikiri, mkuu wa nchi alijisikia yuko nyumbani kabisa, maana alitulia tulii na kuwasikiliza wasomi, maprofesa na watu wengine mashuhuri wakitoa “materials” zao pale.

Kwa maneno yake mwenyewe alisema, ninanukuu” “…Leo sikutegemea kuzungumza, nilipanga kuja kusikiliza tu na kijinoti changu. Nimeandika yote…”

Kilichonikosha sana mimi mpaka nikaamua kuandika makala hii ni kule kujiamini kwake mkuu huyu. Pamoja na ongea yake kana kwamba anatania, lakini alikuwa ameteka ukumbi wote wa Nkrumah siku ile.

Aliamua kuonesha Utanzania wake wa dhati tunaoita uzalendo, maana aliongea kwa lugha ya taifa – Kiswahili. Nina mnukuu, “… Chuo changu ninakipenda, nimesoma hapa na kukaa hapa…”

Kwa kujitambulisha vile mara moja unapata picha kuwa alijisikia ni mmoja wao, wala si mgeni aliyekuwa amealikwa kuhutubia na kisha kujibu maswali halafu yamekwisha, anajiondokea. Haikuwa hivyo. Yeye alifika akatuama kama maji ndani ya mtungi.

Kule kujieleza kuwa alisoma pale, alipata shahada yake ya kwanza pale, alifanya tasnifu yake palepale na maprofesa waliomtahini akawataja, kukawa hakuna mantiki kwa wanazuoni wale kusema kwanini hatumii ile lugha ya chuoni pale, “Kiingereza”.

Alidhihirisha Kiingererza anakimanya vizuri tu, vinginevyo mitihani yake angefanyaje hata kufaulu?

Inajulikana, shahada au hiyo tasnifu kamwe haviandikwi kwa Kiswahili, bali kwa lugha za chuoni hapo. Kwa maana hiyo alishawatangulia kimawazo (priemptied them) wale wasomi wote waliokitazamia kuwa Rais atamomboa, lakini basi waliambulia patupu.

Na aliwatania kwa kusema hataongea Kiingereza, maana yeye ni kielelezo cha utaifa na uzalendo. Wachina wako bilioni moja na nusu wanaongea Kichina, Warusi wanaongea Kirusi, Wajerumani kule kwao wanaongea Kijerumani. Hivyo Kiigereza si alama ya usomi! Ni lugha kama lugha nyingine, Kijaluo, Kikinga, Kilugulu na kadhalika; wala kutokujua Kiingereza haimaanishi mtu hakusoma au hana elimu –“period!”

Matamshi ya aina ile Rais wetu alipata kuyatamka kinaga ubaga kule Chuo cha Mkwawa, Iringa. Nako alifafanua vizuri kwanini hataongea hicho Kiingereza. Siyo kwamba eti hajui, la hasha bali ni katika kutuhimiza tuone fahari kwa lugha yetu ya taifa. Lugha ya nchi yoyote ndiyo kitambulisho (identity) kikubwa cha utaifa.

Mimi naona sasa Watanzania tumepata kiongozi mwenye uzalendo na mpenda Utanzania wake kwa dhati. Profesa Quorro alisema katika mada yake kuwa lugha ni chombo au nyenzo kuu ya mawasiliano na lugha ieleweke kwa pande zote mbili, msemaji na msikilizaji.

Profesa huyu alikwenda mbali ya hapa hata akasema tafiti zilizofanyika Afrika  zinasema moja ya sababu ya kutokuwa na maendeleo Afrika ni kule kuandaa mipango katika lugha ngeni za Ulaya/Uchina.

Naomba nimnukuu huyu Profesa Quorro pale aliposema, “…Baba wa Taifa alisema wasomi ni watu waliotumwa nchi nyingine wakienda kusoma wanarudi kwa jamiii kuwatafsiria kile walichokisoma, hivyo kila mtu afundishe kwa jamii kile walichosoma kwa Kiswahili…”

Dhana hii inamaanisha hao wasomi waendapo huko ng’ambo (overseas kama tunavyoita sisi wa zamani) kwenye nchi za Wazungu au Wachina kwanza walilazimika kujifunza lugha  mahalia – iwe Kijerumani, Kifaransa, Kirusi, Kibulgaria, Kinordic au Kichina. Baada ya kuimudu lugha ile mahalia ndipo wanasomea fani waliyoendea kule kwa kadri ya mitaala yao nchi husika. Wakishahitimu wanarudi sasa kutugawia sisi, Watanzania wenzao yale waliyovuna kwa lugha yetu ya Kiswahili tunanufaika na elimu ile.

Lakini baadhi ya wasomi wetu hao wakienda kule “majuu” basi wanajibadilisha na kuwa wa kule kule na kuchukia huku walikotoka hata wakirudi wanaona vigumu kutuelimisha sisi wenzao. Hapo ndipo wanageuka na kuwa vibaraka wa wageni. Baba wa Taifa alisema wanakuwa manokoa – kupenda kuwa kama mabwana wao vile wanaiga yale ya kule.

Jambo la pili, lililonikosha mimi ni kule kuweka wazi hali ya uchumi katika nchi yetu na jitihada za serikali kutujegea hali ya kujitegemea. Mheshimiwa Rais alisema leo hii Tanzania ina akiba (forex) ya fedha za kigeni dolari za Marekani bilioni 5.4

Haijapata kutokea tangu tupate Uhuru, kuwa na uwezo (sustainability) namna hii. Hii maana yake nchi yetu ina uwezo wa kununua vitu kutoka nje kwa muda wa miezi sita! Hili jambo la kujivunia. Kutokana na hali hiyo nchi inaanza kuheshmika.

Sasa kuona ufahari wa nchi ni kielelezo kimojawapo cha uzalendo. Nchi inaweza kulipa madeni na inaweza kujipangia maendeleo yake bila vikwazo vyovyote. Ni uamuzi wetu sisi wenyewe.

Hapa napenda niwaoneshe wasomaji namna Wazungu wakoloni Waingereza waliozuru kwa mara ya kwanza bara letu hili la Afrika walituonaje. Hapa nanukuu maneno ya Lord Macaulay alivyosema katika Bunge la Uingereza mwaka 1835. Mzungu huyu alisema hivi:-

“I have traveled across the length and breadth of Africa and I have not see one person who is a beggar, who is a thief such wealth I have seen In this country, such high moral values, people of such caliber, that I do not think we would ever conquer this country, unless webreak the very/ backbone of this nation, which is her spiritual and cultural heritage and therefore, I propose that we replace her old and ancient education system her culture, for if the Africans think that alf that is foreign and English is good and greater than their own, They will lose their selfesteem, their native culture and they will become what we want them, a truly dominated nation”.

Lord Macaulay ‘s Address to theBritish Parliament on 2nd Feb 1835

Hapo mnaona wazi kuwa sisi Waafrika tuliogopwa sana na Wazungu. Hatukuwa ombaomba, hatukujua wizi na tulijiamini sana katika mila na desturi zetu. Ili watutawale basi mkoloni yule aliwaomba wenzake ndani ya Bunge la Uingereza kwa maneno namna hii, “… Unless we break the very backbone of this nation…”

Hii ilikuwa na maana kutuondolea ule utu wetu (to dehumanize the Africans) ndipo watutawale kimawazo na kiuchumi ndiyo maana alisema, “… I propose that we replace her old and ancient education system, her culture for if the Africans think that all that is foreign and English is good and greater than their own, they will lose their esteem, their native culture and they will become what we want them – truly dominated nation…”

Hatua ya kwanza  ya unyanyasaji walitufanya watumwa, hatua ya pili wakavunja tawala zetu za kimila na baada ya hapo sasa wakatutawala na hatua ya tatu ndiyo wakatupakia kasumba za uzungu mpaka tukawa hoi hadi wasomi wengine zile enzi za ukoloni walidiriki kujiita wazungu-weusi.

Sasa kwa mpango wa wakoloni Waingereza, walitunga sera ya elimu kwa makoloni yao huku barani Afrika. Sera ile iliitwa “Education Policy For British Tropical Africa” ndiyo iliyotumika kwa Waafrika wote katika makoloni ya Waingereza barani Afrika.

Hapa kwetu mkurugenzi wa kwanza wa elimu aliyeitwa Bwana Stanley River-Smith alikuja mwaka 1920 na ndiye aliyesimamamia utekelezaji wa sera ile kwa Waafrika nchini Tanganyika.

Moja ya shabaha za elimu ya wakoloni kwa Waafrika ilisema hivi, nanukuu,

“…The central school, education was intended to uproot those who received it from their rural environment and transplant them into urban centers as wage earners and agents of the colonial economy and administration…” (Soma haya kutoka kitabu kiitwacho Education And Social Change in Rural Community by Z. E. Lawuo uk 55).

 Basi shabaha hii ni kama alivyosema yule Lord Macaulay huko nyuma, “Unless we break the backbone of their culture and make  think that all that is foreign and English is good and greater than their own we cannot change them.”

By Jamhuri